RC MPYA TANGA AANZA KAZI RASMI.

December 13, 2014
  MKUU wa Mkoa mpya wa Tanga, Said Magalula, amesema mambo ya kwanza atakayoyashughulikia ofisini kwake ni migogoro ya ardhi na utoro sehemu za kazi na  kuwataka watendaji kumpa ushirikiano.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano ya ofisi na mtangulizi wake, Rajab Rutengwe aliehamishiwa Morogoro, alisema hatomuonea aibu mtendaji  au mkuu yoyote wa idara  ambaye atakuwa kikwazo cha maendeleo.

Alisema mambo ambayo atayapa kipaumbele atakapoingia ofisini ni migogoro ya ardhi kwa kuanzia idara ya mipango miji kuliko na chimbuko la malalamiko ya wananchi juu utoaji wa huduma na ushughulikiaji.

“Niko na faraja ya kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Tanga sehemu ambayo kwa miaka mingi nimeshafanya kazi na  nizungumzapo sura nyingi nazifahamu----wengi wanatambua utendaji wangu kuwa ni waufuatiliaji” alisema Magalula

“Mimi sina mchezo katika kazi na nimfuatiliaji mzuri wa mahudhurio ya makazini ufikaji na utokaji----watendaji wote na wakuu wao wa idara wafike makazini kwa wakati” alisema Magalula

Aliwataka wafanyakazi maofisini kumpa ushirikiano katika kuhakikisha anayaendeleza aloyaacha mtangulizi wake na hivyo kusema kuwa maendeleo hayatoweza kuja ikiwa hatoweza kupata ushirikiano.

Alisema ili kuweza kuupandisha Mkoa huo kiuchumi ni lazima kuwepo kwa ushirikiano baina ya wafanyakazi na watendaji pamoja na wananchi na kuweza kuupandisha Mkoa huo kukua kiuchumi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma elietokea Tanga, Chiku Gallawa amewaaga wakuu wa Idara na wafanyakazi wa Mkoa wa Tanga kwa kuwashukuru kumpa ushirikiano kwa kipindi chote alichokuwepo.

Alisema ataendelea kuwa bega kwa bega na wananchi wa Tanga pamoja na wafanyakazi wake na ataendelea kushirikiana na kuwa tayari kufika akihitajika.

“Nitaikumbuka Tanga kwa mambo  mengi likiwemo ukarimu wa watu na ushirikiano wa watendaji makazini----lakini pia mukumbuke Dodoma pia nakupenda na nimefika” alisema Gallawa

Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma alitoa shukurani zake kwa waandishi wa habari na kuwataka kuutangaza vyema Mkoa huo katika mambo mbalimbali vikiwemo vivutio vyake vya utalii.

Alisema Tanga iko na vivutio vingi lakini utangazaji wake ni mdogo na hivyo kuwataka kuvitumia vyombo vyao katika kuutangaza na kutambulika ndani na nje ya nchi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »