March 20, 2014
MADADI MKURUGENZI MPYA WA UFUNDI TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemteua Salum Madadi kuwa Mkurugenzi wake mpya wa Ufundi.

Uteuzi huo umefanya na Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha dharura kilichofanyika jana (Machi 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Kabla ya uteuzi, Madadi alikuwa akikaimu nafasi hiyo tangu Januari mwaka huu baada ya Mkurugenzi wa Ufundi aliyekuwepo kumaliza mkataba wake Desemba 31 mwaka jana.


Madadi mwenye leseni A ya ukocha ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni kocha mwenye uzoezi wa zaidi ya miaka 30 ambapo alianza kufundisha mpira wa miguu mwaka 1980 katika klabu ya Maji SC ya Lindi.

Ana elimu ya sekondari aliyoipata katika shule ya Chidya na diploma ya ukocha wa mpira wa miguu aliyoipata nchini Ujerumani. Pia ni Mkufunzi wa makocha wa CAF, na alijiunga na TFF mwaka 2006 akiwa Ofisa Maendeleo.

Alikuwa Kocha wa Taifa Stars mwaka 2000. Mbali ya Maji SC, amewahi kufundisha timu za Nyota Nyekundu, Ushirika ya Moshi, Simba, Shangani ya Zanzibar, Malindi ya Zanzibar, Cardif ya Mtwara na Kariakoo ya Lindi.

Pia amewahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

YANGA, SIMBA ZAPIGWA FAINI MIL 25
Klabu za Yanga na Simba zimeagizwa kulipa jumla ya sh. milioni 25 kutokana na uharibifu wa viti na vurugu zilizofanywa na washabiki wao kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly ya Misri iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga italipa sh. milioni 15 ambayo ni gharama ya uharibifu wa viti uliofanywa na washabiki kwenye mechi hiyo. Pia imepigwa faini ya sh. milioni tano kutokana na vurugu za washabiki wake. Nayo Simba imepigwa faini ya sh. milioni tano kutokana na washabiki wake kuhusika katika vurugu hizo.
Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao chake cha dharura kilichofanyika jana (Machi 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Tunatoa onyo kwa washabiki wa mpira wa miguu kujiepusha na vurugu viwanjani ikiwemo uharibifu wa miundombinu mbalimbali ya viwanja ikiwepo viti, na tutachukua hatua kali zaidi kwa klabu na washabiki wake iwapo vitendo hivyo vitajitokeza tena.

RAMBIRAMBI KIFO CHA MSHABIKI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mshabiki Deodatus Mwakyangula kilichotokea jana (Machi 19 mwaka huu) wakati ya mechi kati ya Yanga na Azam iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa kwa familia ya Mwakyangula na kwetu, kwani umetokea wakati akiwa uwanjani kushuhudia mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Mwakyangula, na klabu ya Yanga na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina

RWIZA, LIUNDA KUSIMAMIA MECHI ZA CAF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua Watanzania Alfred Rwiza na Leslie Liunda kusimamia mechi zake za wikiendi hii na mwezi ujao.

Liunda ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi ya Kombe la Shirikisho (CC) kati ya How Mine ya Zimbabwe na Bayelsa United ya Nigeria itakayochezwa Jumamosi (Machi 22 mwaka huu) jijini Bulawayo.

Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Eritrea, na wanaongozwa na Maeruf Kherseed. Wasaidizi wake ni Angeson Ogbamariam, Berhe O’Michael na Luelseghed Ghebremichael.

Naye Rwiza atasimamia mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 kati ya Lesotho na Swaziland itakayochezwa kati ya Aprili 25-27 mwaka huu jijini Maseru.

Mechi hiyo ya marudiano itachezwa na waamuzi Duncan Lengani, Innocent Kaundula, Hendrix Maseko na Jones Makhuwira, wote kutoka nchini Malawi.

Boniface Wambura Mgoyo
Media and Communications Officer
Tanzania Football Federation (TFF)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »