VIJANA wilayani Mkinga Mkoani Tanga wametakiwa
kujikita kwenye kilimo ili waweze kupata mafanikio makubwa badala ya kukaa
vijiweni ambapo hutumia muda mwingi kufikiria kufanya vitendo viovu badala yake
wahakikisha wanashiriki katika shughuli za uzalishaji ili waweze kuchangia
ukuaji wa maendeleo yao.
Mkuu wa wilaya ya Mkinga,Mboni Mgaza aliyasema
hayo juzi wakati ziara yake iliyolenga kuhamasisha shughuli za kilimo ambapo
alisema endapo vijana hao watatumia muda wao kwenye kilimo itawasaidia kuweza
kujikwamua kiuchumi.
Alisema kuwa vijana hao wanapaswa
kubadilika na kuona umuhimu wa kuwajibika hasa wakati huu ambao wananchi
wilayani humo wanaweka msukumo kwenye kilimo kwa kushiriki shughuli hizo kwa
umakini mkubwa.
“Unajua vijana ndio nguvu kazi kubwa kwa Taifa letu hivyo niwaase badala
ya kukaa vijiweni na kucheza pool table wakati wa kazi watumie nafasi hiyo
kwenye kilimo ambacho ndio ute wa mgongo kwa maendeleo ya nchi “Alisema
Aidha ili kuhakikisha jambo hilo
linapata mafanikio makubwa aliwaagiza maafisa ugani kuacha kukaa maofisini
badala yake wawafuate wakulima kwa ajili ya kuwapa utaalamu wa kilimo ili
waweze kulima kisasa.
Sambamba na hayo mkuu huyo wa wilaya
aliwataka maafisa ugani kuona umuhimu wa kwenda vijijini na kuacha kukaa
maofisini ili waweze kutoa mbinu kwa wakulima waweze kulima kilimo chenye tija
kwao.
Hata hivyo pia aliwataka wananchi
kubadilika na kulima kilimo cha kisasa ikiwemo kuandaa mashamba yao sambamba na
kupanda kisasa ili kupata mavuno mengi hali itakayowasaidia kukuza vipato vyao.