KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YAKAGUA MIRADI YA UMEME VIJIJINI MKOANI NJOMBE

April 06, 2016

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wameendelea na ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Wizara husika ambapo mwishoni mwa wiki hii walitembelea miradi ya umeme vijijini, mkoani Njombe.

Miradi waliyotembelea Wajumbe hao ni pamoja na wa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Makambako hadi Songea na usambazaji umeme kwenye vijiji vya mikoa ya Njombe na Ruvuma.

Vilevile, Kamati ilitembelea maeneo ya vijiji mbalimbali mkoani Njombe ambako miradi ya umeme vijijini inatekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.

Aidha, Kamati ilipata fursa kuzungumza na baadhi ya wananchi wa vijiji husika ambako miradi hiyo ya umeme inatekelezwa na kusikiliza maoni yao.

Baada ya ziara mkoani Njombe, Kamati hiyo itatembelea Mkoa wa Mbeya, eneo la Kiwira katika Mradi wa Makaa ya Mawe na baadaye itaelekea Biharamulo kukagua mgodi wa dhahabu wa Tulawaka.

Awali, Kamati ilifanya ziara mkoani Mtwara ambapo ilitembelea Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Madimba pamoja na Kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Dangote. Pia, Wajumbe wa Kamati hiyo walitembelea machimbo ya Tanzanite yaliyopo Mirerani mkoani Manyara.
Mkandarasi anayesambaza umeme vijijini kwa Mkoa wa Njombe, kutoka Kampuni ya Lucky Exports Ltd (wa tatu kutoka kushoto), akimwonesha na kumpa maelezo kuhusu transfoma iliyofungwa katika Kijiji cha Isindagosi – Njombe, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Ussi Pondeza, wakati wa ziara ya kamati hiyo mkoani humo hivi karibuni kukagua miradi ya umeme vijijini.
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Njombe, Mhandisi Emmanuel Kachewa (mwenye suti ya bluu-kushoto), akiwapa maelezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kuhusu sehemu ya kuchukulia umeme (taping point) iliyopo kijiji cha Italahumba – Njombe, wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua miradi ya umeme vijijini mkoani humo hivi karibuni.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Njombe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Anatory Choya, akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Mkoa wake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, walipotembelea mkoani humo hivi karibuni kukagua utekelezwaji wa miradi ya umeme vijijini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe (wa pili kutoka kulia) akijadiliana jambo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anatory Choya (kulia), wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani), mkoani humo hivi karibuni, kukagua utekelezwaji wa miradi ya umeme vijijini. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje.
Mwananchi kutoka Kijiji cha Ihanzutwa – Njombe, Karison Mgoba akitoa maoni yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kuhusu utekelezwaji wa miradi ya umeme vijijini, hususan katika kijiji chake.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakiwa katika ziara kukagua miradi ya umeme vijijini mkoani Njombe hivi karibuni.
Meneja wa Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Umeme wa Msongo wa Kilovolti 220 kutoka Makambako hadi Songea, Mhandisi Didas Lyamuya, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipokuwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kabla ya kutembelea miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa mkoani humo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Ussi Pondeza, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Isindagosi – Njombe kuhusu miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa mkoani humo, wakati wa ziara ya Kamati hiyo hivi karibuni. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe.
Mmoja wa wananchi katika kijiji cha Isindagosi – Njombe, akitoa maoni yake kuhusu utekelezwaji wa miradi ya umeme vijijini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara mkoani humo hivi karibuni kutembelea miradi ya umeme vijijini.
Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Nishati na Madini wakiwaongoza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kutembelea miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa mkoani Njombe hivi karibuni.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »