Na, Anna Makange
MJI wa Tanga unaweza kurudisha historia ya umaarufu na umuhimu wake kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kihistoria endapo wakazi wake wataunga mkono kwa dhati juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na wawekezaji na wadau wengine mbalimbali wa maendeleo.
MJI wa Tanga unaweza kurudisha historia ya umaarufu na umuhimu wake kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kihistoria endapo wakazi wake wataunga mkono kwa dhati juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na wawekezaji na wadau wengine mbalimbali wa maendeleo.
Harakati mbalimbali zimekuwa zikifanywa
na viongozi wa serikali kwa kuwashirikisha wananchi ili kuhakikisha
kwamba mambo yanakwenda vizuri kwa lengo la kurudisha hadhi ya Tanga na
ustawi wake kwa ujumla.
Hadhi iliyokuwa imefifia kwa muda hasa
baada ya kuanguka kwa shughuli za uzalishaji katika mashamba ya mkonge,
viwanda na bandari kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1980.
Kupungua kwa shughuli za kiuchumi pamoja
na kuchochewa na kuanguka kwa uzalishaji wa zao kuu la biashara la
Mkonge lililokuwa likitegemewa sana kama uti wa mgongo wa uchumi mkoani
hapa, pia kulisababisha idadi kubwa ya wakazi kukosa ajira katika
mashamba ya Mkonge, viwandani, bandarini na hivyo kuwanyima uhakika wa
kipato.
Pia athari hizo kwa upande mwingine
zilisababisha kuzorota kwa mwendelezo wa shughuli za kijamii na
utamaduni wa asili ya Tanga ikiwemo hali ya kurithishana mila, desturi
na utamaduni uliokuwa umestawi miongoni mwa wakazi wake.
Aidha, katika kipindi hicho pia wakazi
wa Tanga walishuhudia mabadiliko ya aina mbalimbali yakiwemo ya kufa kwa
viwanda, kubadilishwa matumizi ya baadhi ya maeneo yaliyokuwa ya
kijamii, kiuchumi na kiutamaduni na kuanza kutumika kwa kazi nyingine
tofauti au kutelekezwa kabisa bila kuendelezwa.
Kwa mfano baadhi ya majengo yaliyojengwa
zamani wakati wa ukoloni yalibomolewa na kujengwa nyumba mpya za
Ghorofa, uvaaji wa mavazi kwa wanaume na wanawake ulibadilika kutoka
yale ya asilia na kuingizwa mitindo mipya ambayo imeendelea kubeba
majina ya mavazi hayo hayo likiwemo vazi la Buibui.
Mfano mwingine ni Uwanja maarufu wa
Sabasaba ulioko eneo la Gofu Juu katika Kata ya Nguvumali ambao ulikuwa
ukitumika kwa shughuli za maonesho ya shughuli za kilimo, ufugaji na
uzalishaji wa viwanda wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima
Tanzani yaliyokuwa yakifanyika kuanzia Julai Mosi hadi Saba kila mwaka
kabla ya kubadilishwa na kuitwa Nanenane ambayo hufanyika Agosti Mosi
hadi Nane kila mwaka.
Eneo hilo la ‘Sabasaba’ Tanga kwa sasa
limebaki kuwa jina tu la ki historia kutokana na kubadilika ki matumizi
ambapo baadhi ya wafanyabiashara walipangishwa humo uwanjani wanatumia
eneo hilo kwa shughuli za kilimo cha bustani za mboga, nyumba za ibada,
vilabu vya pombe na biashara ya nyama ya Nguruwe (Kitimoto).
Kwa ujumla hali hiyo ya mabadiliko ya
kijamii na kiutamaduni pamoja na kutajwa kwamba ni miongoni mwa hatua za
maenedeleo kwa upande mwingine zilidhoofisha kasi ya wenyeji wa mji wa
Tanga kutunza na kurithisha mila, desturi na tamaduni zao kutoka kizazi
cha wakati huo hadi sasa.
Ni kwa kutambua umuhimu wa jamii
kurithisha mila, destruti na tamaduni zake kutoka kizazi kimoja hadi
kingine Taasisi isiyo ya kiserikali ya URITHI Tanga iliamua kubeba
jukumu hilo ili kuhakikisha utamaduni wa asili unaendelea kudumishwa.
Imeazimia kuelimisha wanajamii na wageni
wasio wenyeji wa mji wa Tanga kuhusu mambo muhimu ya kihistoria
yaliyokuwepo Tanga kwa kuamua kuanza kukiimarisha kituo maalumu cha
Makumbusho ya Tanga ili kuiweka pamoja historia na utamaduni wa mwenyeji
wa hapo katika eneo moja linalofikika kwa urahisi.
Taasisi hiyo ya URITHI Tanga ilianzishwa
mwaka 1998 kwa shabaha ya kufufua, kukusanya taarifa na kuhifadhi
kumbukumbu za majengo, miundombinu, tamaduni, mila na desturi za
mswahili wa Tanga na makabila mengine yaliyomo ndani ya makumbusho.
Lengo ni kuusaidia mkoa kuendelea
kutangaza Utalii na urithi wa kiasili wa Tanga kitaifa na kimataifa kwa
ajili ya maendeleo ya vizazi vilivyopo na vijavyo vya wakazi wake na
taifa kwa ujumla.
Wazo lililosababisha kuanzwa kwa
mchakato wa uwepo wa makumbusho ya Tanga inaelezwa kwamba lililetwa na
baadhi ya wazawa ambao waliona kwamba kuna umuhimu wa kufanya hivyo hasa
baada ya kubaini kasi ya upoteaji wa urithi wa kiasili na vitu vya
kihistoria vilivyoanzia Tanga kabla ya maeneo mengine nchini.
Alhaj Abdalah Majura ambaye ni
Mwenyekiti wa taasisi hiyo ya Urithi Tanga amezungumza na Mwandishi wa
makala haya akisema ilipofika katikati ya miaka ya 1990 walibaini kwamba
idadi kubwa ya vitu vilivyokuwa vikinakshi historia ya Tanga vilikuwa
vikipotea kwa kasi ya ajabu.
“Vitu hivyo vinajumuisha majengo ya aina
mbalimbali yaliyojengwa katika zama tofauti za ukoloni ambayo katika
kipindi hicho yalikuwa yakiathiriwa na kasi ya ujenzi wa nyumba za
kisasa na majengo mengine ya ghorofa…. hasa kwa kuyavunja majengo hayo
ya zamani ili kutumia maeneo hayo kwa kujenga mapya” kisasa, anaeleza.
Anataja sababu nyingine kwamba ni
kuibuka kwa biashara ya vifaa na samani mbalimbali zilizokuwemo katika
majengo ya zamani yaliyojengwa na wakoloni.
Samani na vifaa hivyo vya zamani
vilijumuisha saa za ukutani, milango, madirisha na taa za karabai
ambavyo watu wasiojulikana kwa makusudi walikuwa wakivamia majengo
yaliyoko katika maeneo mbalimbali ya mji na kuviiba kasha kuvitorosha
nje ya nchi kwa lengo la kuviuza.
Shughuli nyingine zilihusisha kazi ya
uharibifu wa mazingira uliojumuisha vitendo vya ukataji wa miti ikiwemo
ya aina ya ‘Mikanju’(Mikorosho) katika eneo la Mikanjuni na
‘Mitiki(iliyokuwa na majani mapana)’ katika eneo la MajaniMapana kwa
ajili ya kupata maeneo ya ujenzi (viwanja) na mbao na kusababisha maeneo
hayo kubaki na majina ya ki historia tu tofauti na umuhimu wa uoto wa
asili uliokuwemo ambao umesadifi majina ya maeneo hayo.
Anasema kulikuwepo pia na utekelezaji wa
shughuli za kilimo hasa uzalishaji wa Mkonge, uvaaji wa mavazi kama
Buibui, Mapishi yaliyoambatana na ulaji wa Vyakula vya asili kwa kutumia
vifaa(vyombo) vya asili pamoja na uvuvi.
“Tanga ulikuwa mji muhimu sana uliowahi
kufanikiwa ki maendeleo kabla na baada ya kuja kwa wakoloni, ki ukweli
histotia nyingi za Tanzania kwa ujumla zina mahusiano ya karibu sana na
maeneo ya mkoa huu kutokana na kuunganishwa moja kwa moja na mji wa
kihistoria na vijiji vya Tanga”.
“Kwa mfano katika enzi ya utawala wa
Wajerumani walihusisha sana Tanga kwa mfumo wake wa kiuongozi uliotumia
Maliwali, Maakida na Makadhi pamoja na kujenga majengo mengi makubwa
katika mji wa Tanga”.
Alitaja baadhi ya majengo hayo ambayo
yalijengwa jijini Tanga wakati wa utawala wa wakoloni wa Kijerumani ni
Hospitali ya kwanza ya serikali “Cliff Block’ ambayo sasa inafahamika
kama Hospitali ya Bombo.
Cliff Block ilijengwa katika kipindi cha
zaidi ya mika 100 iliyopita wakati wa utawala wa Wajerumani kwa sasa
jengo hilo halitumiki hasa baada ya serikali kujenga majengo mengine ya
kisasa zikiwemo gorofa na nymba za kawaida ambayo hutumika kwa shughuli
za Hospitali ya mkoa wa Tanga. Jengo hilo kwa sasa lipo kwenye hali
mbaya ya uharibifu.
Majengo mengine yalihusisha sekta ya
elimu ambapo wakoloni hao wa Kijerumani walijenga Sekondari ya kwanza ya
serikali nchini ambayo ilifahamika kama ‘Tanga School’.
Shule hiyo ya ki historia ilijengwa
zaidi ya miaka 100 iliyopita na sasa inafahamika kama Old Tanga
Secondary School na inamilikiwa na Halmashauri ya jiji.
Majura anataja vitu vingine vya ki
historia vilivyoanzishwa Tanga na baadae kuenezwa katika maeneo mengine
nchini ni kilimo cha Zao la Mkonge ambalo alisema kwa mara ya kwanza
lilianza kupandwa katika kijiji cha Kikokwe kilichopo jijini humo.
“Kwa mara ya kwanza barani Afrika
wakulima wa Kikoloni kutoka Mexico waliamua kubeba miche 1,000 ya mkonge
ili kuja kufanya utafiti wa kuanzisha kilimo hicho huku Afrika
Mashariki.
“Kutokana na safari ndefu na misukosuko
ya njiani ni miche 62 tu kati ya miche yote ndiyo ilifika salama katika
pwani ya bahari ya Hindi eneo la Tanga na kupandwa hapo Kikokwe kabla ya
kuanzishwa mashamba makubwa baadae”.
Aidha, anasema pamoja na kutambua vitu
hivyo vya kihistoria ambavyo ki msingi havikuwa katika eneo moja ndipo
taasisi ya Urithi ikaona umuhimu mkubwa wa kuvihifadhi hasa kwa
kuunganisha shughuli zote hizo katika eneo moja la Makumbusho ya Tanga.
Makumbusho ya Tanga inapatikana
pembezoni mwa barabra ya Uhuru kwenye jengo lililokuwa la Ofisi ya mkuu
wa wilaya kabla na baada ya uhuru na baadae likatumika kama ofisi ya
mkuu wa Mkoa wa Tanga miaka kadhaa baada ya uhuru wa Tanzania.
Jengo hilo lililopo jirani na makataba
ya mkoa wa Tanga ni miongoni mwa maeneo ya historia ambayo yaliwahi
kusahauliwa na kuanza kuhujumiwa na watu hao wasiojulikana hadi katikati
ya miaka ya 2000 taasisi hiyo ilipofanikiwa kulichukua na kuanza
kulikarabati.
Ukarabati wa jengo hilo ulifanywa kwa
awamu kwa ufadhili wa shilingi Milioni 35 kutoka Ubalozi wa Ujerumani
pamoja na majengo mengine ikiwemo mahakama ya mwanzo ya Usambara, mnara
wa Saa ulioko jirani na benki ya CRDB.
Majura anasema madhumuni ya kuanzishwa
kwa makaumbusho hayo ni kuhamasisha utalii wa ndani kwa kujaribu
kuonesha maisha, makazi(majengo), historia ya Tanga, mila, ngoma za
asili pamoja na habari muhimu za Tanga.
Pia kuelezea kwa ufasaha historia ya
masuala mbalimbali ukiwemo uchumi wa Tanga ambao ulitegemea Mkonge, watu
maarufu kama Shaaban Robert, Makata Mwintwana, Kihere, Kadhi Ali bin
Hemed ambaye ndiye baba yake Mufti wa kwanza Tanzania ambaye alitokea
Tanga.
Aidha, anasema Mkumbusho hiyo itahifadhi
alama hizo ili kuendeleza historia halisi na maana ya Tanga kwa kutumia
mbinu mbalimbali zikiwemo kuwajegea ufahamu mara kwa mara viongozi wa
ngazi mbalimbali katika serikali za mitaa, serikali kuu, wanafunzi na
vyombo vya habari ili kuongeza uhamasishaji.
Naye Joel Niganile ambaye ni mmoja wa
watumishi katika makumbusho ya Tanga alisema kuanzishwa kwake kuwezesha
kutoa fursa ya kuongeza ufahamu kwa wananchi hasa wakazi wa jiji la
Tanga.
“Pia wageni kutoka maeneo mbalimbali ya
ndani na nje ya nchi wanatutembelea mara kwa mara kwa lengo la kuangalia
na kupata taarifa mbalimbali muhimu zilizopo ndani ya makumbusho.
Hata hivyo Majura anasema licha ya
kupata mafanikio hayo makumbusho hiyo bado inakabiliwa na changamoto
kadhaa ikiwemo bajeti ya uhakika ya kuendesha utendaji wa kila siku hasa
kwakuwa bado hawajakamilsha kazi ya kuingiza vitu vyote vya kihistoria
kutoka katika maeneo yake ya asili.
“Kwa sasa bado tunalazimika kuendelea
kutegemea sana wafadhili na mchango mdogo kutoka kwa wafanyabishara na
kampuni binafsi za hapa jijini Tanga hivyo kushindwa kujitegemea na
kujikimu ki mahitaji”,anaeleza.
Anasema changamoto nyingine ni uelewa
mdogo miongoni mwa wananchi hasa kutambua kwamba majengo ya zamani
yanathamani na wanawajibiika kuyatunza badala ya kuthamini ujenzi wa
nyumba za kisasa naza gorofa ambazo zinabadilisha mwonekano wa asili wa
mji.
“Pia tunakabiliwa na uhaba mkubwa wa
watendakazi katika makumbusho haya ambako hivi sasa tupo watu wane tu
ambao ki msingi tunafanya kazi kwa kujitolea”.
Majura anahimiza kwamba kuna haja kwa
wakazi wa Tanga na vitongoji vyake kuanza kuuunga mkono harakati hizo
ili kuwezesha makumbusho ya Tanga kufikia lengo lake ililokusudia.
Aidha, ni wakati muafaka umefika kwa
serikali, wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanajitoa
na kutumia fursa hiyo ya makumbusho kupeleka taarifa sahihi na vifaa
muhimu vya kihistoria ili kuiwezesha makumbusho hiyo kusheheni vitu
hivyo tofauti.
Ni vema baadhi ya wakazi ambao
wamebahatika kuendelea kuhifadhi au kumiliki vitu vya asili ya Tanga na
vya historia yake kwa ujumla kuviwasilisha hapo Makumbusho na kuachana
na tamaa ya kutafuta wateja wa kuwauzia kama baadhi yao wanavyoendelea
kufanya hivi sasa kwa siri.
EmoticonEmoticon