TTCL YATOA MSAADA WA KOMPUTA KUMI NA KIFURUSHI CHA INTANET VYOTE VIKIWA NA THAMANI YA SHILINGI 20, 197,600/=.

May 13, 2015


  3
Mkuu wa Biashara kanda ya Nyanda za juu kusini Bw. Juvenal Utafu akiwasihi wanafunzi ( hawapo pichani) kutumia vema mtandao uliotolewa na TTCL kwa manufaa ya elimu na si vinginevyo. Kushoto ni Bw. Nasibu Mengele aliyemwakilisha Afisa Elimu mkoa wa Iringa Bw. Eusedius Mtavangu kulia ni Meneja wa TTCL Iringa Bw. Humprey Ngowi.
1
Baadhi ya wafanyakazi wa TTCL waliohudhuria katika hafla ya makabidhiano hayo. Kutoka kulia ni meneja msaidizi (biashara) Bw. John Ngh’onoli, Meneja msaidizi (mtandao) Amani Kichele, afisa Utawala Bw. Silas Hokororoni na mratibu wa biashara kanda ya Nyanda za juu kusini Bw. Ephraim Vitalis .
4 
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa ICT, chuo kikuu Iringa Bw. Frederick Ngumbuke, Meneja maktaba kutoka Mt. Maiko sekondari Bw. Denis Mwamlima, Mkaguzi wa shule za sekondari kanda ya Nyanda za juu kusini Bw. Kadius Kiwanga. Wengine ni Mwakilishi wa diwani wa kata ya Gangilonga Bi. Maria Gotfried Sangana, Mchungaji Andendekisye M. Ngogo, mkuu wa shule ya sekondari Image, mwakilishi wa BAKWATA mkoa wa Iringa Sheikh Issa Said Gwere na Mchungaji Breyson M. Mbogo kutoka kanisa la Kilutheri Tanzania dayosisi ya Iringa.
5
Askofu mkuu wa jimbo la Iringa Tarcisius J. Ngalalekumtwa (kulia)akipokea moja ya komputa zilizotolewa na TTCL kutoka kwa Rais wa Global Outreach Tanzania Bw. Lucas Mwahombela. Askofu huyo amesaidia kutoa majengo ambayo ndiyo yanatumika kama maktaba ya Global Outreach bila malipo yoyote.
6
Picha ya pamoja .
…………………………………..
Kampuni ya simu Tanzania imetoa msaada wa komputa kumi pamoja na kifurushi cha internet ya bure yenye kasi ya 2Mbps kwa muda wa miezi sita kwa kituo cha Global Outreach Tanzania vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni ishirini laki moja na tisini na saba elfu mia sita ( Tshs.20, 197,600/=) ili kuendeleza juhudi zinazofanywa na Serikali na wadau wengine katika kuboresha mfumo wa elimu yetu kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Akiongea wakati wa kukabidhi komputa hizo kwa niaba ya afisa Mtendaji mkuu wa TTCL Dr. Kamugisha Kazaura, Mkuu wa biashara kanda ya Nyanda za juu kusini Bw. Juvenal Utafu ameipongeza Global Outreach Tanzania kwa kuanzisha mchakato huu wa kuinua elimu kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) ili kuendana na wakati na kuwafikia walengwa wengi kwa gharama nafuu na anaamini juhudi zao zitasaidia kujenga jamii yenye maarifa( knowledge society) katika zama hizi za uchumi maarifa (knowledge economy) na hivyo kuchangia katika juhudi za serikali kufikia malengo yake hasa katika kuleta maendeleo ya haraka kwa kwa wananchi wake wa kada mbalimbali.
Aidha Bw. Utafu amewaasa wanafunzi waitumie huduma hiyo ya internet kwa malengo yaliyokusudiwa. Waachane na matumizi mengine yasiyo na tija ambayo yanapatikana kwenye internet kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Aliongeza kuwa TTCL kwa sasa iko kwenye utekelezaji wa mabadiliko ya kibiashara na teknolojia kwa lengo la kuporesha huduma zake kwa wateja; wanatarajia ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu kuingia kwenye teknolojia ya GSM na LTE ili kuboresha utoaji wa huduma za simu za mkononi/kiganjani, simu za mezani na huduma za data nchi nzima hivyo Wananchi na taasisi mbalimbali watarajie kupata huduma nyingi na bora zikiwemo kutuma na kupokea fedha na vifurushi vya intanet yenye kasi kubwa.
Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo Bw. Nasibu A. Mengele aliyemwakilisha Afisa Elimu Mkoa wa Iringa Bw. Eusedius Mtavangu ameishukuru TTCL kwa juhudi zake za kuinua sekta ya elimu pamoja na sekta nyingine pia. Jambo hili ni mfano wa kuigwa kwa makampuni mengine, sisi serikali tunatambua mabadiliko na ukuwaji wa teknolojia kwa kasi ambao si budi kwa Tanzania- tukiwemo wana Iringa, tukajiandaa vyema ili kukabiliana na maendeleo hayo ili tusibaki nyuma. Global Outreach Tanzania inasaidia shule 13 na inatoa elimu ya komputa bure kwa wakuu wa shule, wasimamizi wa maktaba za komputa na walimu kwa ujumla. Mpaka sasa zaidi ya walimu 500 na wanafunzi 5000 wamenufaika na mafunzo hayo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »