MKUU wa wilaya ya Muheza Mkoani Tanga,Mhandisi Mwanasha Tumbo amesema hajaridhishwa na hali ya ufaulu kwa shule za msingi na sekondari wilayani humo kwa kuwataka walimu ambao shule zao zitafanya vibaya wawajibishwe.
DC Mwanasha aliyasema hayo mwishoni mwa wiki ambapo alisema licha ya kutambua zipo changamoto mbalimbali lakini sio sababu inayoweza kuchangia hali hiyo .
Alisema wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya ambazo zina historia kubwa kwa elimu hapa nchini hivyo wanapaswa kuienzi kwa wanafunzi kufanya vizuri ili kuweza kuinua kiwango cha taaluma kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Nafahamu zipo changamoto mbalimbali ikiwemo za elimu lakini suala hilo linafanyiwa kazi na serikali ili kuona namna ya kulipatia ufumbuzi kama jamii ni sehemu ya elimu tushirikiane jinsi ya kuboresha miundombinu “Alisema.
Hata hivyo aliitaka jamii kuwafichua watoto wenye ulemavu ambao wamekuwa wakihifadhiwa majumbani na kushindwa kupata elimu ili waweze kupatiwa elimu ambayo inaweza kuwasaidia kukabiliana na maisha yao ya baadae.
“Tusiwafiche watoto wenye mahitaji maalumu majumbani badala yake tuone jinsi ya kuwapeleka shuleni ili waweze kupata elimu bora ambayo inaweza kuwasaidia maishani”Alisema.
Naye kwa upande wake,Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya
Muheza,Julita Akko alisema wao wapo kwenye mikakati ya kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinaongezeka licha ya kukabiliwa na uhaba wa upungufu wa miundombinu.
Alisema licha ya hivyo wanakabiiliwa pia na uhaba wa vifaa vya
kujifunzia kwa shule za msingi na sekondari hasa kwenye masomo ya sayansi na hisabati.
EmoticonEmoticon