MAALIM SEIF AZIBARIKI KMKM NA SHABA NGAO YA JAMII ZANZIBAR

September 12, 2014


1 (19)
Makamu wa kwanza wa rais wa serikali ya mapinduzi Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na mmoja wa wachezaji wa timu ya soka ya KMKM wakati akikagua timu hizo kwenye mchezo wa ngao ya jamii baina ya KMKM na Shaba ya Pemba kabla ya ufunguzi wa ligi kuu ya soka ya Grandmalt inayotarajiwa kuanza jumatatu tarehe 15/09/2014, KMKM ilishinda kwa mabao 2:0 dhidi ya shaba ya Pemba.
2 (13)Sehemu ya washabiki waliofurika kwa wingi kwenye uwanja wa Amani mjini Zanzibar kushudia mchezo kati ya kmkm na Shaba kwenye mchezo wa ngao ya Jamii
3 (13)Makamu wa kwanza wa rais wa serikali ya mapinduzi Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akimkabidhi ngao ya jamii nahodha wa timu ya KMKM Khasim Ali mara baada ya kushinda mchezo dhidi ya timu ya Shaba ya pemba kwa magoli 2:0 kushoto mwenye fulana ya njano ni meneja mauzo Tanzania wa kinywaji cha Grandmalt Kassiro Msangi.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Soka ya Grand Malt ya Visiwani hapa, KMKM juzi walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Shaba kutoka Pemba katika mchezo  wa Ngao ya Jamii uliofanyika kwenye Uwanja wa Amaan.
Ikicheza mbele ya mgeni rasmi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Seif Shariff Hamad, KMKM ilikabidhiwa zawadi maalum ya ngao na kiongozi huyo wa nchi.
Bao la kwanza la KMKM katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani lilifungwa na Pandu Haji  katika dakika ya 83 huku lile lililowanyamazisha mashabiki wa Shaba waliofika uwanjani hapo liliwekwa kimiani na Faki Mwalimu sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho.
Hata hivyo KMKM walipoteza nafasi nyingi za kufunga katika kipindi cha kwanza kupitia kwa washambuliaji wake Mudrik Muhibu na Mwalimu ambao walishindwa kumalizia nafasi walizotengeneza.
Dakika ya 89 Shaba ilipoteza nafasi ya kusawazisha kupitia kwa mchezaji wake Suleiman Nuhu ambaye akiwa mita chache na kipa wa KMKM, Mudathir Khamis, kwa kupiga juu na kupoteza nafasi ya wazi ya kufunga.
 Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii ilifanyika chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Grand Malt ambao ndio wadhamini wakuu wa ligi hiyo na ulikuwa ni maalumu kwa ajili ya uzinduzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Grand Malt Zanzibar ambayo inatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 15 mwaka huu.
KMKM:  Mudathir Khamis, Pandu Haji, Mwinyi Haji, Makame Haji, Khamis Ali, Ibrahim Khamis, Iddi Kambi/ Am Khamis (dk 45), Juma Mbwana, Abdi Kassim, Mudrik Muhibu/  Faki Mwalim (dk 46) na Maulid Ibrahim/  Nassor Ally (59).
Shaba: Mhando Twaha, Robert Mtuge, Hassa Shaaban, Amour Said, Mahmoud Salmin, Juma Mwalimu, Bakari Suleiman/ Kheri Shaaban (dk 56), Sheha Khamis, Mohammed Nyasa, Jackson Dickson na Suleiman Nuhu.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »