WAZIRI MBARAWA AZITAKA TAASISI ZA SEKTA BINAFSI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KATIKA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA VIWANDA

July 05, 2016

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Makame Mbarawa amezitaka Taasisi za Sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kukuza uchumi wa viwanda.

Amezitaka sekta hizo kutumia fursa za uwekezaji zinazotolewa na Serikali kama vile ujenzi wa reli ya kati, njia ya magari ya haraka (Dar- Chalinze express way) na upanuzi wa viwanja vya ndege mbalimbali nchini.

Ametoa pendekezo hilo jijini Dar es salaam wakati akifungua semina ya wataalamu wa Tanzania na China katika kujadili namna bora ya kuboresha miundombinu ya viwanda.

“Naamini kwamba serikali pamoja na Taasisi hizi zikishirikaiana kwa pamoja zitaweza kuboresha viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020”, amesema Waziri Mbarawa.

Aidha, amewataka wadau kutumia fursa hiyo katika kujifunza na kuiga mbinu mbalimbali zinazotumiwa na nchi ya China ambayo imeendelea katika sekta ya viwanda mara baada ya kumalizika kwa semina hiyo.

Amefafanua kuwa kupitia uboreshwaji wa viwanda nchini, Serikali inatarajia kuongeza pato kutokana na ushindani wa kibiashara ambao utafanywa na wawekezaji kutoka nchi hizo mbili hususani katika masuala ya miundombinu.

“Tunakaribisha wawekezaji wengi kutoka China ambao wataleta mapinduzi ya viwanda nchini kwetu na hivyo kukuza uchumi na pato kwa ujumla”, amesisitiza Mbarawa.

Amesema kuwa suala la kuboresha viwanda linaenda sambamba na utunzaji wa mazingira kwani viwanda vingi vimekuwa vikileta athari katika afya ya mwanadamu.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Mhe. Dkt. Suzan Kolimba, ameipongeza Serikali ya China kuichagua Tanzania kuwa ni nchi ya kwanza kuifanyia utafiti wa kujadili uboreshaji wa viwanda Afrika na kuahidi kutoa ushirikiano ili kutekeleza maendeleo chanya.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Lu Youqing, amesema kuwa kutokana na ushirikiano wa karibu uliopo baina ya Serikali ya China na Tanzania anaamini kuwa wadau wa nchi hizo mbili watashirikiana kikamilifu katika kuwekeza na kuboresha viwanda nchini ili kuongeza uzalishaji.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifungua mkutano wa Uwezeshaji viwanda baina ya China na nchi za Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam leo (jana), wa pili kutoka kulia ni Balozi wa China nchini Dr.Lu Youqing.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akizungumza jambo na Balozi wa China nchini Dr.Lu Youqing wakati wa mkutano wa Uwezeshaji viwanda baina ya China na nchi za Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya Wajumbe wa mkutano wa Uwezeshaji viwanda baina ya China na nchi za Afrika wakifuatilia hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), katika mkutano wa Uwezeshaji viwanda baina ya China na nchi za Afrika.
Balozi wa China nchini Dr.Lu Youqing kulia akiongea na mmoja wa wajumbe wa mkutano huo Prof. Ibrahim Lipumba mara baada ya ufunguzi wa mkutano wa uwezeshaji viwanda baina ya China na nchi za Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam leo .
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa kushoto akiongea na mjumbe wa mkutano huo mara baada ya ufunguzi wa mkutano wa Uwezeshaji viwanda baina ya China na nchi za Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam leo .
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa kushoto akifurahia jambo na Prof. Ibrahimu Lipumba mjumbe wa mkutano wa Uwezeshaji viwanda baina ya China na nchi za Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.katikati ni Balozi wa China nchini Dr.Lu Youqing.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa tano kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa mkutano wa Uwezeshaji viwanda baina ya China na nchi za Afrika. Picha na Benjamini Sawe-Maelezo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »