EU KUISAIDIA TANZANIA MSAADA WA SHILINGI BILIONI 134

May 08, 2014


 Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacious Likwelile (kulia) akisaini mkataba wa msaada wa sh. Bilioni 134 kwa niaba ya Serikali ya Tanzania leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Balozi EU nchini Filberto Sebregond.



Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacious Likwelile (kulia) akibadilishana hati ya mkataba wa msaada wa sh. Bilioni 134 waliosaini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Balozi EU nchini Filberto Sebregond.

Na Eleuteri Mangi-MAELEZO


SERIKALI ya Tanzania imetiliana saini mkataba wa msaada wa zaidi ya Shilingi Bilioni 134 sawa na Euro milioni 59.5 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kusaidia sekta ya kilimo na usafirishaji nchini.

Mkataba huo ulisainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa EU nchini Filberto Sebregond leo jijini Dar es salaam.

Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo, Dkt. Likwelile alisema kuwa sehemu ya msaada huo ambao ni Shilingi Bilioni 82.4 ambazo ni sawa na Euro milioni 36.5 utatumika kuendeleza sekta ya kilimo na kukuza uchumi nchini kwa kupitia kituo  maalum cha uendelezaji kilimo ukanda wa Kusini Tanzania (SAGCOT) na kuboresha miundombinu ya barabara za ukanda huo.

Vilevile Dkt. Likwelile alisema kuwa sehemu iliyobaki ya msaada huo ambao ni Shilingi Bilioni 51.9 ambazo ni sawa na Euro milioni 23 itatumika kuimarisha biashara na ushirikiano katika jumuiya kwa kuanzisha  kituo cha pamoja cha ukaguzi mipakani (OSIS).
“Vituo hivyo vya ukaguzi mipakani vitakuwa na manufaa si kwa Tanzania tu, bali hata katika nchi mbalimbali zinazopakana na Tanzania” alisema Dkt. Lkwelile.

Alifafanua kuwa msaada uliosainiwa unamanufaa kwa wananchi kwa kuboresha miundombinu vijijini na kusambaza umeme vitu ambavyo vitasaidia kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »