Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe.Dkt John Magufuli akisaini makubaliano ya kuikaribisha
Sudan kusini katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais wa Jamhuri ya Sudan kusini
Mhe. Salva Kiir akisaini hati za makubaliano ya kuikaribisha rasmi
Sudan kusini kuwa Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe.Dkt John Magufuli akizungumza wakati wa kumkaribisha Rais
wa Jamhuri ya Sudan kusini Mhe. Salva Kiir Salaam katika ziara yake ya
kikazi lenye dhumuni la kujiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais wa Jamhuri ya Sudan kusini
Mhe. Salva kiir akiagana na Jaji Mkuu wa Tanzania jaji O5thman Chabde
mara baada ya kumaliza kutia saini ya makubaliano ya nchi yake kujiunga
na jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe.Dkt John Magufuli akiaga viongozi mbalimbali wa ikiatifa na
kimataifa mara baada ya kumaliza kutia saini ya makubaliano ya nchi ya
Sudan Kusini kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki.
………………………………………………………………………………………………..
Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Sudani ya
Kusini Salva Kiiri ametia saini makubaliano ya mkataba wa kujiunga
rasmi na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki katika hafla iliyofanyika leo
Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kutia saini
mkataba huo, Rais Salva Kiiri amesema uamuzi wa nchi yake kujiunga na
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki si tu kuwa kunaimarisha ujirani ulipo
kati ya nchi hizo, lakini pia kunaimarisha ushirikiano wa Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki pamoja na watu wake ikiwa ni pamoja na kuendelea
kukuza utamaduni wa Afrika.
“Naishukuru Jumuiya ya Afrika ya
Mashariki kwa kukubali Sudani ya Kusini kuwa mwanachama wa Jumuiya, na
sasa Sudani ya Kusini imepata sehemu sahihi kwa kujiunga na Jumuiya hii
ambayo inalenga kuleta maendeleo kwa wananchi wake” amesema Rais Kiir.
Rais Kiir amesema “tunajua
malengo makubwa ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ni kuleta maendeleo
kwa wananchi wake, na tunashuhudia kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni
mfani bora Afrika na duniani kwa ujumla”.
Ameongeza kuwa Sudani ya Kusini
imeona fursa zilizopo katika Jumuiya hii ikiwa ni pamoja na soko la
pamoja (Common markert). Tayari tumetengeneza mifumo itakayosaidia
ushiriki wetu katika Jumuiya ikiwemo kuanzishwa kwa Wizara
itakayoshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ikiwa ni
pamoja na kutunga sheria mbalimbali zitakazowezesha kupatikana kwa Amani
ya kudumu nchini humo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amepongeza juhudi
zilizofanywa na Sudani ya Kusini na hatimaye kujiunga na Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki ikiwa ni muda mfupi tu tangu nchi hiyo ipate uhuru
wake mnamo Julai 20, 2012.
Rais Magufuli amesema kuwa siku
zote Sudani ya Kusini imekuwa sehemu ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
kwa uchumi wake, utamaduni wake, lugha pamoja na historia yake na
inaunganishwa na nchi za Jumiya hii kwa barabara pamoja na mto Nile.
Aidha, Rais Magufuli “amesema
malengo ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ni pamoja na kukuza biashara
na uwekezaji, kutoa bure huduma na uhuru wa wananchi kwenda popote ndani
ya Jumuiya. Hata hivyo, Jumuiya hii inakumbwa na machafuko ya mara kwa
mara na kuwa kikwazo kwa maendeleo ya uchumi wake”.
Amesema Sudani ya Kusini
imekubaliwa kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa kuwa
imetimiza makubalino yaliyowekwa na Jumuiya ikiwemo kuunda serikali ya
umoja wa kitaifa.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ambaye ni Waziri wa Mambo ya
Nje, Ushirikiano wa Afika ya Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi,
Dkt. Augustine Mahiga, amesema kuwa Sudani ya Kusini inakuwa mwanachama
wa sita wa Jumuiya hiyo, na kuwa ushirikiano wa kiuchumi uliopo katika
nchi hizi utakuwa mfano wa kuigwa kwa nchi zinazoendelea.
Sudani ya Kusini iliomba kujiunga
na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki mnamo Novemba 10, 2012, ikiwa ni
chini ya miezi minne tangu nchi hiyo ipate uhuru wake.