ZAO LA PAMBA LINAWEZA KUPUNGUZA UMASKINI KUANZIA NGAZI YA KAYA MPAKA TAIFA

June 03, 2025 Add Comment

 


Na Oscar Assenga,TANGA

WANANCHI wanaoishi kwenye maeneo yanayostahimili kilimo cha Pamba wametakiwa kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo ambalo ni la kimkakati la kibiashara kutokana na kwamba linaweza kusaidia kupunguza kiasi cha umaskini kwenye ngazi ya kaya,wilaya na Taifa kwa ujumla

Hayo yalisemwa jana na Afisa wa Bodi ya Pamba Tanzania Alphonce Ngawagala wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya 12 ya Biashara na Utalii yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwahako Jijini Tanga.

Alisema kwamba leng la wao kushiriki kwenye maonyesho hayo ni kutangaza fursa zinazopatikana kwenye bodi hiyo kwa kuwaelimisha wananchi maeneo gani yanafaa kulima pamba na pembejeo  zinapatikana kwa utaratibu upi ambao ni bure.

Alisem kwamba pia baada ya mkulima na kuvuna wanaanzisha soko la mkulima ili aweze kuuza mazao yake kwa wakati ili aongeze kipato chake apate awekeze kwenye mambo mengine ya kimaendeleo.

Aidha alisema kwamba bodi hiyo imepewa dhamana ya kusimamia usindikaji,uzalishaji na kusimamia masoko pamoja na kuelimisha wananchi maeneo yanayotakiwa kulimwa pamba na pembejeo zinapatikana kwa utararibu upi ambao ni bure na baadae ya kulima hizo wao wanasimamia soko ili wakulima wauze.

“Lakini uchakataji wa Pamba inapokwenda kiwandani napo bodi ipo  kwa ajili ya kusimamia inasimamia kuhakikisha shughuli zote zinafuata utaratibu, sheria na kanuni zilizowekwa ikiwemo kuangalia ubora na usafi unapatikani”Alisema

Alisema wanafanya hivyo ili kumuwezesha yule mchambuaji baada ya kumaliza taratibu zake aweze kupata kibali kama maborota yake yanapelekwa nje ya nchi apeleke kwa wakati kwa kukamailisha tararibu zote.

Mwisho.

VITONGOJI 284 ARUMERU MASHARIKI VYAFIKIWA NA UMEME

June 03, 2025 Add Comment

*📌  Ni kati ya Vitongoji 330 vya Jimbo la Arumeru Mashariki.*


*📌Kapinga asema upelekaji umeme unafanyika kwa  awamu kulingana na upatikanaji wa fedha*


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imevifikishia huduma ya umeme Vitongoji 284 katika Jimbo la Arumeru Mashariki kati ya Vitongoji 330.


Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Juni 03, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mhe. Dkt. John Danielson Pallangyo aliyeuliza ni  lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme wa REA katika Vitongoji 37 ambavyo vipo gizani katika Jimbo la Arumeru Mashariki.

 


"Mheshimiwa Mwenyekiti, Vitongoji 17 vipo katika hatua ya utekelezaji kupitia Mradi wa Ujazilizi (Densification IIB) na mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji Awamu ya Pili  A (HEP IIA), aidha, katika Vitongoji 29 zabuni imetangazwa ili kupata Wakandarasi wa kutekeleza miradi kupitia mradi wa kupeleka umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB). 


Amesema kukamilika kwa miradi hiyo, kutawezesha vitongoji vyote vya Jimbo la Arumeru Mashariki kufikiwa na umeme.


Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mhe. Dkt.John Danielson Pallangyo aliyeuliza kuhusu  Kata za Arumeru Mashariki zinazo pata maji kutoka msitu wa mlima Arumeru na kuwa na  flouride ambapo Kampuni ya Kweka imejitolea kuweka mtambo wa kusafisha lakini kinachohitajika ni umeme,   Mhe. Kapinga amesema tayari Serikali imetenga fedha katika mwaka ujao wa fedha kukipelekea umeme wa uhakika Kitongoji cha Seneto Kata ya Legeruki kwa ajili ya kutibu flouride katika maji.

Akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Mhe. Profesa Patrick Alois Ndakidemi aliyeuliza Serikali itakiunganishia lini umeme Kitongoji cha Orera kilichopo Kijiji cha Mweka, Mhe. Kapinga amesema katika Jimbo la Moshi Vijijini yupo Mkandarasi anayetekeleza miradi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji 15 vya kila Mbunge na kuongeza kuwa kitongoji hicho kipo katika orodha hiyo ya Mkandarasi.


Akijibu swali la Mbunge wa Kondoa Mjini, Mhe. Ally Makoa aliyeuliza Serikali itapeleka lini umeme kwenye mitaa ya Mongoroma, Chandimo na Hachi,  Mhe. Kapinga amesema Serikali imeipelekea umeme mitaa ya Kondoa Mjini ambapo imebaki mitaa hiyo mitatu na kuongeza kuwa itatengwa fedha katika bajeti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuifikishia mitaa hiyo umeme.


Mhe. Kapinga ameongeza kuwa upelekaji wa umeme unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na bajeti ambayo imetengwa.


Akijibu swali la Mbunge wa Mwibara, Mhe. Charles Kajage aliyeuliza kuhusu lini Serikali itavipelekea umeme Vitongoji vya Jimbo la Mwibara ambavyo havina umeme, Mhe. Kapinga amesema Jimbo la Mwibara lina miradi ya Vitongoji ambayo inaendelea kutekelezwa. 


Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Rita Kabati aliyeuliza kauli ya Serikali kuhusu uwepo wa nguzo Kata ya Ilula Wilaya ya Kilolo toka mwezi wa 11 mwaka jana na hadi leo umeme haujawaka, Mhe. Kapinga amesema hadi kufikia mwezi wa saba eneo hilo litakuwa limefikiwa na huduma ya umeme.

BALOZI DK.NCHIMBI AMWAKILISHA RAIS SAMIA KUMUAGA HAYATI SONGAMBELE MKOANI RUVUMA

June 02, 2025 Add Comment



Na Mwandishi Wetu,Songea

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika shughuli ya kuaga mwili wa Hayati Alhaj Mustafa Mohamed Songambele iliyofanyika nyumbani kwa marehemu eneo la Mahenge, mjini Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Dkt. Nchimbi amemuelezea Hayati Songambele kama mmoja wa mashujaa waliotoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru wa Tanzania na kujenga misingi ya taifa jipya baada ya ukoloni.


Dk.Nchimbi amesema Hayati Songambele alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Chama cha TANU na alishiriki kikamilifu katika harakati za kujenga taifa huru na lenye mshikamano.


"Tuendelee kujifunza kutoka kwa wazee hawa ambao wamefariki wakiona amani na upendo wa Tanzania ukiendelea, heshima pekee tunayoweza kuwapa ni kuendeleza mshikamano, amani na maendeleo ya nchi yetu…


“Tuendelee kujua sisi ni Taifa moja, tuna wajibu wa kupendana na kujiepusha na vishawishi vyote ambavyo vinaweza vikavuruga amani na kuvunja mtangamano wa kitaifa," alisema Dkt. Nchimbi.


Dkt. Nchimbi aliongeza kuwa Rais Dkt. Samia ameguswa sana na msiba huo, akimwelezea Hayati Songambele kama kiongozi mwenye moyo wa kipekee wa kulitumikia taifa kwa hali na mali, na kwamba wananchi wa Ruvuma wana kila sababu ya kujivunia mchango wake mkubwa.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema kifo cha Mzee Songambele ni pigo kubwa kwa Taifa, akieleza kuwa marehemu alikuwa ni hazina ya busara na kumbukumbu muhimu ya historia ya Tanzania.


"Hakuwa tu kiongozi bali alikuwa taa na mwelekeo katika giza la ukoloni, aliyesimama kidete kwa ujasiri, hekima, na moyo wa kizalendo katika kuijenga Tanzania mpya. Alisimama kwa haki, kupitia juhudi zake na viongozi wenzake wa wakati huo, tunauona leo mwanga wa uhuru, umoja, na amani uliodumu kwa zaidi ya nusu karne," alisema Kanali Ahmed.


Akizungumza kwa niaba ya familia, Mtoto wa Hayati Songambele, Rajab Songambele amesema wataendelea kuyaenzi na kuyatekeleza mema yote waliyofundishwa na Mzee wao ili yadumu kwa vizazi vijavyo.

Hayati Alhaj Mustafa Mohamed Songambele alikuwa ni mmoja wa waanzilishi wa Chama cha TANU akiwa miongoni mwa wanachama wa kwanza 30 wa chama hicho, na alipata kadi ya uanachama namba 27.

Alizaliwa Mei 25, 1925 katika eneo la Bombambili, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma na amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100.






TASAC YATOA ELIMU YA UTUNZAJI MAZINGIRA DODOMA

June 02, 2025 Add Comment



Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania TASAC, leo tarehe 02 Juni, 2025 limetoa elimu ya utunzaji wa mazingira majini kwa wadau waliotembelea banda lao jijini Dodoma.

TASAC imetoa elimu hiyo kwa wadau na wananchi wa Dodoma katika Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani 2025 yanayofanyika kuanzia tarehe 01 - 05 Juni, 2025 jijini humo. 



Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wataalamu wa TASAC wameeleza wananchi namna wanavyotekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na jukumu la kusimamia na kudhibiti Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira pamoja na kupambana na umwagikaji wa mafuta majini.

Baadhi ya wadau waliotembelea banda hilo ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a ambapo amepongeza juhudi za TASAC katika kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

TASAC ni moja ya taasisi za umma zinazoshiriki maadhimisho hayo yenye kauli mbiu: “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki”. Kilele cha maadhimisho hayo ni tarehe 05 Juni 2025.

DKT.BITEKO AZINDUA MKAKATI WA TAIFA WA MAWASILIANO WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

June 02, 2025 Add Comment


📌 *Aagiza usiishie kwenye makabati; ukatekelezwa katika ngazi zote za Serikali/Wadau*


📌 *Atoa wito kwa vyombo vya Habari kuwa mstari wa mbele uhamasishaji wa Nishati Safi ya Kupikia*


📌 *Asema Ajenda ya Rais Samia imeonesha mafanikio; Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia yaongezeka kutoka 6% mpaka 16%*



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia, pamoja na Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na Uelimishaji kuhusu Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na hivyo kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania kuhamia katika matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.

Akizindua Mkakati huo wa Mawasiliano jijini Dodoma, tarehe 2 Juni  2025, Dkt. Biteko ameagiza kuwa mkakati huo usiishie kukaa kwenye makabati bali utekelezwe katika ngazi zote za Serikali hadi ngazi ya mtaa bila kusahau Sekta binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na vyombo vya Habari kuwa mstari wa mbele katika kuutekeleza.


Katika uzinduzi huo, Dkt. Biteko amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara namba moja wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi ambapo kutoka azindue Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia (2024-2034) mnamo tarehe 08 Mei, 2024 matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6 hadi 16. 

“ Katika kuthibitisha jinsi anavyolipa umuhimu suala hili la Nishati Safi ya Kupikia, Mheshimiwa Rais pia ameunda Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia ambacho kina jukumu maalumu la kusimamia ajenda ya nishati safi ya kupikia na kwa kupitia kitengo hiki Serikali itaendelea na shughuli mbalimbali ikiwemo kubuni na kusimamia miradi, pia kusimamia kampeni zote za Kitaifa za uelimishaji na uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia yanaendelea kuathiri afya na maisha ya watumiaji wengi hasa kina mama na watoto chini ya umri wa miaka mitano ambapo taarifa zinaonesha kuwa, watu bilioni 2.1 sawa na asilimia 24.7 ya Watu wote Duniani hawana nishati safi ya kupikia ambapo  kati yao watu Milioni 990 sawa asilimia 47.1 ya wanaotumia nishati isiyo salama wanatoka barani Afrika. 

Ameeleza kuwa, Afrika inalazimika kufunga mkanda katika safari ndefu ya kuelekea kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambapo kwa upande wa Tanzania amesema kuwa kila Taasisi inapaswa kutambua na kutekeleza jukumu lake kikamilifu.

Dkt. Biteko amewasisitiza Wadau wote wanaohusika na Nishati Safi ya Kupikia kuhakikisha kuwa wanandaa na kutekeleza Kampeni zinazolenga makundi maalum katika jamii, kukuza uelewa wa umma kuhusu njia za ufadhili na gharama nafuu, kuhakikisha ujumbe thabiti wenye kueleweka unafika kwa wadau wote na kuendeleza na kuimarisha njia za mawasiliano za kuaminika. 

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia Kitengo cha Tathmini na Ufuatiliaji kufanya tathmini katika kila robo mwaka ili kuweza kujipima juu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amempongeza Rais, Dkt. Samia kwa kuendelea  kuonesha kuwa nishati safi ya kupikia si suala la maneno bali ni vitendo na ndio maana anatambulika duniani kama kinara wa nishati safi ya kupikia.

Amesema kuwa suala la Nishati Safi ya Kupikia ni kipaumbele cha Mkoa wa Dodoma ambapo  juhudi  mbalimbali zinachukuliwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia akitoa mfano kuwa kwa Mkoa wa Dodoma kwa sasa tayari magereza 9 yanatumia nishati safi ya kupikia, shule za VETA 3 na shule 9 za bweni huku kazi ya uhamasishaji ikiendelea.


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema katika kipindi cha miaka minne sekta ya Nishati imekuwa mashuhuri kwa masuala mbalimbali kubwa likiwa ni nishati safi ya kupikia na kueleza kuwa nguvu ya ushawishi ya Rais, Dkt.Samia imefanya ajenda ya nishati safi ya kupikia kukubalika ndani na nje ya nchi na hivyo kutoa hakikisho la usalama wa afya za wananchi na mazingira pia.


Ameongeza kuwa Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa utaongeza kasi za programu za nishati safi ya kupikia na kuleta mapinduzi ya kuhama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia kwenda kwenye nishati safi ya kupikia.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuzinduliwa kwa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.


Ameeleza kuwa Mkakati huo umeandaliwa na  Wizara ya Wizara ya Nishati  kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) ambapo Mkakati huo unaongozwa na kaulimbiu ya kitaifa isemayo “Nishati Safi ya Kupikia, Okoa Maisha na Mazingira”, 


Amesema lengo kuu la mkakati ni kuongeza uelewa wa wananchi na taasisi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na malengo mengine mahususi ni kuandaa na kutekeleza kampeni maalum za uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuhakikisha ujumbe wenye lengo la pamoja unafika kwa wadau wote pamoja na kuendeleza na kuimarisha njia za mawasiliano.


Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo amempongeza Rais, Dkt. Samia kwa kuanzisha gurudumu la Nishati Safi ya Kupikia, pia amempongeza Dkt. Biteko kwa jinsi anavyoongoza Wizara na kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo.


Aidha, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Rodney Thadeus amesema kuwa Wizara hiyo itahakikisha mkakati wa mawasiliano uliozinduliwa unatekelezwa kwa mafanikio kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati pamoja na wadau wengine vikiwemo vyombo vya Habari.


Vilevile, Mshauri wa Rais ( Nishati Safi ya Kupikia na Maendeleo ya Jamii) Angellah Kairuki amepongeza juhudi za serikali katika kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia huku kielelezo mojawapo kikiwa ni uzinduzi wa mkakati wa mawasiliano ambao ni muhimu katika kufikisha ujumbe kwa umma kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Naye, Lamine Diallo, Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali kutoka Umoja wa Ulaya ( EU), ameipongeza Wizara ya Nishati kwa tukio hilo muhimu la kuzindua Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia na kusema kuwa inaonesha kwa vitendo juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia Nishati Safi ya Kupikia.