UWEKEZAJI WA NSSF MKULAZI WAONGEZA AJIRA KWA WANANCHI NA UZALISHAJI WA SUKARI

May 14, 2025 Add Comment


*Bodi ya Wadhamini ya NSSF yaridhishwa na uwekezaji huo wa ubia na Jeshi la Magereza


Na MWANDISHI WETU,

Morogoro. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kudhihirisha mafanikio ya uwekezaji wake mkubwa katika sekta ya viwanda kupitia mradi wa kimkakati wa kiwanda cha sukari cha Mkulazi kilichoko mkoani Morogoro, ambacho kimeanza rasmi uzalisha Julai 2024, kimezalisha ajira kwa Watanzania na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara ya Bodi ya Wadhamini ya NSSF,  Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bi. Mwamini Malemi, alieleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa kwa ubia kati ya NSSF na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri, hongereni sana. Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini tumejionea na tunathamini mnachokifanya,” alisema Bi. Mwamini mara baada ya kupokea taarifa ya Kiwanda kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi (MHCL), Bw. Selestine Some.

Kwa upande wake, Bw. Masha Mshomba, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF alisema kupitia ziara hiyo ya kikazi, Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wameweza kushuhudia shughuli mbalimbali za uendeshaji wa mradi huo ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kupunguza nakisi ya sukari nchini.

Akisoma taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi Bw. Some alisema katika msimu wa mwaka 2024/25, kampuni ilipanga kuzalisha tani 20,000 za sukari ya majumbani, ambapo hadi mwisho wa msimu kiasi cha tani 19,124 sawa na asilimia 96 kilizalishwa.

Alisema pia, katika msimu wa 2025/26, Kampuni itaanza pia kuzalisha sukari ya viwandani ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa kiwanda,uliofanyika tarehe 8 Agosti 2024.

Bw. Some alisema uzalishaji wa sukari ya viwandani utapunguza uagizwaji wa bidhaa hiyo nje ya Nchi.  

Alisema pia katika msimu wa uzalishaji wa sukari 2024/25 kiwanda kimetoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 2,172 na zisizo za moja kwa moja 8,000, na kuongeza biashara, shughuli za kiuchumi na kipato kwa Wananchi wa Mji wa Dakawa, Dumila na vijiji jirani.

MWISHO

JK ASHIRIKI IBADA YA MAZISHI YA MAREHEMU CLEOPA DAVID MSUYA MWANGA

May 14, 2025 Add Comment

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa miongoni mwa maelfu ya waombolezaji katika ibada ya Mazishi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. David Cleopa Msuya, ibada iliyofanyika Kanisa la KKKT Usharika wa Usangi Kivindu Dayosisi ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro  jana Jumanne Mei 13,2025.


WAZIRI ULEGA AUNDA TIMU KUCHUNGUZA KIVUKO CHA MV TANGA

May 13, 2025 Add Comment

 



Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameunda timu ya wataalamu na kuipa siku saba kuchunguza changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika Kivuko cha MV TANGA kilichopo wilayani Pangani, mkoani Tanga baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu kusuasua kwa utendaji wake.

Pia, katika ziara yake mkoani Tanga, Ulega pia amemtaka mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga barabara ya Tanga - Pangani - Mkwaja - Bagamoyo (Makurunge) sehemu ya Tungamaa - Mkwaja – Mkange, kuilipa serikali fidia kutokana na uzembe uliofanya ujenzi usikamilike kwa wakati ilhali tayari serikali imetimiza upande wake wa mkataba ikiwamo kumlipa mkandarasi huyo.

Akizungumza kwa nyakati tofauti mkoani humo, Ulega alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya jitihada kubwa za ukarabati na ununuzi wa vivuko ili kurahisisha maisha ya wananchi na kwamba wananchi hawapaswi kupata shida wakati miundombinu ipo.

Kivuko aambacho kimeundiwa tume ni ya uchunguzi kinatoa huduma kati ya Pangani na Bweni na Ulega alisema lengo ni kuhakikisha kuwa kivuko hicho kinafanya kazi kwa wakati wote kama ilivyokusudiwa.

Naunda timu ya watu watatu, mmoja kutoka Ofisi ya Rais wa kutoka hapa na wawili Katibu Mkuu wa Ujenzi atawateua kutoka wizarani ili iniambie ni nini hasa kinaendelea hapa Pangani, haiwezi ikawa kila siku wananchi wanapata usumbufu”, amesisitiza Ulega.

Ulega amefanya maamuzi hayo kutokana na Kivuko hicho cha MV TANGA kushindwa kufanya kazi kwa siku nne huku watendaji na wasimamizi wakishindwa kufanya maamuzi ya haraka ya upatikanaji wa vipuri vya kufungwa katika kivuko hicho na kusisitiza kuwa endapo itabainika kuna hujuma zinafanyika katika kivuko hicho atachukua hatua za kinidhamu.

Akizungumza kabla ya Ulega, Mbunge wa Jimbo la Pangani ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alimuomba waziri huyo kushughulikia changamoto ya usafiri wa Kivuko cha MV TANGA ambacho ni muhimu na msaada kwa wananchi wa Pangani.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amekagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa.






DKT.BITEKO AWASILI NCHINI MOROCCO KWA ZIARA YA KIKAZI

May 13, 2025 Add Comment



📌Ushirikiano Tanzania, Morocco kuimarishwa


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewasili nchini Morocco kwa ziara ya kikazi inayolenga kukuza na kuimarisha mahusiano  kati ya nchi hizi mbili katika Sekta ya Nishati. 

Mara baada ya kuwasili,  Dkt. Biteko amepokelewa na Naibu Waziri wa Mageuzi ya Nishati na Maendeleo Endelevu nchini humo, Mhe. Mohamed Ouhmed, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na mwakilishi katika eneo la Morocco, Mhe. Ali Jabir Mwadini. 

Akiwa nchini humo, Dkt. Biteko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na mwenyeji wake Waziri wa Nishati na Maendeleo Endelevu wa Ufalme wa Morocco, Mhe. Leila Benali ambapo watajadili masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Nishati. 

Dkt. Biteko ameongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Dennis Londo, Wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa  nishati vijijini (REA), Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).


Mwisho.

MAWAZIRI WA SADC WAKUTANA KUJADILI USIMAMIZI WA MAAFA

May 13, 2025 Add Comment

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga, ameshiriki mkutano wa dharura wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Usimamizi wa Maafa kwa Nchi Wanachama wa SADC, uliofanyika leo tarehe 13 Mei 2025 kwa njia ya mtandao.

Mkutano huo wa dharura umelenga kujadili hatua za kuimarisha mfumo wa usimamizi wa maafa na huduma za kibinadamu kwa nchi wanachama wa SADC.

Pia Mkutano huo umelenga kujadili hatua za kuimarisha usimamizi wa maafa na kuunga mkono ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na maafa na kuendelea kujenga usalama wa watu na mali, Aidha Waziri wa Serikali za Mitaa na Kazi za Umma wa Zimbabwe, Bw. Daniel Garwe, ameongoza mkutano huo kama Mwenyekiti.

Pamoja na hayo Mhe. Ummy Nderiananga ameutumia mkutano huo kutoa pongezi kwa Sekretarieti ya SADC kwa kuanzisha kituo cha huduma za kibinadamu na operesheni za dharura kilichopo Msumbiji, akisisitiza umuhimu wa kituo hicho katika kuimarisha ushirikiano na kukabiliana na maafa. Pia, amekubaliana na ongezeko la wataalamu 35 katika timu ya SADC ya utayari wa kukabiliana na dharura. 

Mkutano huu umeonesha mshikamano wa kikanda katika kuimarisha usalama na kukuza uchumi wa nchi za SADC kupitia usimamizi bora wa maafa.