Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika benchi la kibanda cha
kupigia kiwi (Shoe Shine) pamoja na wakazi wengine wa Chato katika eneo
maarufu kama Stendi za zamani Chato mkoani Geita. Kibanda hicho cha Kiwi
ndicho Rais Dkt. Magufuli alichokuwa akisafishiwa viatu vyake kabla ya
kuwa Rais, pia ni sehemu ambayo alikuwa akipenda kukaa na
kubadilishana mawazo na wakazi wa Chato wakati akiwa mapumzikoni kipindi
cha Nyuma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia pamoja na wanafunzi wa
Shule ya Msingi Chato mkoani Geita. Shule hiyo ya Msingi Chato ndiyo
Rais Dkt. Magufuli alisoma kuanzia darasa la kwanza mpaka Darasa la
Saba. Rais Dkt. Magufuli amewaasa Wanafunzi hao kusoma kwa bidii
kwasababu yeye pia alisoma shuleni hapo. Picha na Mpigapicha Maalum.
…………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 9 Januari, 2017 amefanya
ziara ya kushtukiza katika Shule ya Msingi Chato,ambapo ndipo aliposoma
kuanzia darasa la kwanza hadi la saba na kuzungumza na walimu na
wanafunzi wa shule hiyo.
Rais Dkt Magufuli ameahidi
kujenga madarasa matatu na ofisi moja ya walimu katika Shule hiyo
kufuatia ombi la Walimu kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba
vya madarasa ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaosoma shuleni
hapo.
Aidha Dkt.Magufuli amewaasa
wanafunzi kutilia mkazo masomo ili waweze kufaulu na kuwataka walimu
kuhakikisha wanatumia vyema fedha zinazotolewa na Serikali kila
mwezi katika kutoa elimu bila malipo na pasiwe na wanafunzi hewa kama
ilivyo kwa baadhi ya shule ambazo zimegundulika kuwa na wanafunzi hewa
katika uhakiki uliofanywa na serikali.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa
Shule ya Msingi Chato, Bwana Mwita Chacha amemshukuru Rais Dkt.Magufuli
kwa msaada aliowapatia katika kukabiliana na uhaba wa madarasa uliokuwa
unaikumba shule hiyo, pia kuitembelea Shule yao jambo ambalo
limewatia moyo walimu na wanafunzi shuleni hapo.
Rais Magufuli pia ametembelea
eneo la Stand ya zamani na kuzungumza na baadhi ya wananchi waliokuwepo
eneo hilo na kutoa msaada kwa kikundi cha wasafisha viatu ili kuongeza
mtaji wa biashara yao.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita.
9 Januari, 2017
EmoticonEmoticon