Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Tanzania inatarajiwa kuwa nchi ya
kwanza barani Afrika kuwa na reli ya kisasa inayotumia umeme na mafuta
itakayokuwa na uwezo wa kusafiri masafa marefu kwa mwendokasi wa
kilometa 160 kwa saa.
Akizungumza katika uwekaji wa jiwe
la msingi wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo ya leo huko Pugu
nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa reli hiyo itakuwa ya
kisasa zaidi barani Afrika na itasaidia kukuza uchumi wa nchi kwa
kuchochea fursa za biashara ndani na nje ya nchi.
Awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli
hiyo ambayo itahusisha kipande cha kilomita 300 kutoka Dar es Salaam
hadi Morogoro utagharimu jumla ya shilingi trilioni 2.8 na utatarajiwa
kukamilika katika kipindi cha miezi 30.
Dkt Magufuli alitoa mfano wa nchi
zenye reli za mwendokasi lakini masafa mafupi barani Afrika kuwa ni
Morocco ambayo inasafiri kwa mwendokasi wa kilomita 220 kwa saa na
Afrika Kusini inayosafiri mwendokasi 150 kwa saa.
Dkt Magufuli alieleza kuwa baada
ya kukamilika kwa mradi huo Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kuwa na
treni itakayosafiri masafa marefu kwa mwendokasi wa km 160 kwa saa.
Alifananua kuwa mradi huo wa
ujenzi wa reli unatekelezwa kwa fedha za Tanzania ambapo tayari serikali
imeshawalipa wakandarasi malipo ya awamu ya jumla ya shilingi bilioni
300.
Akizungumzia umuhimu wa ujenzi wa
reli hiyo, Rais Magufuli alisema kuwa reli hiyo itasaidia kuongeza kasi
ya usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwa haraka na
kuwafikia wateja ndani ya muda mfupi.
Vilevile, reli hiyo itarahisisha
usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na kukuza biashara kati ya
Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Uganda,
Burundi, Rwanda na Sudani ya Kusini.
Sambamba na hayo, Rais Magufuli
alisema kuwa ujenzi wa reli hiyo utasaidia kuimarisha sekta nyingine za
uchumi ikiwemo utalii, viwanda, kilimo, pamoja na kutoa ajira kwa
watanzania ambapo kutakuwa na ajira muda zipatazo 600,000, na ajira za
kudumu 30,000.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema kuwa reli hiyo
ya kisasa inayojengwa na wakandarasi kutoka muungano wa kampuni mbili
za nchi ya Uturuki na Ureno itakuwa na uwezo wa kusafirisha mizigo
tani 10,000 kwa mara moja na kutumia saa 2 kutoka Dar es salaam hadi
Dodoma na saa 7 na dakika 40 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Naye, Mjumbe wa Bodi ya Kampuni ya
ujenzi kutoka Uturuki ya Yapi Merkezi Bw. Emre Aykar alisema kuwa reli
hiyo itaimarisha zaidi uhusiano wa Uturuki na Tanzania na kuongeza
kiwango cha shughuli za biashara nchini.
“Tunaahidi kujitahidi kumaliza mradi kwa wakati na katika kiwango kinachotakiwa” alisema Bwana Aykar.
Reli hiyo ya kisasa inatarajiwa
kujengwa pembeni ya reli ya kati ambayo ilijengwa wakati wa utawala wa
kikoloni wa Wajerumani na Waingereza miaka 112 iliyopita.
EmoticonEmoticon