Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akijadiliana
jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Amos Makala walipokutana mjini
Moshi kwa ziara ya ukaguzi wa miradi iliyo chini ya sekta ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano.
Mkuu
wa Wilaya ya Same Bw. Herman Kapufi akisisitiza jambo kwa wafanyakazi
wanaofanya kazi katika kampuni ya Dott Services Limited inayojenga
barabara ya Same-Mkumbara Km 96. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa wafanyakazi wa kampuni ya Dott Services Limited kuhusu
madai yao ambapo ameagiza waanze kulipwa madai yao baada ya siku mbili.
wafanyakazi
wa kampuni ya Dott Services Limited wakishangilia kwa furaha baada ya
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa kumtaka
mkandarasi kuwalipa madai yao yote ifikapo Februari 26, mwaka huu.
Muoneano wa Jengo la Kituo cha Forodha cha pamoja (One Stop Border Post) kwa upande wa Tanzania lililopo Holili.
Ujumbe
wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
ukielekea katika kituo cha pamoja cha forodha (One Stop Border Post) kwa
upande wa Taveta nchini Kenya.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipata
ufafanuzi wa namna ya kituo cha pamoja cha Forodha kinavyofanya kazi
kutoka kwa Meneja Forodha kwa upande wa Taveta – Kenya Bw. Daniel
Nyambaka.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiagana na
Meneja Forodha kwa upande wa Taveta – Kenya Bw. Daniel Nyambaka mara
baada ya kukagua kituo hicho.
SERIKALI imesema iko mbioni kukamilisha mkataba maalumu wa ajira
utakaotumiwa na makandarasi wote nchini katika kuajiri watanzania
wazalendo kwenye miradi ya ujenzi inayosimamiwa na sekta ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasilino.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
amesema hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Mkumbara-Same yenye
urefu wa Km 96 mkoani Kilimanjaro.
Amemtaka mkandarasi Dott Services Limited kukamilisha hatua za
mwisho za ujenzi wa barabara hiyo na kulipa stahili zote za wafanyakazi
kwa mujibu wa mikataba.
“Nakupa mwezi mmoja kukamilisha ujenzi uliobaki wa barabara hii
pia hakikisha kila mfanyakazi ambaye amemaliza mkataba wake analipwa
stahili zake zote kwa muda usiozidi siku mbili”, amesisitiza Prof.
Mbarawa.
Prof. Mbarawa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Same Bw. Herman Kapufi
kufatilia kwa makini madai ya wafanyakazi wazalendo ya malipo ya likizo,
mafao ya NSSF, malimbikizo ya mishahara, matibabu na mazingira magumu
ya kazi ili yalipwe sambasamba na madai mengine na hivyo kuondoa
malalakimiko yaliyopo na yanayoweza kujitokeza mara baada ya kukamilika
kwa mradi.
“Kuanzia sasa mameneja wa TANROADS wahakikishe kwenye ujenzi wa
barabara na miradi iliyo chini ya wizara hii kazi ambazo watanzania
wanaweza kuzifanya zisifanywe na wageni kwani hali hiyo huwanyima haki
watanzania wenye ujuzi wa kuijenga nchi yao”, amesema Waziri Prof.
Mbarawa.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa
Kilimanjaro Eng. Marwa Rubirya amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa kwa
sasa km 1,020 za mtandao wa barabara wilayani Same zinapitika na
serikali imeanza kuongeza kiwango cha barabara za lami Wilayani humo
ikiwemo ujenzi wa barabara ya Same-Kisiwani-Maore-Ndungu na Kihuriyo
hadi Mkomazi.
Amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kwamba TANROADS itaendelea
kuhakikisha barabara za milimani wilayani Same ambazo ni sawa na
asilimia 75 ya barabara zote wilayani humo zinapitika wakati wote wa
mwaka kutokana na umuhimu wake kwa shughuli za kiuchumi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Same Bw. Herman Kapufi amemuomba Waziri
Mbarawa kuzipandisha hadhi barabara za Hedaru-Vunta-Miamba Km 41.2,
Bangarara-Chome-Ikokoa Km 25.6, na Ndungu-Lugulu Km 8 ili zihudumiwe na
TANROADS kutokana na umuhimu wake kiuchumi na kijiografia.
Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amekagua kituo cha pamoja cha
forodha kilichopo Holili (Tanzania) na Taveta (Kenya) na kuona shughuli
za usafirishaji na uchukuzi zinavyoendeshwa na kusisitiza umuhimu wa
kituo hicho kufanyakazi kwa kushirikiana ili kuongeza mapato kwa nchi za
Kenya na Tanzania.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
EmoticonEmoticon