Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya
Kilimanjaro chini ya Kocha wake Mkuu Charles Boniface Mkwasa imefanya
mazoezi yake ya mwisho leo asubuhi katika viwanja vya hoteli ya Green
Park Kartepe – Kocaeli nchini Uturuki.
Taifa Stars ambayo imeweka kambi nchini Uturuki kwa takribani wiki
moja, inajiwinda na mchezo wake dhidi ya Nigeria siku ya Jumamosi
Septemba 5, 2015 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuwania
kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika mwaka 2017.
Kocha Mkuu wa Stars Charles Mkwasa akiongea na tovuti rasmi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) www.tff.or.tz amesema anashukuru kambi imekua na mafanikio makubwa kwani vijana wanaonyesha mabadiliko makubwa sana.
“Ukiondoa mchezaji moja tu ambaye ni majeruhi Abdi Banda, Mkwasa
amesema wachezaji wengine wote wapo fit na kila mmoja atakayepata nafasi
katika mchezo wa sikuya jumamosi atafanya vizuri” amesema Mkwasa.
Mkwasa amesema mazingira ya kambi yamekua mazuri, na katika mechi ya
maozezi dhidi ya Libya iliyochezwa siku ya ijumaa, vijana wake walicheza
vizuri kwa nguvu na kufuata maelekezo yake, makosa machache
yaliyojitokeza katika mchezo huo wameyafanyia kazi na sasa anaamini wako
tayari kuwakabili Nigeria.
Mwisho Mkwasa amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi uwanja wa
Taifa siku ya jumamosi kuishangilia timu ya Taifa, kwani uwepo wa
washabiki wengi uwanjani utawaongeza morali zaidi wachezaji na kujiona
wapo nyumbani wanapambana kwa ajili ya Taifa lao.
Naye nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub “Cannavaro” amesema
maandalizi waliyopata ni mazuri na yamewajenga vilivyo kuelekea kwenye
mchezo dhidi ya Nigeria siku ya jumamosi na kuwaomba watanzania kuja kwa
wingi kuwasapoti.
Nadir amesema wao kama wachezaji kila mmoja yupo fit na anahitaji
kucheza mechi hiyo, hivyo yeyote atakayepata nafasi ya kucheza ana imani
atafanya vizuri katika kuipeperusha bendera ya Tanzania.
Stars ambayo iliweka kambi ya takribani siku nane katika milima ya
Katrepe - Kocaeli, inatarajiwa kuodoka kesho jumanne saa 1 jioni nchini
Uturuki kurejea nyumbani kwa usafiri wa shirika la Ndege la Uturuki
(Turkish Airlines) na kuwasili uwanja wa JK Nyerere majira ya saa 9
kasoro usiku.
Mara baada ya kuwasili Dar es salaam timu itaendelea na kambi kwa
kufanya mazoezi mepesi siku ya jumatano pamoja wa wachezaji wa kimataifa
Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Mrisho Ngasa katika uwanja wa Taifa
kujiandaa na mchezo wa siku ya jumamosi dhidi ya Nigeria.
EmoticonEmoticon