Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mgeni wake
Makamu wa Rais wa Cuba Mh. Salvador Valdes Mesa wakati alipokutana naye
Ikuu leo kwa mazungumzo ambapo wamezungumzia jitihada za Serikali hizi
mbili ya Cuba na Tanzania katika kuendelea kuimarisha na kudumisha
mahusiano mazuri yaliyopo kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi
mbili.(PICHA KWA HISANI YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mgeni wake Makamu wa
Rais wa Cuba Mh. Salvador Valdes Mesa wakiwa katika picha ya pamoja na
baadhi ya viongozi wa Tanzania na Cuba.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi zawadi ya
picha ya mnyama Chui anayepatikana katika mbuga za wanyama za Tanzania
Mgeni wake Makamu wa Rais wa Cuba Mh. Salvador Valdes Mesa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya picha
kutoka kwa Mgeni wake Makamu wa Rais wa Cuba Mh. Salvador Valdes Mesa ,
Kulia ni Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa.
……………………………………………………………………………………
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali ya Tanzania na Cuba
zimeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo, ambao umeasisiwa na viongozi
wa mataifa hayo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania pamoja na
Fidel Castro Rais mstaafu wa Cuba.
Akizungumza na waandishi wa
habari, Ikulu leo jijini Dar es salaam, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu, amesema kuwa Makamu wa Rais wa
Cuba, Mhe. Salvador Valdes Mesa ameitikia mwaliko huo wa kuja nchini
kwa vile nchi hizo mbili zimekua na ushirikiano na mahusiano mazuri kwa
muda mrefu.
“Ziara hii ni moja ya jitihada za
Serikali hizi mbili ya Cuba na Tanzania katika kuendelea kuimarisha na
kudumisha mahusiano mazuri yaliyopo kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi
mbili ili kuhakikisha mahusiano yaliyopo yanaimarika zaidi” alisema
Makamu wa Rais
Katika ziara hiyo ya Makamu wa
Rais wa Cuba nchini, mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwemo masuala ya
Afya, Elimu, Michezo, na Utamaduni, ambapo katika sekta ya afya nchi ya
Cuba imepiga hatua na kuahidi kushirikiana na Tanzania ili kujenga
kiwanda cha kisasa cha kutengeneza madawa ya binadamu.
Aliongeza kuwa Tanzania imeomba
Serikali ya |Cuba kuendelea kusaidia sekta hiyo kwa kufundisha wataalamu
wa afya, ambapo tayari madaktari 24 kutoka Cuba wako nchini kwa ajili
ya kusaidia kutoa huduma za kitabibu na mafunzo katika mikoa
mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani.
Masuala mengine yaliyojadiliwa katika ziara hiyo ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya elimu, biashara, utalii na uwekezaji.
Ambapo pia Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Suluhu amesisitiza nia ya Serikali
ya Tanzania kudumisha ushirikiano huo ikiwa ni pamoja kupongeza jitihada
za kuboresha uhusiano wa Cuba na Marekani.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais
wa Cuba, Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa ameishukuru Serikali ya
Tanzania kwa kuendelea kuonesha ushirikiano kwa nchi yake na kuahidi
kuendelea kutoa msaada kwa Tanzania.
“Tumeamua kuendelea kuboresha
mahusiano yetu na Tanzania kwa kuongeza ushirikiano wetu katika sekta
nyingine ambazo hatukuwa tunashirikiana hapo awali kama vile sekta ya
utalii” alisema Makamu wa Rais wa Cuba
Aidha, Mhe. Mesa ameiomba
Tanzania kuendelea kuiunga mkono Cuba katika masuala ya kimataifa ili
kuendeleza ushirikiano na kukuza uchumi kwa nchi zote mbili.
Makamu wa Rais wa Cuba aliwasili
nchini jana jioni kwa ziara ya siku tatu ambapo alipata fursa ya
kuonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John
Magufuli .
EmoticonEmoticon