Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
amesema kwamba ataendelea kuwa karibu na vijana na Timu ya Tanzania ya
vijana ‘Serengeti Boys’ licha ya kuondolewa na Congo kwenye harakati za
kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika
Madagascar, hapo Aprili, mwakani.
Mipango ya TFF kwa sasa inayoongozwa na Malinzi kwa sasa ni
kuiiingiza timu hiyo kwenye program ya timu ya vijana wenye umri wa
chini ya miaka 20 maarufu kwa jina la Ngorongoro Heroes baada ya kuguswa
na kilio cha vijana hao ambao walishindwa kujizuia kumwaga machozi
mbele ya Malinzi ambaye alifanya kazi kubwa kuwatuliza pamoja na
viongozi wengine.
Serengeti Boys ilipoteza mchezo dhidi ya Congo Oktoba 2, 2016. Kwa
kupoteza mchezo huo dakika ya pili kati ya nne ya nyongeza baada ya
kumalizika kwa dakika 90, kumefanya vijana hao wa Tanzania kuenguliwa
kwenye mashindano ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika – fainali zitakazofanyika Madagascar.
Dakika moja ndiyo iliyoipoteza Serengeti Boys kufuzu kwa fainali hizo
kwa bao la dakika ya 92 la lililofungwa na Mountou Edoward.
“Niko nanyi, najua mna group la WhatsApp, naomba msifute namba yangu.
Iwe humo na mambo yenu mengi naomba mniambie humo, na nitayashughulikia
iwe binafsi au kiofisi. Nawahakikishia sitawaacha,” alisema Malinzi
alipowafariji vijana hao ambao wanatarajiwa kuingia leo saa 3.00 usiku
huu kwa ndege ya Shirika la Ndege ya Rwanda.
“Umri wenu bado sana wa kucheza soka. Program za TFF, CAF na FIFA
ziko nyingi pia mnaweza kupata nafasi ya kucheza Olimpiki na kuna
michuano mingi, sitawaacha,” alisema Malinzi na kusisitiza ana imani na
timu hiyo ambayo kwa dakika 90 za mchezo dhidi ya Congo walipambana
kwelikweli kutetea taifa lao pendwa Tanzania.
EmoticonEmoticon