DC KINONDONI AUNDA TUME HURU KUCHUNGUZA UBOVU WA BARABARA

April 14, 2015

 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, kuhusu tume aliyoiunda kwa ajili ya kuchunguza ubovu wa barabara katika wilaya hiyo.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
…………………………………………………………….
 
Na Dotto Mwaibale
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda ameunda tume ya wajumbe saba wakiwamo wawili kutoka serikalini kwa ajili ya kuchunguza ubovu wa barabara katika wilaya hiyo.Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana Makonda amesema amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakilalamikia ubovu wa barabara katika wilaya ya Kinondoni kuwa zinajengwa chini ya kiwango. Alisema wananchi hao wanasema barabara hizo zinajengwa chini ya kiwango kwani lami inawekwa leo lakini haimalizi miezi sita inabanduka na kuacha mashimo ambayo yamekuwa ni sehemu ya maisha ya kawaida kwa barabara ndani ya wilaya hiyo.
Makonda alisema katika wilaya hiyo barabara nyingi mitaro yake haipitishi maji kama inavyotakiwa, mitaro mingine imechimbwa mifupi kuliko mahitaji halisi, barabara kujengwa nyembamba kutoka kushoto kwenda kulia bna kuwa ujenzi wa barabara hizo hauendani na kasi ya mahitaji na kukua kwa mji.
Alisema kutokana na hali hiyo kwa kuwa si mtaalamu wa masuala ya barabara ameamua kuunda tume huru ya wataalamu itakayojumuisha wasanifu, wahandisi, wataalamu wa mikataba, ugavi na manunuzi na watu wengine kutoka vyombo mbalimbali ili wachunguze.
“Tume hii na vyombo hivyo vingine tumevipatia kazi ya kuchunguza usanifu wa barabara kama unazingatia viwango, taratibu za manunuzi na kutoa tenda kama zinazingatiwa, wakandarasi wetu wazalendo kama wanawajibika ipasavyo au kuna njama yoyote inafanywa ili kuhujumu kazi waliyopewa na kama wahandisi wetu wanatimiza wajibu wao ipasavyo kamtika mchakato mzima wa usanifu na ujenzi ili kuhakikisha ubora wa barabara unafikiwa” alisema Makonda.
Makonda alisema Tume hiyo itafanyafakazi kwa siku 21 kuanzia kesho Aprili 15 mwaka huu na kukabidhi ripoti yake ofisini kwake mbele ya waandishi wa habari Mei 5 mwaka huu saa 5 asubuhi na kuwa matokea ya ripoti hiyo ndiyo yatakayotoa majibu ya kupanua wigo wa uchunguzi kwenye kandarasi nyingine za ujenzi wa shule za serikali, ofisi za umma za wilaya hiyo.
Wajumbe wanaounda tume hiyo ni Mhandisi Julius Mamilo ambaye atakuwa mwenyekiti , Mhandisi Ronald Rwakatare (Katibu), John Malisa, Abednego Lyaga, Mhandisi Patrick Balozi na wajumbe wengine wawili kutoka vyombo vingine vya serikali vinavyoshughulikia uchunguzi.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »