DC SAME APIGA MARUFUKU MAJI MACHAFU YA KIWANDA KUINGIA MTONI

May 21, 2025 Add Comment

 




Na Ashrack Miraji

Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amepiga marufuku mara moja utiririshaji wa maji machafu yenye kemikali kutoka katika Kiwanda cha kuchakata mkonge kinachomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MELT), kilichopo katika shamba la mkonge la Hassan Sisal Estate, Kata ya Makanya.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia wasiwasi wa uchafuzi wa mazingira na athari za kiafya kwa wakazi wa Makanya na maeneo jirani yanayopata huduma ya maji kupitia mto unaopita karibu na kiwanda hicho.

Mhe. Kasilda alitembelea baadhi ya maeneo ya mto huo na kujionea hali ya maji yaliyobadilika rangi kuwa nyeusi na kutoa harufu kali, hali iliyomsukuma kufika kiwandani kujiridhisha na chanzo cha uchafuzi huo.


“Kuanzia sasa ni marufuku kuelekeza maji machafu yenye kemikali kwenye mto ambao maji yake yanatumika kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu, hususan kilimo na mifugo. Baadhi ya wananchi wanayatumia moja kwa moja,” alisema DC Kasilda.

Alisisitiza kuwa uamuzi huo unalenga kulinda afya za wananchi na mazingira kwa ujumla.

Aidha, Mhe. Kasilda alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same kuhakikisha wataalam wa mazingira na afya wanafika kiwandani hapo kufanya uchunguzi wa kina ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.


“Serikali inathamini uwekezaji, lakini ni lazima wawekezaji wazingatie sheria na taratibu ili kulinda afya za wananchi na kukuza uchumi wa taifa kwa njia endelevu,” alisema.

Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa wilaya pia alieleza kutoridhishwa na hali ya usafi kiwandani hapo na kuwataka wasimamizi wa kiwanda kufanya usafi wa maeneo yao ya kazi ili kuepuka hatari ya magonjwa ya mlipuko kwa wafanyakazi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 129 kinakataza mtu yeyote kuachilia maji taka au taka hatarishi moja kwa moja kwenye mazingira bila kibali au bila kuyatibu.

Sheria hiyo pia inataka viwanda kuwa na mitambo ya kisasa ya kutibu majitaka kabla ya kuyamwaga kwenye mazingira. Endapo ukiukwaji utabainika, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC) itachukua hatua kali dhidi ya wahusika.




 

BENKI YA CRDB KUIWEZESHA ZANZIBAR KUJENGA SHULE 23 ZA GHOROFA

May 21, 2025 Add Comment

 

Zanzibar. Tarehe 21 Mei 2025: Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo baada ya kusaini mkataba wa mkopo nafuu wa takriban Euro milioni 80 (shilingi bilioni 240).

Akizungumza kwenye hafla ya kutiliana saini mkopo huo kati ya Benki ya CRDB na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi amesema maendeleo ya taifa yanahitaji ushirikiano wa serikali na sekta binafsi na Benki ya CRDB imekuwa ikionyesha hilo kwa vitendo kwa kujitoa kwake kila inapohitajika kufanya hivyo.
“Mkopo wa Euro milioni 79.962 utatusaidia kujenga shule 23 za ghorofa mbili. Shule hizi zitajengwa Pemba na Unguja hivyo kusaidia kutatua uhaba wa vyumba vya madarasa kwa kiasi kikubwa. Lengo letu ni kuwaona vijana wetu wanasoma katika mazingira rafiki ya kukua kiumri na kielimu,” amesema Rais Dkt. Mwinyi.


Uboreshaji huu wa mazingira ya shule, Rais amesema ni muhimu ili kuwapata viongozi bora, madaktari, wahandisi, wahasibu, wanasheria na wasomi wengine mahiri hivyo ni lazima kuwekeza kwenye elimu.
“Kila mtu mwenye maono mazuri anatambua umuhimu wa elimu hivyo mkopo huu utakaoboresha miundombinu, umekuja kwa wakati sahihi sasa hivi. Nawapongeza Wizara ya Elimu kwa kulifanikisha hili kwani ilikuwa nikipita wananchi wanaomba shule ya ghorofa kila mahali mpaka kule Tumbatu. Sasa suala hilo limekamilika na fedha za ujenzi wake ndio hizi hapa,” amesema Rais Mwinyi.

Benki ya CRDB imetoa mkopo huo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikishirikiana na Benki ya Deutsche ya nchini Hispania kwa malengo ya kufanikisha ujenzi wa shule hizo zitakazokuwa na madarasa ya kisasa, vyoo bora, bustani za kuvutia, ofisi nadhifu za utawala, maabara na maktaba za kisasa pamoja na viwanja safi vya michezo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Adulmajid Nsekela amesema kwa muda mrefu wamekuwa wadau muhimu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Serikali zote yaani ile la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi mjini au vijijini.


“Kwa hatua tuliyofikia, kwa sasa pande zote yaani Benki ya CRDB, Benki ya Deutsche na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunakamilisha masharti ya awali ya mkopo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi kusudiwa. Ni matumaini yetu kuwa masharti haya ya awali yatakamilishwa kabla ya mwishoni mwa mwezi ujao hivyo kuwezesha kuanza haraka iwezekanavyo utekelezaji wa mradi huu,” amesema Nsekela.
Nsekela ameongeza kuwa mkopo huo unajumuisha Euro milioni 69.312 sawa na asilimia 85 utakaotolewa kwa ushirikiano wao na Benki ya Deutsche huku kiasi kilichobaki cha Euro milioni 10.65 sawa na asilimia 15 kitatolewa na Benki ya CRDB peke yake suala lililopata baraka zote za SMZ kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.

Nsekela pia amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha uchumi wa Zanzibar ikiwamo uuzaji na uorodheshaji wa Hatifungani ya Sukuk iliyotolewa na SMZ mapema mwaka huu na kukusanya shilini bilioni 381 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa kufuata misingi ya dini ya Kiislamu.
Benki ya CRDB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo visiwani Zanzibar ikishiriki kufanikisha miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 130. Kwa mkopo uliosainiwa, unaifanya Benki ya CRDB kufikisha jumla ya shilingi billion 375 ya uwezeshaji wa miradi inayosimamiwa na SMZ.





RAIS WA NAMIBIA ATEMBELEA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM,ALAKIWA NA MKUU WA CHUO DKT KIKWETE

May 21, 2025 Add Comment


Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Namibia Mhe. NetumboNandi-Ndaitwah alipowasili chuoni hapo leo asubuhi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kiserikali ya siku mbili nchini.

Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah amefurahi kualikwa kuzungumza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo na ameeleza kuwa atatumia fursa hiyo kuwahamasisha wanafunzi kushiriki katika fursa mbalimbali za kujenga nchi kizalendo na za uongozi.



PUBLIC ANNOUNCEMENT FROM EQUITY BANK TANZANIA

May 21, 2025 Add Comment

 

NCAA YANADI VIVUTIO VYA UTALII MAADHIMISHO YA SIKU YA NYUKI DUNIANI YALIYOFANYIKA DODOMA

May 20, 2025 Add Comment


Na Philomena Mbirika, Dodoma 


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imetumia fursa ya maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yanayofanyika jijini Dodoma kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii  vinavyopatikana katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. 


Maadhimisho hayo yaliyoanza Mei 17 na kuhitimishwa leo Mei 20, 2025 katika Viwanja vya Chinangali Park Dodoma Mgeni rasmi akiwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, yamewakutanisha wadau wa sekta ya nyuki kutoka Mikoa mbalimbali nchini kujadili maswala yanayohusu sekta ya ufugaji nyuki katika uhifadhi na kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.



Katika maadhimisho hayo NCAA imepata fursa ya kutangaza vivutio vyake vya utalii vikiwemo Bonde la kreta ya Ngorongoro lenye muonekano wa pekee, wanyama mbalimbali ikowemo wa wanyama wakubwa watano “The big Five “,  Laitoli zinakopatikana Nyayo za binadamu wa kale aliyeishi miaka milioni 3.7 iliyopita, Olduvai George eneo lenye gunduzi za kihistoria ya akiolojia, Kreta ya Empakai iliyopambwa na ndege aina ya Flamingo, Tambarare za Ndutu, Kreta ya Olmoti, Jabali la Nasera (Nasera Rock”, Pango la Olkarien, Mchanga unaohama na vivutio vingine.


Akizungumza ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye maadhimisho hayo Afisa wa Uhifadhi- Utalii Joseph Mzaga amesema kwamba maadhimisho haya yamewakutanisha na taasisi mbalimbali pamoja na watu binafsi ambao wameza kuwaeleza shughuli mbalimbali zinazofanywa na NCAA kwenye Utalii, Uhifadhi na maendeleo ya jamii. 


“Maadhimisho haya yametupa fursa ya pekee ya kutangaza vivutio vilivyopo ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa watu  mbalimbali zikiwemo taasisi, watu binafsi na makundi ya wanafunzi walioweza kukutembelea mahali hapa ambapo wameonesha shauku kubwa ya kwenda kutembelea vivutio hivi” Alisema Joseph 


Katika kuelekea Mkutano wa 50 wa Kimataifa wa Shirikisho la Umoja wa Vyama vya Wafugaji nyuki Duniani (Apimondia 2027) unaotarajiwa kufanyika Tanzania, NCAA imejipanga kuonesha utajiri wa rasilimali za asili, utalii wa kipekee na jitihada za uhifadhi  kupitia sekta ya nyuki na utalii.