ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 107 ZAKAMILISHA USAMBAZAJI UMEME VIJIJINI SIMIYU

June 18, 2025 Add Comment


*📌Kapinga asema sasa Serikali inapeleka umeme kwenye Vitongoji 638*


*📌Ataja miradi ya kuimarisha umeme Simiyu*


📌 *Simiyu yapata mitungi ya gesi 16,275 kwa bei ya ruzuku*


Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati imetumia takribani shilingi  bilioni 107.36 kupeleka umeme kwenye Vijiji vyote  474 vya Mkoa wa Simiyu. 


Kapinga ameyasema hayo leo Juni 18, 2025 wakati akitoa tathmini ya hali ya upatikanaji wa umeme Mkoa wa Simiyu na maendeleo ya usambazaji wa nishati safi ya kupikia wakati wa kuhitimisha ziara  ya kikazi ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Simiyu. 

"Mheshimiwa Rais baada ya kumaliza upelekaji wa umeme kwenye Vijiji, hivi sasa tunapeleka umeme kwenye Vitongoji na hivi sasa tunatekeleza miradi ya umeme kwenye Vitongoji 638 kati ya Vitongoji 1,408 vya Mkoa wa Simiyu”. Amesema Mhe. Kapinga


Ameongeza kuwa Serikali itajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Simiyu kupitia mradi wa gridi imara na kuongeza kuwa hivi sasa Mkoa wa Simiyu unapata huduma ya umeme kutoka Mikoa mitatu ya Shinyanga, Mwanza na Mara.

Amesema kituo hicho kitazidi kuimarisha hali ya umeme Simiyu na hivyo kuwa muhimu kwa maendeleo ya watu wa Simiyu. 


Amesema mradi wa gridi imara  mkoani Simiyu una sehemu mbili ambazo ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Ibadakuli Shinyanga hadi Bariadi utakaojengwa kwa takribani shilingi bilioni 48 na ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Bariadi kitakachojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 49.

Ameongeza kuwa, kukamilika kwa mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme Mkoa wa Simiyu utawezesha Mkoa kuwa na  uwezo wa megawati 150.

Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Kapinga amesema Mkoa wa Simiyu umepata mitungi ya gesi ya  ruzuku takribani 16,275 ambayo yote tayari imeshachukuliwa na wananchi kwa bei ya ruzuku.



WAENDELEZAJI WA MRADI WA KUZALISHA UMEME WA LUPALI MKOANI NJOMBE WAELEKEZWA KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA WA MRADI

June 18, 2025 Add Comment
-Waishukuru REA kwa uwezeshaji wa zaidi ya shilingi bilioni 4.3

-Utekelezwaji wake wafikia 97.5%

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu ameelekeza waendelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa kilowati 317 kwa kutumia maporomoko ya Mto Lupali kuimarisha ulinzi na usalama wa mradi ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Ameelekeza hayo Juni 18, 2025 katika Kata ya Matola Wilaya ya Njombe Mkoani Njombe alipofanya ziara iliyolenga kujionea maendeleo ya utekelezaji wa Mradi huo unaosimamiwa na Watawa wa Kanisa Katoliki wa Shirika la Wabenediktini, Imiliwaha Njombe kwa ufadhili wa REA.

"Mradi huu hadi kufikia hatua hii umetumia gharama kubwa, na ni mradi utakaokuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa maeneo haya na Taifa kwa ujumla, tuna kila sababu ya kuhakikisha unalindwa," alielekeza Balozi Kingu.

Alielekeza kujengwa kwa uzio utakaozunguka bwawa la kuzalishia umeme sambamba na kusimika mifumo ya taa na kamera maalum za ulinzi maarufu kama CCTV Camera maeneo yote muhimu ya mradi.

Sambamba na hilo, Balozi Kingu aliwapongeza kwa hatua waliyofikia na aliwaelekeza waendelezaji wa mradi huo kushirikiana kwa karibu na waendelezaji wa miradi mingine ili kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa miradi.

"Hapa mmezungukwa na waendelezaji wa miradi ya namna hii wenye uzoefu, ni vyema mkajenga utaratibu wa kuwa mnabadilishana uzoefu ili kuimarisha uendeshaji wa mradi," alisisitiza Balozi Kingu.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mratibu wa Mradi, Sista Imakulata Mlowe alitoa shukrani kwa uwezeshwaji unaofanywa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na aliahidi kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Balozi Kingu.

"Tangu kuanza kwa mradi mwaka 2011, REA imetuwezesha sehemu kubwa katika hatua zote; tunaahidi kutimiza maelekezo yote yaliyotolewa," alisema Sista Mlowe.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage alisema hadi sasa REA imewezesha zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi.

"REA imetoa ruzuku kwa awamu tofauti kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo wakiwemo benki ya Dunia na Serikali ya Sweden ili kuwezesha mradi huu tangu hatua za mwanzo za utafiti wa awali, ujenzi wa njia kuu za kusafirisha na kusambaza umeme kwa watumiaji takriban 600.

Mhandisi Advera alibainisha maeneo mengine yaliyowezeshwa na REA kuwa ni pamoja na ruzuku iliyotolewa kukamilisha mradi ikihusisha ujenzi wa sehemu ya kupokelea maji, nyumba ya mtambo, uwekaji wa mabomba pamoja na shughuli nyingine za Mradi.

Alisema kukamilika kwa mradi kutazalisha kiasi cha kilowati 317 ambazo kiasi zitatumiwa na mwendelezaji na kiasi kitakachobaki zitaingizwa katika Gridi ya Taifa.

Alisema kuwa REA imeendelea kufadhili miradi ambayo itaongeza wigo wa Gridi ya Taifa ili kukuza uchumi wa Taifa kwa kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi.

"REA imefadhili miradi ya uzalishaji na usambazaji nishati vijijini inayotekelezwa na taasisi mbalimbali za Serikali na Sekta Binafsi kwa kutoa ruzuku pamoja na kuwezesha mikopo ya masharti nafuu sambamba na kuwajengea uwezo waendelezaji wa miradi," alisisitiza Mha. Mwijage.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu yupo Mkoani Njombe kwa ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya uzalishaji na usambazaji wa umeme inayowezeshwa na REA.






MEATU MTAENDEA KUPATA MIRADI MIKUBWA YA MAENDELEO IKIWEMO NISHATI -DKT.SAMIA

June 18, 2025 Add Comment


*📌Asema baada ya Vijiji vyote Meatu kupata umeme kasi inaelekea vitongojini*


📌 *Ataka umeme utumike kuongeza thamani ya mazao, kilimo na ufugaji*.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani amesema Serikali imeendelea kupeleka maendeleo katika Wilaya ya Meatu ikiwemo ukamilishaji wa usambazaji  umeme katika Vijiji vyote 109 vya Wilaya hiyo.


Dkt. Samia ameyasema hayo Juni 17, 2025 Wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu akiwa kwenye ziara ya kikazi.

"Kama tulivyoahidi, hatujaishia hapo, kazi ya usambazaji umeme sasa inaendelea kwenye vitongoji lakini pamoja na jitihada hizi zote ninafahamu kuna changamoto ya umeme kutokuwa na nguvu ambayo inatatuliwa." Amesema Dkt. Samia

Ameeleza kuwa, Wizara ya Nishati inatatua   changamoto hiyo  ya umeme kutokuwa na nguvu  kwa kujenga  njia ya kusafirisha umeme kutoka Shinyanga hadi Simiyu na ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme. 

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutapelekea uwepo wa umeme wenye nguvu na wa kutosha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uzalishaji ikiwemo Viwanda.

Amesisitiza kuwa, lengo la Serikali ni kuona wananchi wanatumia nishati ya umeme kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kuongeza thamani ya mazao, kilimo na ufugaji.



Wazalishaji wa Chanjo za Mifugo Kuungana Afrika Waandaa Mwongozo wa Kudhibiti Chanjo

June 17, 2025 Add Comment
Na Daudi Nyingo, Dar es Salaam

Wasajili wa Chanjo na Wakurugenzi wanaosimamia uzalishaji wa chanjo za mifugo kutoka nchi 25 za ukanda wa Afrika wamekutana nchini Tanzania kujadili namna ya kuwa na mfumo wa pamoja wa kutokomeza ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo. Mkutano huu umeanza tarehe 16 hadi 20 Juni 2025 katika Ukumbi wa King Jada Hotel uliopo jijini Dar es Salaam.

MRAMBA AWASILI NCHINI AFRIKA KUSINI KUSHIRIKI JUKWAA LA NISHATI AFRIKA 2025

June 17, 2025 Add Comment

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felichesm Mramba amewasili nchini Afrika ya Kusini kushiriki Jukwaa la Nishati Afrika 2025 ambalo ambalo litaangalia masuala mbalimbali ya Nishati ikiwemo Nishati Safi ya Kupikia.

Jukwaa hilo linaanza leo Juni 17,2025 na linatarajiwa kumalizika Juni 20,2025.

Nchini Afrika Kusini, Mhandisi Mramba ameambata na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia Wizara ya Nishati Bw. Nolasco Mlay sambamba na wataalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini ( REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).