Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
SIMBA SC inawakosa wachezaji wanne muhimu katika
mechi yake ya pili, ligi kuu soka Tanzania bara inayopigwa leo jioni dimba la
Taifa, Dar es salaam dhidi ya Maafande wa Polisi Morogoro.
Wachezaji hao ambao kocha Patrick Phiri atawakosa ni
kipa namba moja, Ivo Philip Mapunda, beki wa kushoto, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’,
Winga hatari Haroun Chanongo na Mshambuliaji Paul Kiongera , wote ni majeruhi.
Mechi ya ufunguzi wikiendi iliyopita ambayo Simba
ililazimishwa sare ya 2-2 na Wagosi wa Kaya, Coastal Union katika uwanja huo wa
Taifa, Issa Rashid pekee ndiye hakucheza kati ya wachezaji hao wanne.
Ivo alisimama langoni na alifanya jitihada kubwa
kuisaidia timu yake ipate ushindi, lakini hakufanikiwa kufuatia kuruhusu nyavu
zake kuguswa mara mbili.
Licha ya kufungwa, Ivo hakustahili lawama za moja
kwa moja, kwasababu magoli yote mawili yalitokana na timu kushindwa kudhibiti
eneo la kiungo na kuwaacha Coastal wafike golini na kutengeneza nafasi za
mabao.
Makosa binafsi ya beki kinda, Hassan Isihaka yalichangia
Simba kufungwa, lakini kijana huyu mdogo aliyerithi mikoba ya Donald Mosoti hakustahili
lawama kwasababu ndio kwanza anachipukia.
Chanongo alicheza dhidi ya Coastal Union lakini
aliumia. Mshambulijai huyu wa pembeni katika mechi hiyo hakucheza kwa kiwango
chake.
Hakutumia staili yake ya kukimbia na mpira,
kupunguza mabeki na kuingia ndani. Mipira mingi aliyoshika katika eneo la
hatari alikuwa anageuka na kutoa pasi.
Chanongo alionekana kuwa muoga kuwafuata mabeki
kama alivyokuwa anafanya msimu uliopita. Inawezekana hayuko sawa kisaikolojia
kutokana na kuwahi kushutumiwa kuuza mechi.
Kiongera alitokea benchi, lakini alipata majeruhi
katika dakika za majeruhi. ‘Baba Ubaya’ hakucheza kabisa na nafasi yake
ilishikwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Paul Kiongera hachezi leo
Kutokana na usajili mzuri waliofanya Simba, Kipa
bora wa msimu uliopita, Hussein Sharrif ‘Casillas’ ataziba nafasi ya Ivo,
Ibrahim Twaha anaweza kuchukua nafasi ya Chonongo, nafasi ya Issa bado
ataendelea kucheza Tshabalala wakati nafasi ya Kiongera anaweza kuziba na Elias
Maguli.
Mechi iliyopita, Simba walianzia kufa katikati.
Piere Kwizera aliyecheza nafasi ya kiungo wa ulinzi alishindwa kupiga pasi
katika maeneo sahihi.
Kwa kiasi kikubwa alikuwa anapiga pasi sahihi,
lakini hazikuwa na madhara. Kuna wakati alikuwa anachelewa kuanzisha ‘Movement’
kwa kwenda mbele.
Kama atabadilika leo na kuipandisha timu kwenda
mbele, basi Simba inaweza kufanya vizuri. Pia itakuwa nzuri kama Phiri
atamuanzisha Shaaban Kisiga nafasi ya kiungo mshambuliaji (namba 10).
Kisiga huwa anacheza kwa ubora wa hali ya juu
katika nafasi hiyo. Huwa anaweza kupiga pasi nzuri na kuipandisha timu kwa kasi,
lakini kitendo cha kuchezeshwa namba 8, kinamfanya asitoe ubora wake.
Kwa safu ya ushambuliaji, nadhani Amissi Tambwe
ataendelea kuwa mtu hatari. Lakini itategemea na viungo wake na watu
watakaokuwa nyuma yake.
Sitegemei kuona maajabu kutoka kwa Emmanuel Okwi
kama atakuwepo. Mpaka leo asubuhi hakukuwa na taarifa za nyota huyo kupewa
kibali cha kufanya kazi nchini licha ya kusajiliwa kihalali na Simba.
Okwi amepunguza kasi yake, haingia ndani kama
zamani, nadhani imechangiwa na kutocheza mpira wa muda mrefu. Ni mchezaji
hatari, lakini kwasaa dhahiri anahitaji kupewa muda na kufanya mazoezi maalumu
ili kurudisha kasi yake.
Emmanuel Okwi (kulia)
Tambwe ataendelea kuwa mtu muhimu na kama
atapigiwa mipira ya krosi na pasi nyingi za mwisho, basi anaweza kufunga.
Simba wanaweza kuvuna pointi mbele ya Polisi
Morogoro, lakini sio kwa kirahisi tu. Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa
Stars, Danny Mrwanda ni mchezaji wa kuchungwa sana.
Mwaka juzi alisajiliwa na Simba, lakini alitemwa
kabla ya kuanza ligi kwa madai kuwa ameshuka kiwango na baadaye akatimkia
Vietnam.
Aina ya mchezaji kama Mrwanda ni hatari sana, na
kwakuwa Simba walishindwa kuona thamani yake, anaweza kuingia uwanjani kwa
lengo la kutaka kulipa kisasi.
Kama Bantu Admin na Suleiman Kassim ‘Selembe ‘
watakuwa katika ubora wao na kumlisha mipira sahihi, nadhani Mrwanda anaweza kufanya kitu.
Nahodha wa Polisi, Lulanga Mapunda ni mtu sahihi
sehemu ya ulinzi. Ni mzoefu sana, hivyo imekuwa rahisi kwake kuwa kiongozi
uwanjani.
Kwenye mechi dhidi ya Azam, Polisi walifungwa 3-1.
Na kipindi cha kwanza walionekana kuwa na hofu kubwa, walitawaliwa na Azam kwa
kila kitu.
Waliruhusu mpira kucheza zaidi katika eneo lao,
hivyo vijana wa Joseph Omog waliweza kupanga mashambulizi mengi. Kama washambuliaji
wa Azam, Kipre Tchetche, Didier Kavumbagu wangekuwa makini, basi wangefunga
magoli mengi.
Lakini kipindi cha pili walibadilika na kujaribu
kucheza mpira. Bila shaka kocha Adolf Rishard aliona makosa yake na kuyafanyia
kazi.
Polisi hawana rekodi ya kushinda dhidi ya Simba
uwanja wa Taifa, kama Historia haitawatendea haki, basi wataendelea kufungwa.
Lakini Simba wasiingie kichwa-kichwa, mpira umebilika siku hizi. Timu ndogo inaweza kupata matokeo pia.
EmoticonEmoticon