AFRIKA IPEWE UHURU WA KUZALISHA NISHATI KWA KUTUMIA RASILIMALI ZAKE -DKT.BITEKO

June 19, 2025 Add Comment


📌*Ahimiza Tanzania na Urusi kuendeleza uhusiano wake wa kuheshimiana*


📌*Tanzania kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme wastani wa  megawati 120*


📌 *Tanzania yapongezwa kwa mafanikio yake sekta ya nishati*


📌 *Ahimiza mfumo sawa wa uzalishaji nishati kati ya nchi tajiri na masikini*


📌 *Kampuni za Urusi zaombwa kuwekeza zaidi Afrika* 


*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa nchi za Afrika kupewa uhuru wa kuzalisha nishati kwa kutumia raslimali zilizopo barani humo.


Dkt. Biteko ametoa wito huo leo Juni 19, 2025 wakati akizungumza katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg linalofanyika nchini Urusi.

Amesema Afrika inahitaji programu itakayosaidia kufikia dhamira yake ya kuondoa idadi kubwa ya watu ambao hawatumii nishati safi huku akitaja baadhi ya athari za matumizi ya nishati isiyo safi ikiwemo uharibifu wa mazingira.


Ameongeza kuwa Afrika ina vyanzo  vingi vya kuzalisha nishati, mfano Tanzania kuna vyanzo kama vile jua, maji na gesi asilia. Hata hivyo barani humo hakuna uhuru wa kutumia makaa ya mawe licha ya kuwepo kwa kiwango kikubwa pamoja na kuwa nchi kubwa duniani zinaweza kufanya hivyo.

“ Hivyo iangaliwe namna kwa kila nchi kutumia raslimali zake ili kuzalisha nishati, mfumo uliopo unazifanya nchi zote kuwa sawa lakini ukweli ni kwamba hatuko sawa. Kwa mfano Afrika inachangia asilimia 3 hadi 4 pekee ya uchafuzi wa mazingira, lakini imepewa mzigo mkubwa zaidi.” Amesema Dkt. Biteko.


Amesisitiza” Kila nchi itumie utaratibu wake wa kuzalisha nishati lakini kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa mazingira.”

Amezungumzia uhusiano  mzuri uliopo wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Urusi na kusema kuwa uendelee kuwa wa kuheshimiana na kukubaliana.


Ambapo ametaja manufaa yake kuwa ni  pamoja na kubadilishana ujuzi na kuisaidia Tanzania katika mitaji ya  miradi nishati.

Amebainisha kuwa Tanzania ina mpango wa kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya kuzalisha takribani megawati 120 za umeme.


Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Urusi, Mhe. Sergey Tsivilev amesema kuwa Rais wa nchi hiyo Mhe. Vladimir Putin amekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha zinaungana na nchi zingine katika kupatia ufumbuzi  changamoto za masuala ya nishati.

Naye, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya African Energy Chamber, Bw. NJ Ayuk amesema kuwa ni muhimu kwa nchi za Afrika na Urusi kuungana na kuhakikisha sauti ya Afrika inasikika na kutekeleza wanayokubaliana ili wote waweze kunufaika na uhusiano kati yao.


Aidha, ameiomba Serikali ya Urusi kuwezesha kampuni kutoka nchini humo ili ziweze kuwekeza zaidi Afrika hususan katika sekta ya nishati.



Pia, ameipongeza Tanzania katika hatua iliyopiga na mafanikio yake katika sekta ya nishati  sambamba na kutoa wito kwa nchi za Afrika kujifunza zaidi kutokana na mafanikio yaliyopo nchini Urusi.


Jukwaa hilo la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg linatarajiwa kuwa na washiriki kutoka takribani nchi 140.


Mwisho.

TANZANIA NA BENKI YA DUNIA WAJADILIANA UTEKELEZAJI MPANGO MAHSUSI WA NISHATI WA MISHENI 300

June 19, 2025 Add Comment


📌 *Mhandisi Mramba aeleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kutekeleza Misheni 300*


📌 *Benki ya Dunia yapongeza*


📌 *Yaahidi kuendelea kuiunga mkono Tanzania*



Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felichesmi Mramba amekutana na Viongozi Waandamizi kutoka Benki ya Dunia ( WB) kwa lengo la kujadili hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa Mpango Mahsusi wa kuwafikishia  umeme Waafrika milioni 300 ifikapo 2030 ujulikanao kama Misheni 300.


Kikao hicho kimefanyika  katika Jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini kando ya Mkutano wa Jukwaa la Nishati Afrika ambapo Tanzania inashiriki.


 Mhandisi Mramba ameeleza kuwa, katika Mpango huo uliosainiwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika mwezi Januari 2025, Tanzania kwa upande wake imeuweka Mpango huo kwenye mipango yake ya Serikali ili kutimiza malengo yaliyowekwa.


Amesema  kukamilika kwa Mpango huo kutaiwezesha Tanzania kuongeza upatikanaji umeme kutoka asilimia 78.4 ya sasa hadi asilmia 100 ifikapo mwaka 2030 na kuongeza matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia hadi kufikia asilimia 75 ifikapo 2030.


Kwa upande wao, Watendaji wa Benki ya Dunia, Bi.Yadviga Semikolenova, Meneja Mtendaji Ukanda wa  Kusini Mashariki mwa Afrika pamoja na Dkt. Rhonda  Antoine, Mtaalam Mwandamizi wa Nishati Ukanda wa Afrika wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua inazochukua ili kuhakikisha Mpango wa Misheni 300 unafanikiwa na hivyo kuwezesha wananchi kupata nishati ya uhakika. 

Aidha, Benki ya Dunia imeonyesha utayari wa kuendelea kuunga mkono juhudi  zinazofanywa na Tanzania  kuhakikisha inaendelea kuutekeleza mpango wa Misheni 300.


Katika kikao hicho, Mhandisi Mramba aliambatana na Mhandisi Innocent Luoga, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO, REA, TPDC na EWURA

WADAU WA CHANJO ZA MIFUGO AFRIKA WATEMBELEA KIWANDA CHA HESTER BIOSCIENCES TANZANIA

June 19, 2025 Add Comment
Na Daudi Nyingo

Kiwanda cha Hester Biosciences Africa Limited kilichopo katika Eneo la Viwanda la TAMCO, Kibaha – Mkoa wa Pwani, kimepokea ugeni wa wasajili wa chanjo na wakurugenzi wa uzalishaji wa chanjo za mifugo kutoka nchi 25 za Afrika terehe 18 Juni 2025. 

TADB na TWCC Waingia Mkataba Kuinua Wanawake na Vijana Kwenye Kilimo

June 18, 2025 Add Comment
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeingia makubaliano na Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) kwa lengo la kuwawezesha wanawake na vijana wajasiriamali wanaoshiriki katika minyororo ya thamani ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.

JUKWAA LA NNE LA UTEKELEZAJI WA USHIRIKISHWAJI WA WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI LILETE MABADILIKO -OLLAL

June 18, 2025 Add Comment


MWANZA


Wadau wa madini nchini wametakiwa kutumia Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta la Madini kama kichocheo cha mabadiliko katika Sekta ya Madini hasa kwenye eneo la ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini  katika eneo la ajira na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini kama vile  usambazaji wa vifaa na  vyakula.

Hayo yamesemwa jijini Mwanza leo Juni 18, 2025 na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini, Augustine Ollal kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo wakati akifunga Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta la Madini.


Jukwaa hilo lililoanza mapema Juni 16, 2025 limekutanisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na  Wizara ya Madini na Taasisi zake, Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Taasisi za Fedha, Kampuni za Uchimbaji wa Madini na Watoa Huduma kwenye Migodi ya Madini.


Amesema kufanyika kwa jukwaa hilo ni mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Madini kuhamasisha ushiriki wa watanzania katika shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini na usambazaji wa bidhaa na huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ili wananchi waendelee kunufaika na rasilimali madini na kukuza uchumi wa nchi.

Katika hatua nyingine, amezitaka kampuni za madini kuendelea kutoa kipaumbele kwa watanzania kwenye  ajira na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.

Wakati huo huo amempongeza Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde kwa kutafsiri maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hali iliyopelekea mchango wake katika Pato la Taifa kufikia asilimia 10.1.

 Jukwaa hilo lenye kaulimbiu inayosema Ongezeko la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ni chachu ya Ukuaji wa Uchumi limeambatana na maonesho yenye lengo la kuelimisha kuhusu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini.