African Sports mabingwa wa soka Tanga.

May 08, 2013
Na Mwandishi Wetu,Tanga.
TIMU ya African Sports "Wanakimanumanu" mwishoni iliweza kufanikiwa kuwa mabingwa wa wapya wa mkoa wa Tanga baada ya kuibamiza Makorora Star mabao 5-0 ikiwa ni ligi ya mkoa wa Tanga mchezo uliochezwa uwanja wa soka Mkwakwani.

Licha ya African Sports kuwa mabingwa lakini bado wamesalia na michezo michache kwenye ligi hiyo kutokana na kuwa na wingi wa pointi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye ligi hiyo ambapo mpaka sasa wamekwisha kujikusanyia pointi 54.

Furaha ya wanakimanumanu hao ilianza baada ya mchezaji wao James Mendy kupachika bao katika dakika ya 5 ambaye alitumia uzembe wa mabeki wa makorora waliokuwa wamezubaa langoni mwao wakishindwa kujua nini cha kufanya.

Bao hilo lilidumu mpaka timu zote zinakwenda mapumziko ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi kutokana na kila timu kuonekana kujipanga kwa ngwe hiyo ya mwisho kwa kufanya mashambulizi kwa zamu langoni mwa timu pinzani.

Wakionekana kujipanga na kupanga mashambulizi langoni mwa Makorora Star,African Sports waliweza kucheza kwa umakini na kucheza pasi fupifupi na ndefu na kuweza kukitawala kipindi hicho na kupelekea kuandika bao la pili dakika ya 47 kupitia Thabiti Mgoha ambaye alimalizia kazi iliyofanywa na Pera Ramadhani.

Baada ya kuingia mabao hayo langoni mwa Makorora Star nao waliweza kucharuka na kucheza kwa umakini huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza lakini mlinda mlango wa African Sports Omari Jengo aliweza kupanchi mashuti yaliyokuwa yakielekezwa kwenye lango lao.

Wakiendeleza wimbi la mashambulizi ,African Sports waliweza kuongeza mabao mengine mawili kupitia dakika za 67 likifungwa na Shekue Salehe na bao la nne likifungwa na Mohamed Issa kwenye dakika ya 75 ambapo zilipoingia bao hizo ziliwafanya wapinzani wao kukata tamaa mapema na kucheza ilimradi mchezo umalizike.

Katika dakika ya 88 ya mchezo huo mchezaji Gidatu Akudae aliweza kuwainua mashabiki wa timu hiyo baada ya kuhitimisha karamu ya mabao langoni mwa Makorora kwa kupachika bao la tano ambapo alitumia uzembe wa mlinda mlango wa timu hiyo,Ally Salim kufunga bao hilo.

Akizungumza mara baada ya kumalizika mchezo huo,Kocha Mkuu wa timu ya African Sports "Wanakimanumanu"Edmund Nyoni alisema wanamshukuru mungu kwa kuweza kuwa mabingwa na kuhaidi kuyafanyia kazi mapungufu yaliyopo kwenye kikosi chake kabla ya kuanza mashindano ya mabingwa wa mikoa.

 Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »