TUME YA KUREKEBISHA SHERIA YATOA ELIMU KWA WANANCHI MIKOA YA PWANI

April 25, 2025 Add Comment


Mwanasheria wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT), Vick Mbunde, akizungumza na Wanafunzi  wa Shule ya Sekondari ya Nyumbu wakati akitoa elimu ya sheria ya makosa ya kimtandao Kibaha Mkoa wa Pwani Aprili 24, 2025.

................................................... 

Na Mwandishi Wetu, Kibaha

TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT), imeto elimu kwa wananchi zaidi ya Milioni 2 katika mkoa wa Pwani, Lindi na Mtwara inayohusu Sheria ya makosa ya kimtandao, maadili na ulinzi wa mtoto dhidi ya makosa hayo.

Mwanasheria wa Tume hiyo, Vicky Mbunde, akizungumza kwa nyakati tofauti Kibaha mkoani Pwani Aprili 24, 2025 wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo cha Walimu cha A3, Uuguzi na Uandishi wa Habari pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyumbu aliwataka kuwa mabalozi na walinzi wa mtoto dhidi ya makosa ya kimtandao huku wakijiepusha kufanya makosa hayo.

Alisema makosa ya kimtandao yamekuwa yakitumika kwa kutumia vifaa vya kielektroniki kama kompyuta, simu janja na vishikwambi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Makosa hayo ni kurekodi picha mbaya za watoto kama za utupu, kufanyiwa vitendo vya ukatili, kudhalilishwa na vitendo vingine vinavyofanana na hivyo na kuzisambaza mtandaoni,” alisema Mbunde.

Mbunde alisema mwanafunzi yeyote atakapoona vitendo hivyo vikifanyika au anafanyiwa atoe taarifa kwa walimu, wazazi na polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema vitendo hivyo havikubaliki katika jamii na ndio maana zimetungwa sheria kali dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kutenda makosa hayo.

Wakili Baraka Chipamba kutoka tume hiyo alisema makosa yote hayo yakiwepo ya ubakaji, kutia mimba na utoaji wa mimba adhabu yake ni kifungo cha zaidi ya miaka mitano nafaini kuanzia shilingi milioni tano hadi milioni 20 au zote kwa pamoja.

Walimu wa shule hizo waliipongeza tume hiyo kwakutoa elimu hiyo na wakaomba iwe endelevu kwani itasaidia kuwaondolea watoto hao madhira ambayo yanaweza kuyapata kutokana na vitendo hivyo.

Tume hiyo inatoa elimu hiyo chini ya Kaulimbiu isemayo Mabadiliko ya Sheria ni fursa ya kujenga taifa lenye haki na usawa kwa wote

Kuhusu Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ni idara ya Serikali inayojitegemea chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Sura ya 171, na ilianza kazi rasmi tarehe 21 Oktoba, 1983.  Kwa mujibu wa sheria, Tume ina jukumu la kufanya mapitio ya sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ziandane na mazingira ya wakati uliopo kwa maendeleo endelevu.Mwanasheria Baraka Chipamba kutoka Tume hiyo, akitoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo cha Walimu cha A3, Uuguzi na Uandishi wa Habari.Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyumbu, Juma MMrope akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo.

Wanafunzi wa Chuo cha Walimu cha A3, Uuguzi na Uandishi wa Habari. wakipata elimu hiyo
Mwanasheria Vicky Mbunde, akisisitiza jambo wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa wa Chuo cha Walimu cha A3, Uuguzi na Uandishi wa Habari cha Kibaha mkoani Pwani.
Mwanasheria Baraka Chipamba kutoka Tume hiyo, akitoa elimu hiyo.
Wanafunzi wakiuliza maswali.
Picha ya pamoja 
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyumbu wakipata elimu hiyo. 

ONGEZEKO LA MAPATO NAMANGA LAMKOSHA DKT. BITEKO

April 24, 2025 Add Comment


📌Ailekeza TANESCO kufunga Kituo cha Kupoza Umeme Longido


📌Maelekezo ya Serikali yatekelezwa Longido


📌Amuagiza Makonda kusimamia ufungaji vifaa vya maabara Sekondari ya Longido Samia


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza kufurahishwa kwake na ongezeko la ukusanyaji wa mapato katika kituo cha huduma za pamoja mpakani mwa Tanzania na Kenya cha Namanga.

Akizungumza Aprili 24, 2025 Namanga mkoani Arusha wakati katika ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano Dkt. Biteko ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania Kituo cha Namanga kwa kufanya kazi kwa ufanisi.

“ Nimefurahishwa sana na urahisi wa biashara na kila eneo limekuwa na ukuaji wa watu na bidhaa kwenye kusafirisha nje ya nchi ili kuleta fedha ya kigeni zitakazowezesha kufanya shughuli zingine nawapongeza sana, nawashukuru kwa kuwa na malengo makubwa ya kukusanya shilingi bilioni 124 na hadi kufikia leo mmekusanya shilingi bilioni 101 huku mkiwa na miezi kadhaa ya kuendelea kukusanya mapato” amesema Dkt. Biteko.

Amewataka watendaji hao kuendelea kuwa na utaratibu mzuri wa kurahisisha biashara kwa kuondosha mizigo inayosafirishwa kwa kutumia muda wa dakika 30 hadi 40 badala ya saa 2 kama ilivyokuwa hapo awali.


Ameendelea kusema kuwa Kituo hicho cha Namanga kilichofunguliwa mwaka 2018 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dkt. John Pombe Magufuli na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta kwa lengo la kurahisisha biashara kati ya nchi hizo mbili. Hivyo, watendaji hao waendelee kuwa mabalozi wazuri kwa kutangaza taswira njema ya Tanzania wakati wakitekeleza majukumu yao.

Awali akikagua Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Longido  Samia, Dkt. Biteko amesema kuwa baada ya siku kadhaa Kampuni ya Taifa Gesi itafunga miundo mbinu ya mfumo wa gesi shuleni ikiwa ni sehemu ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Pia, Dkt. Biteko amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda kuhakikisha Shule hiyo inapata vifaa vya maabara ili wanafunzi waweze kujifunza kwa vitendo na si nadharia pekee.


“ Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya hakikisheni hizi maabara zinafanya kazi kwa kupata vifaa, tabia ya wanafunzi kuchora bunsen bunner badala ya kuziiona na kuzitumia kwa kujifunzia kwa vitendo iishe, ” amesema Dkt. Biteko.

Amebainisha kuwa amemuelekeza Mkuu huyo wa Mkoa kuangalia namna ya kuweka uzio na kupata gari kwa ajili ya shule hiyo, huku akiwataka wanafunzi kujifunza kwa bidii ili watimize ndoto zao  na kuwa Shule hiyo ni kielelezo cha Mkoa wa Arusha.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mundarara, Dkt. Biteko amesema madini ni kichocheo kikubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kuwa Kijiji cha Mundarara kimekuwa na uzalishaji wa madini ya rubi na kuwa anafurahishwa kwa kuona sasa Watanzania wanaweza kufanya kazi za uchimbaji wa madini.

Kuhusu umeme, Dkt. Biteko amesema “Vijiji vyote 52 vina umeme, kuna vitongoji 176 na vitongoji vyenye umeme ni 112 pekee. Kuna maeneo ambayo yanahitaji nguzo 25 na nimemuelekeza Meneja wa TANESCO ndani ya wiki tatu nguzo ziwekwe na watu wapate umeme. Nimemuelekeza pia Meneja na bosi wake transforma ije hapa wiki ijayo ifungwe na watu wapate umeme,” amesema Dkt. Biteko.


Vilevile, Dkt. Biteko ameelekeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kujenga njia nne za kupeleka umeme Loliondo, Namanga, Mundarara na Kamwanga na baadae kujenga kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme ili kusaidia wananchi kupata umeme na kufanya shughuli zao za kiuchumi.


Pamoja na hayo, amesema kuwa Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuwaletea Watanzania maendeleo na kuwaasa wamuunge mkono. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu kwa kuchagua viongozi watakao waletea maendeleo.


Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amebainisha kuwa katika kusheherekea miaka 61 ya Muungano ni vyema kila Mtanzania ajiulize kwa nafasi yake, amefanya nini yeye binafsi, lakini pia amefanya kitu gani hasa cha kukumbukwa kwa watu wake wa karibu, kwa jamii inayomzunguka na pia kwa Taifa.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Madini na Mbunge wa Longido, Mhe.  Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kusaidia miradi ya maendeleo ambapo wachimbaji wadogo wilayani humo sasa  wana umeme wa uhakika.


Ameendelea kusema Wilaya hiyo imenufaika na miradi ya maendeleo ambapo usanifu wa barabara ya kutoka Siha hadi Longido unaendelea.


“ Mgodi wa magadi soda wa  Engaruka umetengewa fedha na tayari watu wako tayari kuja kuwekeza na itasaidia kujenga mji wa kisasa, tuna zaidi ya tani milioni 768 ambayo tunaweza kuchimba kwa muda mrefu bila kuisha. Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia wachimbaji wadogo wameweza kupata kiasi cha shilingi bilioni 9.999 ambapo Serikali inapata mapato, ”amesema Dkt. Kiruswa.


Amesisitiza “ Wilaya hii tumepewa fedha ya kujenga shule za  sekondari sita katika kata zetu na tumebakiza kata tatu ambazo hazina shule za sekondari, kazi ya kujenga shule katika kata hizo inaendelea. Mafanikio haya yasingeweza bila kuwa na ushirikiano na mshikamano kati aya Chama Cha Mapinduzi, Serikali na viongozi wa kimila.”


Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema kuwa maelekezo ya Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa kuhusu ujenzi wa daraja, upatikanaji wa haki na kituo cha afya yamefanyiwa kazi. 


“ Tayari fedha zaidi ya shilingi milioni 250 imetolewa na baada ya wiki moja itaonekana kwenye mfumo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya. Kuhusu barabara, katika bajeti hii imetengwa fedha shilingi milioni 270, fedha hizi ni kwa ajili ya barabara ya Resingita yenye urefu wa km 13 na barabara ya Longido kwenda Meloe imetengewa shilingi milioni 105,”amesema Mhe. Makonda.


MWISHO

HakiElimu na ALI For Impact Waibuka na Mpango Kuibua Viongozi Chipukizi Mashuleni

April 24, 2025 Add Comment
Katika kuhakikisha taifa linapata viongozi bora wa kesho, taasisi zisizo za kiserikali za HakiElimu na The African Leadership Initiative For Impact (ALI For Impact) zimezindua programu maalum ya kuwawezesha vijana walioko mashuleni kupata maarifa na ujuzi wa uongozi.

BALOZI NCHIMBI KWA NYERERE,AKABIDHIWA 'KIFIMBO' KWA KUKUBALIKA

April 24, 2025 Add Comment


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ametembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kijijini Mwitongo na kukabidhiwa fimbo maalum na familia hiyo ya mwasisi wa Tanzania na CCM. 

Balozi Nchimbi ambaye yuko ziara ya kikazi ya siku tano katika Mkoa wa Mara, mbali ya kukabidhiwa zawadi hiyo, yeye pamoja na msafara wake, pia alipata fursa ya kuweka shada la maua na kufanya misa fupi kwenye kaburi alipozikwa Mwalimu Nyerere. 


Kiongozi wa Kabila la Wazanaki, Chifu Joseph Wanzagi, alimwambia Balozi Nchimbi kuwa hicho ni kifaa cha kazi atakachotumia katika dhamana alizoaminiwa kutumikia Watanzania. Alisisitiza kuwa huwa wanafanya hivyo kwa kiongozi mwenye sifa zinazofaa.

“Tunakukabidhi fimbo hii. Huwa tunakabidhi kwa kiongozi tunayemkubali. Kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi utaitumia kuchapa na kuwarekebisha wale wote ambao wanataka kutatiza shughuli za uchaguzi kinyume na utaratibu wa Kikatiba,” alisema Chifu Wanzagi. 

Balozi Nchimbi ambaye aliambatana na mwenza wake, Mama Jane Nchimbi, pamoja na viongozi wa Chama na Serikali Mkoa wa Mara na Wilaya ya Butiama, pia alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Familia ya Mwalimu Nyerere, nyumbani hapo.



NAIBU WAZIRI MKUU AWASILISHA LONGIDO

April 24, 2025 Add Comment


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akipokewa na Kiongozi wa wanafunzi kidato cha kwanza (1), Lucy Lengishoni mara baada ya kuwasili katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Longido Samia.

Ziara hiyo ni sehemu ya shamrashamra za kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanzania Aprili 24, 2025 Mkoani Arusha. @biteko @onwm_tanzania