Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
05 Desemba, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko
ya Afrika wa Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Boeing yenye makao
yake nchini Marekani Bw. Jim Deboo ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali
za kununua ndege kubwa kutoka kampuni hiyo.
Mazungumzo
hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu
Mkuu Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bw. Doto James.
Baada
ya Mazungumzo hayo Rais Magufuli amesema Serikali yake ya Awamu ya Tano
imedhamiria kununua ndege nyingine nne zikiwemo ndege kubwa 3 ambazo
zitasaidia kuinua uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja hapa nchini
moja kwa moja kutoka nchi zao.
"Sisi
hapa tunazungumza kuwa watalii hawajafika hata milioni 2 kwa mwaka,
lakini nchi kama Morocco inapata watalii zaidi ya milioni 12 kwa mwaka,
hii yote ni kwa sababu hatuna mashirika ya ndege ya kwetu, watalii
wakitaka kuja hapa ni lazima waje kwa kuungaunga, wafikie nchi nyingine
halafu ndipo wapate moyo wa kuja huku, licha ya kwamba sisi Tanzania ni
miongoni mwa nchi 5 duniani zenye maeneo mazuri yenye utalii.
"Kwa
hiyo niwaombe tu Watanzania wapende mali zao, kwa sababu wakati
mwingine nikiangalia mitandao na magazeti ni ajabu huwezi kuamini kama
hao ni Watanzania, unakuta wanasifia tu ndege za watu wengine na wanazibeza za kwao" amesisitiza Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli ametaja aina ya ndege mpya ambazo Serikali itazinunua
kuwa ni ndege 1 aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kufika
nchini Mwezi Juni 2017, ndege 2 aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa
kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini
kati ya Mei na Juni, 2018 na ndege moja aina ya Boeing 787 Dash 8 Dream
Liner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 na inayotarajiwa kuwasili
nchini Juni, 2018. Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika.
Dkt.
Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi za Serikali
zenye lengo la kuinua utalii na kuimarisha uchumi wa nchi.
"Tumeleta
ndege aina ya Bombardier hapa, zimepunguza gharama za safari mfano
kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, sasa wanalipa kati ya 160,000/ hadi
200,000/- wakati nauli ilishafika Shilingi laki 8 na kitu, lakini watu
wengine utakuta wanazungumzazungumza wee maneno ya hovyo kwa kutumiwa,
tumeshaamua na tutafanya hivyo" amesisitiza Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Rais
Magufuli ameagana na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika hapa nchini (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero ambaye amepandishwa
cheo na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
Ukanda wa Kusini mwa Afrika katika ofisi zake zilizopo Afrika Kusini.
Rais
Magufuli amemshukuru Dkt. Tonia Kandiero kwa juhudi kubwa alizozifanya
akiwa Mwakilishi Mkazi wa AfDB hapa nchini ambapo miradi mikubwa na
muhimu katika maendeleo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa.
Akizungumza
baada ya kuagana na Rais Magufuli Dkt. Tonia Kandiero amemshukuru Rais
Magufuli na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano alioupata katika
kipindi cha miaka 6 aliyokuwa hapa nchini na amesema anaondoka akiwa
ameiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa ya kimahusiano na AfDB ambapo
miradi yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni imetekelezwa hususani
katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Katika hatua nyingine, Rais
Magufuli ameagana na Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe. Jorge Luis Lopez
Tormo anayemaliza muda wake baada ya kuiwakilisha nchi ya Cuba kwa miaka
minne.
Rais
Magufuli amemshukuru Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo kwa uhusiano na
ushirikiano mzuri aliouendeleza kati ya Tanzania na Cuba uliojengwa na
waasisi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa
Tanzania na Mhe. Fidel Castro wa Cuba.
Mhe.
Jorge Luis Lopez Tormo amemshukuru Rais Magufuli na Serikali kwa
kuendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Cuba
na amesema anaondoka akiwa anaamini kuwa uhusiano kati ya nchi hizi
utaendelea kuwanufaisha wananchi ikiwemo miradi mikubwa ya maendeleo na
huduma za kijamii.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Desemba, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni ya Ndege ya Boeing Jim
Deboo aliyefika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo pamoja na ujumbe wake.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitazama
kitabu cha picha ya ndege aina ya Boeing 787-8 Dream liner wakati
alipokuwa akisikiliza maelezo yake kutoka kwa Mkurugenzi wa mauzo wa
kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo. Ndege hiyo itakuwa na uwezo wa
kubeba abiria 262 na itakuwa na uwezo wa kuruka kutoka nchini Marekani
hadi Tanzania bila kutua mahali popote.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru
Mkurugenzi wa mauzo wa Kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo mara baada
ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto
ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Doto James na anayefuatia ni Katibu
Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
kuhusiana na ununuzi wa ndege hiyo mpya aina ya Boeing 787-8 Dream
liner mara baada ya kumaliza mazungumzo na Mkurugenzi wa mauzo wa
Kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Balozi wa Cuba anayemaliza muda wake nchini George Luis
Lopez Tormo aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na Balozi wa Cuba anayemaliza muda wake hapa nchini George Luis Lopez
Tormo aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na
Balozi wa Cuba anayemaliza muda wake hapa nchini George Luis Lopez
Tormo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
Dkt. Tonia Kandiero aliyefika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo. Dkt. Tonia
ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
katika Ukanda wa Kusini Mwa Afrika katika Ofisi zake zilizopo Afrika ya
Kusini
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana
na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia
Kandiero ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo na kuagana na Mhe.
Rais Dkt. Magufuli. Dkt. Tonia ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki
ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Ukanda wa Kusini Mwa Afrika katika
Ofisi zake zilizopo Afrika ya Kusini
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akijadiliana jambo na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) Dkt. Tonia Kandiero ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya
mazungumzo.Dkt. Tonia Kandiero ameteuliwakuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki
ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Ukanda wa Kusini Mwa Afrika katika
Ofisi zake zilizopo Afrika ya Kusini PICHA NA IKULU
EmoticonEmoticon