Waziri Mpina akutana na Taasisi za kusimamia Kemikali nchini

April 22, 2017

Bw. Justine Ngaile Mkurugenzi wa Kinga na Mionzi kutoka Tume ya Atomiki akiwasilisha mada kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Luhaga Mpina. Waziri Mpini alikutana na Taasisi zinazohusika na usimamizi wa kemikali kujadilili mkakati wa pamoja wa kusimamia kemikali nchini.
Baadhi ya wataalamu kutoka Taasisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Chakula na Dawa na Tume ya Nguvu za Atomiki wakifuatilia majadiliano na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina (hayupo pichani), kikao kazi hicho kimefanyika katika Ofisi ya Makamu wa Rais Dodoma.
Na Lulu Mussa
Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, hii leo amekutana na taasisi zizohusika na uratibu na usimamizi wa kemikali hapa nchini.
Akiongea na Taasisi hizo, Waziri Mpina amewaagiza watendaji hao kudhibiti na kusimamia kemikali hatarishi nchini ikiwa ni pamoja na kuratibu usafirishaji, usambazaji na matumizi ya kemikali hizo hapa nchini kwa namna bora zaidi.
Waziri Mpina amezitaka taasisi hizo kutoa taarifa za utendaji wa kazi kila robo ya mwaka kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimizi wa Mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira kifungu namba 170. “Nawaagiza kuwasilisha takwimu za kemikali zinazozalishwa nchini, zinazoagizwa au kusafirishwa nje ya nchi, pamoja na kuainisha viwanda vinavyozalisha kemikali vilivyosajiliwa na maghala yaliyosajiliwa kuhifadhi kemikali hizo” alisisitiza Mpina.
Katika kikao hicho Waziri Mpina pia ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini ndani ya miezi miwili kuandaa muongozo na kuupitisha katika hatua zote wa namna bora ya kuteketeza taka hatarishi bila kuathiri mazingira.
Aidha Waziri Mpina ameagiza kuandaliwa kwa andiko litakalobainisha umuhimu wa kuteketeza taka hatarishi. “Kama taifa ni lazima tuwe na “dedicated Incinerator” kubwa kutekeza taka hizo hatarishi kwa kuzingatia taka zinazozalishwa hapa nchini” Mpina alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini, Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania, Tume ya Nguvu za Atomiki, Taasisi ya Utafiti ya Viuatilifu katika Kanda za Kitropiki, Mamlaka ya Chakula na Dawa, OSHA na Mkemia Mkuu wa Serikali kwa pamoja wametakiwa kuanda Hati ya Makubaliano ya kuratibu utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuhuisha Sheria zao na kuleta mapendekezo Serikali ya vifungu vya kufanyiwa marekebisho.
Taasisi alizokutana nazo ni pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC), Taasisi ya Nguvu za Atomiki, Mamlaka ya Chakula na Dawa na Mkemia Mkuu wa Serikali.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »