TUME YA UCHAGUZI YAPONGEZWA MAANDALIZI UCHAGUZI MKUU 2025

June 09, 2025 Add Comment

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonaz akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kilichokutana Mjini Unguja Zanzibar leo Juni 9,2025.
 
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Tume akizungumza mapema kabla ya ufunguzi wa kikao hicho.




Wajumbe wa Baraza hilo wakifuatilia mada katika Mkutano huo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonaz (kulia) akizungumza jambo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Tume, Ramadhani Kailima,  wakati Katibu Mkuu huyo alipofika kufungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Tume Mjini Unguja, Zanzibar leo Juni 9,2025.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonaz (kushoto)  na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Tume, Ramadhani Kailima,  pamoja na wajumbe wa baraza la Wafanyakazi la Tume wakiimba wimbo wa wafanyakazi wakati kabla ya kuanza kikao cha Baraza la Wafanyakazi  Mjini Unguja, Zanzibar leo Juni 9,2025. 


Na. Mwandishi Wetu, Zanzibar
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonaz ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kukamilisha zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuendelea vyema na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
 
Dkt. Yonazi ametoa pongezi hizo leo tarehe 09 Juni, 2025 Kisiwani Unguja, Zanzibar wakati wa kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la INEC,  ambapo imewaasa viongozi wa Tume kuendelea kuwa imara na kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unakwenda vizuri.
 
“Kwanza niwapongeze sana kwa kukutekeleza jukumu hili kubwa ambalo mmekabidhiwa na Taifa letu na kwa namna ya pekee kabisa Mwenyekiti wa Baraza unifikishie salamu za pongezi kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele pamoja na wajumbe wa Tume kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya katika kuhakikisha kuwa shughuli za uchaguzi nchini kwetu zinakwenda vizuri,” amesema Dkt. Yonazi.
 
Ameeleza kuridhishwa na jinsi Tume ilivyotekeleza kwa ufanisi zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuongeza kuwa ni matarajio ya Serikali kuwa utendaji huo mzuri wa Tume utaendelea kwa viwango vya juu kwa mujibu wa katiba, sheria na taratibu mbalimbali ambazo zimewekwa.
 
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhan amesema tayari Tume imekamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo kwa sasa inaendelea na uboreshaji wa awamu ya pili.
 
“Tume imeshakamilisha uboreshaji wa awamu ya kwanza na imeshachakata na kutoa daftari la awali na imeshakamilisha uboreshaji wa awamu ya pili mzunguko wa kwanza na mzunguko wa pili. Tunategemea kuanzia tarehe 28 mwezi huu (tarehe 28 Juni, 2025) tutaanza mzunguko wa tatu wa uboreshaji katika Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar na Magereza Tanzania Bara kwa wanafunzi na wafungwa waliohukumiwa kifungo chini ya miezi sita,” amesema Kailima.
 
Katibu huyo wa Baraza amesema mzunguko huo wa tatu utahusisha vituo 140 vya kuandikisha wapiga kura ambapo 130 vipo kwenye magereza Tanzania Bara na vituo 10 vipo kwenye vyuo vya mafunzo Tanzania Zanzibar. Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika kwa siku saba hadi tarehe 04 Julai, 2025.
 
Ameongeza kuwa Tume imekamilisha maandalizi ya nyaraka mbalimbli kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ikiwa ni pamoja na Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 na maelekezo mbalimbali kwa ajili ya watendaji wa uchaguzi na wadau wa uchaguzi kupata miongozo kwa ajili ya utekelezaji wa uchaguzi.
 
Alimkumbusha mgeni rasmi kuwa tayari Tume imekamilisha zoezi la ugawaji wa majimbo na kwamba kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutakuwa na jumla ya majimbo 272 yatakayofanya uchaguzi wa wabunge katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kata 3960 kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani kwa Tanzania Bara.

MRADI WA KUZALISHA UMEME WA JUA KISHAPU WAFIKIA ASILIMIA 63.3-MD TWANGE

June 09, 2025 Add Comment


📌Asema awamu ya kwanza utazalisha Megawati 50 na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa


Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange amesema Mradi wa uzalishaji umeme unaotokana na jua wa Kishapu Mkoani Shinyanga umefikia asilimia 63.3 kukamilika ambapo amesema awamu ya kwanza ya Mradi huo utazalisha Megawati 50 ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwishoni mwa mwezi wa kumi mwaka huu.

MD Twange ameyasema hayo leo Juni 8 mwaka 2025 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo ambao unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 118 kwa awamu ya kwanza huku awamu ya pili ikitarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 204.

‘’Kwanza tunamshukuru Mhe. Rais kwa kutupatia fedha kwa awamu zote, kama mnavyoona kazi inaendelea na Mradi unatarajia kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa mwishoni mwa mwezi wa kumi kwa ajili ya kuwasambazia umeme wananchi, lakini pia tuko katika hatua  za mwisho za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakayetekeleza Mradi kwa  awamu ya pili ambayo itazalisha megati 100’’ alisisitiza Mkurugenzi Mtendaji Twange.

Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa TANESCO inafanya jitihada za makusudi za kuhakikisha Mradi unakamilika kwa wakati  ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya watu na shughuli za uwekezaji ambazo zinategemea nishati ya umeme kujiendesha.

Naye Meneja wa Mradi huo Mhandisi Emmanuel Andarson amesema awali Mradi huo ulipaswa kukamilika mwezi  February mwaka huu lakini Mkandarasi aliongezewa muda baada kukabiliwa na baadhi ya changamoto ambapo ameahidi kukamilisha Mradi huo kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba .

Mradi wa uzalishaji wa umeme unaotokana na nguvu ya jua wa Kishapu uliopo katika Kijiji cha Ngunga Mkoani Shinyanga ulianza utekelezaji wake Desemba 8  mwaka 2023 na unatarajia kukamilika rasmi Oktoba 29 2025 ambapo unagharimu jumla ya shilingi bililioni 323 kwa awamu zote mbili ukitarajia kuzalisha megawati 150 za umeme.



MRADI WA KUZALISHA UMEME WA JUA KISHAPU WAFIKIA ASILIMIA 63.3 - MD TWANGE

June 08, 2025 Add Comment


📌Asema awamu ya kwanza utazalisha Megawati 50 na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange amesema Mradi wa uzalishaji umeme unaotokana na jua wa Kishapu Mkoani Shinyanga umefikia asilimia 63.3 kukamilika ambapo amesema awamu ya kwanza ya Mradi huo utazalisha Megawati 50 ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwishoni mwa mwezi wa kumi mwaka huu.

MD Twange ameyasema hayo leo Juni 8 mwaka 2025 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo ambao unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 118 kwa awamu ya kwanza huku awamu ya pili ikitarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 204.

‘’Kwanza tunamshukuru Mhe. Rais kwa kutupatia fedha kwa awamu zote, kama mnavyoona kazi inaendelea na Mradi unatarajia kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa mwishoni mwa mwezi wa kumi kwa ajili ya kuwasambazia umeme wananchi, lakini pia tuko katika hatua  za mwisho za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakayetekeleza Mradi kwa  awamu ya pili ambayo itazalisha megati 100’’ alisisitiza Mkurugenzi Mtendaji Twange.

Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa TANESCO inafanya jitihada za makusudi za kuhakikisha Mradi unakamilika kwa wakati  ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya watu na shughuli za uwekezaji ambazo zinategemea nishati ya umeme kujiendesha.



Naye Meneja wa Mradi huo Mhandisi Emmanuel Andarson amesema awali Mradi huo ulipaswa kukamilika mwezi  February mwaka huu lakini Mkandarasi aliongezewa muda baada kukabiliwa na baadhi ya changamoto ambapo ameahidi kukamilisha Mradi huo kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba .

Mradi wa uzalishaji wa umeme unaotokana na nguvu ya jua wa Kishapu uliopo katika Kijiji cha Ngunga Mkoani Shinyanga ulianza utekelezaji wake Desemba 8  mwaka 2023 na unatarajia kukamilika rasmi Oktoba 29 2025 ambapo unagharimu jumla ya shilingi bililioni 323 kwa awamu zote mbili ukitarajia kuzalisha megawati 150 za umeme.m



MAANDALIZI YA MAC D BONANZA YAKAMILIKA ,WASHIRIKI WAVUKA LENGO

June 08, 2025 Add Comment


Maandalizi ya Mac D Bonanza 2025 & Fun Run (Mbio za kujifurahisha) yamekamilika kwa asilimia kubwa huku washiriki wa mbio za kujifurahisha wakivuka lengo la wakimbiaji lililowekwa jambo linaonyesha kuwapo na mwamko kubwa wa watu kushiriki tamasha hilo litakalofanyika Juni 7, 2025.


Akiongea leo Jijini Dar es Salaam kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa Eb Twenty Five, Mratibu wa Mac D Bonanza Denzel Rweyunga amesema wamefurahishwa na namna jamii ilivyohamasika katika kushiriki Bonanza hilo kwa mwaka huu.


“Sisi waandaaji tulijiwekea lengo la kupata washiriki wa mbio za kujifurahisha 700 tu, lakini kutokana na mwamko mkubwa wa jamii na hamasa iliyokuwapo mitaani hadi kufikia leo tuna idadi ya washiriki zaidi ya 1,800,” alisema Denzel.

Amesema kwamba kwa sasa zoezi la kutoa fulana bure na namba za washiriki waliojisajili kwa ajili ya kukimbia mbio za Kilomita 10 na Kilomita 5 nalo linaenda vizuri ambapo washiriki wengi wameshachukua fulana zao katika vituo mbalimbali tayari kwa maandalizi mbio.


Ameeleza kuwa mgeni rasmi wa Mac D Bonanza 2025, ambalo litafanyika katika viwanja vya Chuo Cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Kunduchi, likishirikisha mbio za kujifurahisha, burudani na baadae jioni mchezo wa soka kati  ya Mac D FC na IPP Media, atakuwa Mhe. Hamis Mwinjuma, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi Calvin Obeld amesema amesema kwamba mbio zitaanza 12:00 asubuhi kwa mbio za Kilomita 10 na kufuatiwa na mbio za Kilomita 5, ambapo  zitaanzia katika viwanja vya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichopo Kunduchi na kuhitimishwa katika viwanja hivyo hivyo.


Mac D Bonanza 2025 inadhaminiwa na Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB ), Isumba Trans Limited ( ITL ), Kilimanjaro Water, Namis Corporate Limited, JC Hall, Zakys Bay, Pwani Inland Clearance Deport Ltd PICD) na EB Twenty Five na ITV & Radio One.

DKT.BITEKO AELEZA MAPINDUZI YALIYOFANYWA NA SERIKALI SEKTA YA ELIMU

June 08, 2025 Add Comment


📌 Ataka CWT wasigawanyike, ahimiza amani, upendo na mshikamano*


📌 Serikali kuendelea kuajiri walimu kila mwaka


📌 Serikali ya Awamu ya Sita yajenga madarasa 62,685 ya shule za msingi na sekondari, shule mpya za msingi na sekondari 2,611 na nyumba za walimu 1,792


📌 Serikali kufanyia tathmini ombi la kuwa na chombo kimoja cha kusimamia walimu nchini


📌 CWT yaipongeza Serikali kwa kuendelea kulipa stahiki za walimu


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Serikali imeendelea kutambua mchango wa walimu katika maendeleo ya sekta ya elimu kwani ni wazalishaji wa watalaamu mbalimbali waliopo katika sekta zote ikiwemo afya, nishati, sayansi na teknolojia. Sambamba na kufanya maboresho yatakayowaongezea walimu ari ya kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na kutanguliza mbele maslahi ya Taifa.


Mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo yanachangiwa moja kwa moja na walimu. Hivyo, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kina mchango mkubwa kwa jamii na kwa Taifa kwa ujumla kwa kuwa pamoja na jukumu la kufundisha na kujengea watu maarifa, mwalimu ni mzazi wa kiroho, kiongozi wa fikra, na ni mjenzi wa maadili katika jamii.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko Juni 8, 2025 jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT).


Amesema katika kuimarisha sekta ya elimu ili kuongeza ufanisi na kusogeza huduma kwa jamii. Serikali imefanikiwa kujenga jumla ya madarasa 62,685 kwa shule za msingi na sekondari, shule mapya za sekondari 1,031, shule mpya za msingi 1,580 na nyumba za walimu 1,792.



Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2024/25, Serikali imefanikiwa kuwalipa malimbikizo ya mishahara walimu 101,596, kulipa watumishi 156,556 madeni yasiyo ya mishahara na kuongeza mshahara kwa watumishi wa umma ambapo kima cha chini kuanzia mwezi Julai, 2025 kitakuwa shilini 500,000 badala ya 370,000.


“Serikali inaendelea kutoa ajira za walimu ambapo kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, jumla ya walimu 40,527 wameajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini. Lengo la kufanya hivi ni kutatua changamoto mbalimbali zilizopo,” amesema Dkt. Biteko.


Amepongeza matokeo ya zoezi la ‘Samia Teachers Mobile Clinic’  kwa kuwafikia walimu 48,380 pamoja na kutatua kero zao huku akiwaomba kuongeza ubunifu utakaowawezesha kuwa na mikakati mingine yenye lengo la kuimarisha utendaji katika sekta ya elimu na kushirikiana na Serikali kwa kutekeleza miradi ya Elimu ya TEHAMA kwa walimu na miradi mingine isambae  kwenye mikoa yote nchini.

Kuhusu ombi la walimu kuwa na mwajiri mmoja anayeshughulikia masuala yote ya walimu ili kuimarisha ufanisi katika kuwasimamia. Dkt. Biteko amesema Serikali imelipokea ombi hilo na italifanyia tathmini ili kubaini endapo utaratibu uliopo sasa una changamoto zinazolazimu kutatuliwa kwa kuanzisha chombo kitakachosimamia walimu wote nchini.


Amezungumzia utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa na kusema kuwa lengo lake ni kukuza elimu inayotolewa nchini na kuwafanya wanafunzi waweze kujitegemea wanapomaliza masomo yao. Aidha, Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa walimu wote wanapata mafunzo ili waweze kuendana na mabadiliko hayo. 


Fauka ya hayo, kufuatia kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa CWT, amewasihi wajumbe wa Mkutano huo kutumia haki yao katika kuchagua viongozi watakaowaongoza vyema na kuwataletea maendeleo pamoja  wagombea kuomba kura kwa heshimiana.

  


“ Nawasihi kuendelea kusimamia misingi ya haki, usawa na uwazi hususan wakati wa majadiliano na utatuzi wa masuala yote yanayohusu chama chenu. Niwaombe watakaoshinda msiwanange watakaoshindwa na mtakaokosa nafasi msikasirike, asitokee mtu wa kuwagawanya, msigawanyike hii ni taalamu ya pili ya uumbaji, mshikamane, mpendane na mshirikiane,” amesisitiza Dkt. Biteko.


Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema kuwa Serikali inathamini mchango wa walimu katika mipango mbalimbali ya Taifa na kuahidi kuendeleza ushirikiano mzuri kwa ajili ya ujenzi wa Taifa na uchumi imara.

Kupitia mkutano huo, Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania, Leah Ulaya amempongeza Rais Samia kwa utendaji kazi wake na kuahidi kuwa CWT itaendelea kushirikiana na Serikali .


Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Joseph Misalaba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kulipa stahiki mbalimbali za walimu ambapo walimu wamenufaika kwa kupandishwa vyeo, ulipwaji wa malimbikizo ya mishahara na madeni yasiyo ya mishahara.


“ Kwa niaba ya watumishi wa Tanzania hususan walimu wote tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusikiliza kilio cha wafanyakazi juu ya suala la kikokotoo cha mafao ya kustaafu na kuridhia kuboresha kikokotoo kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40. Chama cha Walimu Tanzania kinaiomba Serikali yako iendelee kufanya maboresho zaidi ili kuleta ustawi wa walimu wetu wastaafu ambao wameitumikia nchi yao kwa uaminifu mkubwa,” amesema Misalaba.

Amefafanua kuwa CWT ni chama cha wafanyakazi ambacho msingi wake mkubwa ni kutetea haki na maslahi ya wanachama wake. Kama mdau wa elimu CWT itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa elimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu nchini.


Aidha, Mkutano huo wa mwaka wa CWT umehudhuriwa pia na wawakilishi wa vyama vya walimu kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Afrika Kusini na Namibia. 


Mwisho