MILIONI MBILI ZA MBUNGE UMMY MWALIMU ZILIVYOCHOCHEA USHINDI WA COASTAL UNION
michezoNa: Mwandishi Wetu, Tanga
Ahadi ya Milioni Mbili iliyoahidiwa na Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini (CCM), Ummy Mwalimu, kwa Timu ya Coastal Union endapo itapata ushindi katika mchezo wao dhidi ya Singida Black Stars, imekuwa chachu ya kuchochea ushindi mara baaada ya kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja (2-1) katika mechi iliyochezwa Aprili 10, 2025, katika viwanja ya CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Ummy Mwalimu ambaye ni mdau mkubwa wa michezo mkoani Tanga, alipata wasaa wa kuongea na wachezaji wa Timu ya Coastal Union kabla ya mchezo huo.
Kimsingi, Ummy Mwalimu aliwasisitiza wachezaji hao kupambana kwa jasho na damu ili kupata ushindi huku akisisitiza kuwa atawakabidhi kitita cha Milioni Mbili mara baada ya kumalizika mchezo huo endapo wataibuka na alama tatu muhimu katika mchezo huo.
Kufuatia ushindi wa (2-1), Ummy Mwalimu alitimiza ahadi yake hiyo kwa kuwakabidhi wachezaji hao fedha taslimu Milioni Mbili, ambapo viongozi na wachezaji wa Coastal Union walimshukuru kwa kutimiza ahadi yake ambayo imewapa nguvu ya kupambana katika mchezo huo katika michezo inayofuata pia.
Hii si mara ya kwanza kwa Ummy Mwalimu kuwaunga mkono Timu ya Coastal Union, amekuwa akifanya hivyo mara kadhaa kuhakikisha Timu hiyo inafanya vizuri ili kuuheshimisha mkoa wa Tanga kimichezo hasa katika mchezo wa mpira wa miguu.
TETE FOUNDATION YAGAWA MAHITAJI /VIFAA VYA SHULE KWA WANAFUNZI WALIOPO KATA YA MIONO,CHALINZE -PWANI KWA MWAKA 2025
michezoTETE FOUNDATION kupitia mradi wake wa “TUNAAMINI KATIKA WEWE” wamekuwa wakigawa mahitaji/vifaa vya shule kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na wenye uhitaji maalumu kwa kuhakikisha mtoto hakosi shule mwaka mzima kwa sababu ya kutokuwa na mahitaji ya shule (Sare za shule, madaftari, Begi, viatu n.k)......

Mradi huu wa “Tunaamini katika wewe” unao dhaminiwa na Kampuni ya Reliance Insurance kwa takribani miaka mitatu sasa, umeongeza ufaulu wa watoto mashule na kupunguza utoro mashuleni
Zoezi hili la ugawaji wa mahitaji ya shule ulienda sambamba na Bonanza la Michezo lililojumuisha shule za msingi na Sekondari zilizopo katika kata ya Miono lililokuwa na dhumuni la kuwaleta watoto pamoja ili kuweza kutambuana na kushirikiana kwenye masomo ili kukuza ufaulu mashuleni
Imetolewa
Afisa Habari
WATANZANIA KUNUFAIKA NA MASHINDANO YA CHAN 2025,AFCON 2027
michezo*📌 Mashindano yameipa heshima Tanzania kimataifa*
*📌 Rais Samia kinara wa Michezo nchini*
*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*
Watanzania watanufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii zitakazopatikana kuelekea katika mashindano wa CHAN 2025 na AFCON 2027.
Hayo yamebainishwa leo Januari 15, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Michezo kuelekea CHAN 2025 na AFCON 2027 jijini Dar es Salaam.
"Nchi yetu imepata heshima kubwa kimataifa na hii haiji kwa bahati mbaya imesababishwa na ukuaji wa demokrasia iliyojengwa na Rais Samia kwenye mataifa mbalimbali duniani," amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amewapongeza wadau wa michezo waliotoa mawazo ya kuanzishwa kwa kongamano hilo ili kutangaziana fursa zitakazotokea wakati wa mashindano hayo.
Ameeleza kuwa, mashindano yatawakutanisha wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali na kuna wajibu wa kufanya maandalizi kwa ufanisi mkubwa ili kunufaika na mashindano kupitia fursa mbalimbali za usafirishaji, malazi na burudani.
"Fursa za mashindano haya zitakuza uchumi wa nchi yetu na kufanya vikundi vya watu au kampuni mbalimbali kufanya biashara na kukuza uchumi wao na hatimaye kuondoa umaskini miongoni mwetu," ameongeza Dkt. Biteko.
Vile vile, Dkt. Biteko amempongeza Rais Samia kwa kuwa kinara wa kuhamasisha ushiriki wa watanzania katika sekta ya michezo ili vijana kukuza uchumi wao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwijuma amesema lengo la kongamano ni kupokea maoni ya wadau mbalimbali na kuchanganua fursa zitakazokuja pamoja kuelekea mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027 ambazo watanzania watanufaika nazo.
Mashindano ya CHAN 2025 yanatarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu na AFCON yamepangwa kufanyika mwaka 2027.
UDSM MARATHON KUBORESHA MAISHA YA WANAFUNZI
michezo📌 Dkt. Biteko Ahimiza Wadau Kuchangia Ujenzi wa Kituo cha Wanafunzi
📌Awashukuru Wadhamini wa UDSM Marathon
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza amefurahishwa kwake na uendeshaji wa UDSM Marathon na kusema kuwa inasaidia kufanikisha malengo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuendelea kutoa elimu bora na kuboresha mazingira ya wanafunzi.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Desemba 7, 2024 mara baada ya kushiriki mbio hizo za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM MARATHON) zilizofanyika chuoni hapo.
“ Ni dhahiri kwamba mbio hizi zimekuwa muhimu kwa Chuo hiki na jamii kwa ujumla. Tukio hili limeleta pamoja wadau mbalimbali na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Natambua kwa misimu mitano mbio hizi zimekua zikichangia katika ujenzi wa Kituo cha Wanafunzi kinachojengwa hapa katika Kampasi Kuu ya Mwalimu Nyerere Mlimani. Ujenzi wa kituo hiki ulianza kwa michango kutoka kwa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na washirika mbalimbali wa maendeleo ya elimu ambapo jumla ya shilingi bilioni 4.4 zimechangwa kutoka kwa wadau.”
Aidha, awamu ya kwanza ya ujenzi imekamilishwa kwa kutumia fedha za ndani na hivyo kazi kubwa iliyobaki ni kukamilisha awamu ya pili ili kutimiza ndoto ya kuwa na Kituo cha Wanafunzi kitakachowezesha wanachuo kuwa na maeneo ya kujifunzia na kupata nafasi ya kukuza vipaji vyao.
Ujenzi wa awamu ya pili unahitaji shilingi bilioni 3.3 na hivyo kufanya gharama za ujenzi kwa awamu hiyo kufikia shilingi bilioni 9.4 badala ya shilingi bilioni 6 zilizokadiriwa awali ambazo zimebadilika kwa sababu mbalimbali.
Akiwahakikishia ushiriki wake katika kufanikisha ukamilishaji wa ujenzi wa Kituo Dkt. Biteko amesema “Nataka niwatoe wasiwasi kuwa jambo hili ni letu sote kwa kuwa majengo haya yatatumika kwetu sote. Nalibeba suala hili kwa uzito wake ili kilichoahidiwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi kipatikane kwa wakati,”
Pia, ametoa wito kwa wadau mbalimbali
kuunga mkono jitihada za kuwezesha mbio hizo kufanyika kwa ustadi mkubwa na kwa kuwa zimeonesha kupitia mshikamano, wanaweza kufanikisha malengo makubwa ya kijamii na kielimu. Sambamba na kuhimiza uongozi wa Chuo kuandaa namna ya kukutanisha wadau zaidi ili kuchangia fedha za kukamilisha ujenzi wa kituo.
Vilevile, Dkt. Biteko amempongeza Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa usimamizi wake katika shughuli za maendeleo ya Chuo hicho.
Kwa upenda wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Chuo hicho kinathamini mchango wa Serikali katika ujenzi wa Kituo hicho cha wanafunzi.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam (Utawala na Fedha), Prof. Bernadeta Kilian amesema Chuo hicho kilianzisha ujenzi wa kituo cha wanafunzi kwa ajili ya kupumzika na kukuza uwezo wa kubuni au kupata mawazo Mapya.