Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

AFRIKA IPEWE UHURU WA KUZALISHA NISHATI KWA KUTUMIA RASILIMALI ZAKE -DKT .BITEKO

June 19, 2025 Add Comment
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko(wa pili kushoto) akishiriki kwenye mdahalo wa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg 2025 (SPIEF'25) lililofanyika leo 19 Juni, 2025 katika kituo cha Mikutano na Maonesho ExpoForum katika jiji la St. Petersburg nchini Urusi. 


📌 Ahimiza Tanzania na Urusi kuendeleza uhusiano wake wa kuheshimiana


📌 Tanzania kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme wastani wa  megawati 120


📌  Tanzania yapongezwa kwa mafanikio yake sekta ya nishati


📌  Ahimiza mfumo sawa wa uzalishaji nishati kati ya nchi tajiri na masikini 


📌  Kampuni za Urusi zaombwa kuwekeza zaidi Afrika 


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa nchi za Afrika kupewa uhuru wa kuzalisha nishati kwa kutumia raslimali zilizopo barani humo.


Dkt. Biteko ametoa wito huo Juni 19, 2025 wakati akizungumza katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg linalofanyika nchini Urusi.


Amesema Afrika inahitaji programu itakayosaidia kufikia dhamira yake ya kuondoa idadi kubwa ya watu ambao hawatumii nishati safi huku akitaja baadhi ya athari za matumizi ya nishati isiyo safi ikiwemo uharibifu wa mazingira.


Ameongeza kuwa Afrika ina vyanzo  vingi vya kuzalisha nishati, mfano Tanzania kuna vyanzo kama vile jua, maji na gesi asilia. Hata hivyo barani humo hakuna uhuru wa kutumia makaa ya mawe licha ya kuwepo kwa kiwango kikubwa pamoja na kuwa nchi kubwa duniani zinaweza kufanya hivyo.

Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti Mtendaji wa Baraza la Nishati Afrika, NJ Ayuk. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Alexander Pankin. Waziri wa Nishati Urusi Mhe. Sergey Tsivilyov na kushoto ni msimamizi wa mdahalo Alexey Bobrovsky na kushoto ni msimamizi wa mdahalo Alexey Bobrovsky. (Picha na ONWM & WN)

“ Hivyo iangaliwe namna kwa kila nchi kutumia raslimali zake ili kuzalisha nishati, mfumo uliopo unazifanya nchi zote kuwa sawa lakini ukweli ni kwamba hatuko sawa. Kwa mfano Afrika inachangia asilimia 3 hadi 4 pekee ya uchafuzi wa mazingira, lakini imepewa mzigo mkubwa zaidi.” Amesema Dkt. Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza kwenye mdahalo wa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg 2025 (SPIEF'25) lililofanyika leo 19 Juni, 2025 katika kituo cha Mikutano na Maonesho ExpoForum uliopo katika jiji la St. Petersburg nchini Urusi. (Picha na ONWM & WN)


Amesisitiza” Kila nchi itumie utaratibu wake wa kuzalisha nishati lakini kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa mazingira.”


Amezungumzia uhusiano  mzuri uliopo wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Urusi na kusema kuwa uendelee kuwa wa kuheshimiana na kukubaliana.

Ambapo ametaja manufaa yake kuwa ni  pamoja na kubadilishana ujuzi na kuisaidia Tanzania katika mitaji ya  miradi nishati.


Amebainisha kuwa Tanzania ina mpango wa kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya kuzalisha takribani megawati 120 za umeme.


Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Urusi, Mhe. Sergey Tsivilev amesema kuwa Rais wa nchi hiyo Mhe. Vladimir Putin amekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha zinaungana na nchi zingine katika kupatia ufumbuzi  changamoto za masuala ya nishati.

Naye, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya African Energy Chamber, Bw. NJ Ayuk amesema kuwa ni muhimu kwa nchi za Afrika na Urusi kuungana na kuhakikisha sauti ya Afrika inasikika na kutekeleza wanayokubaliana ili wote waweze kunufaika na uhusiano kati yao.


Aidha, ameiomba Serikali ya Urusi kuwezesha kampuni kutoka nchini humo ili ziweze kuwekeza zaidi Afrika hususan katika sekta ya nishati.


Pia, ameipongeza Tanzania katika hatua iliyopiga na mafanikio yake katika sekta ya nishati  sambamba na kutoa wito kwa nchi za Afrika kujifunza zaidi kutokana na mafanikio yaliyopo nchini Urusi.


Jukwaa hilo la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg linatarajiwa kuwa na washiriki kutoka takribani nchi 140.


Mwisho.

WADAU WA CHANJO ZA MIFUGO AFRIKA WATEMBELEA KIWANDA CHA HESTER BIOSCIENCES TANZANIA

June 19, 2025 Add Comment
Na Daudi Nyingo

Kiwanda cha Hester Biosciences Africa Limited kilichopo katika Eneo la Viwanda la TAMCO, Kibaha – Mkoa wa Pwani, kimepokea ugeni wa wasajili wa chanjo na wakurugenzi wa uzalishaji wa chanjo za mifugo kutoka nchi 25 za Afrika terehe 18 Juni 2025. 

TADB na TWCC Waingia Mkataba Kuinua Wanawake na Vijana Kwenye Kilimo

June 18, 2025 Add Comment
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeingia makubaliano na Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) kwa lengo la kuwawezesha wanawake na vijana wajasiriamali wanaoshiriki katika minyororo ya thamani ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.

JUKWAA LA NNE LA UTEKELEZAJI WA USHIRIKISHWAJI WA WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI LILETE MABADILIKO -OLLAL

June 18, 2025 Add Comment


MWANZA


Wadau wa madini nchini wametakiwa kutumia Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta la Madini kama kichocheo cha mabadiliko katika Sekta ya Madini hasa kwenye eneo la ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini  katika eneo la ajira na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini kama vile  usambazaji wa vifaa na  vyakula.

Hayo yamesemwa jijini Mwanza leo Juni 18, 2025 na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini, Augustine Ollal kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo wakati akifunga Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta la Madini.


Jukwaa hilo lililoanza mapema Juni 16, 2025 limekutanisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na  Wizara ya Madini na Taasisi zake, Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Taasisi za Fedha, Kampuni za Uchimbaji wa Madini na Watoa Huduma kwenye Migodi ya Madini.


Amesema kufanyika kwa jukwaa hilo ni mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Madini kuhamasisha ushiriki wa watanzania katika shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini na usambazaji wa bidhaa na huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ili wananchi waendelee kunufaika na rasilimali madini na kukuza uchumi wa nchi.

Katika hatua nyingine, amezitaka kampuni za madini kuendelea kutoa kipaumbele kwa watanzania kwenye  ajira na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.

Wakati huo huo amempongeza Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde kwa kutafsiri maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hali iliyopelekea mchango wake katika Pato la Taifa kufikia asilimia 10.1.

 Jukwaa hilo lenye kaulimbiu inayosema Ongezeko la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ni chachu ya Ukuaji wa Uchumi limeambatana na maonesho yenye lengo la kuelimisha kuhusu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini.



WAENDELEZAJI WA MRADI WA KUZALISHA UMEME WA LUPALI MKOANI NJOMBE WAELEKEZWA KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA WA MRADI

June 18, 2025 Add Comment
-Waishukuru REA kwa uwezeshaji wa zaidi ya shilingi bilioni 4.3

-Utekelezwaji wake wafikia 97.5%

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu ameelekeza waendelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa kilowati 317 kwa kutumia maporomoko ya Mto Lupali kuimarisha ulinzi na usalama wa mradi ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Ameelekeza hayo Juni 18, 2025 katika Kata ya Matola Wilaya ya Njombe Mkoani Njombe alipofanya ziara iliyolenga kujionea maendeleo ya utekelezaji wa Mradi huo unaosimamiwa na Watawa wa Kanisa Katoliki wa Shirika la Wabenediktini, Imiliwaha Njombe kwa ufadhili wa REA.

"Mradi huu hadi kufikia hatua hii umetumia gharama kubwa, na ni mradi utakaokuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa maeneo haya na Taifa kwa ujumla, tuna kila sababu ya kuhakikisha unalindwa," alielekeza Balozi Kingu.

Alielekeza kujengwa kwa uzio utakaozunguka bwawa la kuzalishia umeme sambamba na kusimika mifumo ya taa na kamera maalum za ulinzi maarufu kama CCTV Camera maeneo yote muhimu ya mradi.

Sambamba na hilo, Balozi Kingu aliwapongeza kwa hatua waliyofikia na aliwaelekeza waendelezaji wa mradi huo kushirikiana kwa karibu na waendelezaji wa miradi mingine ili kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa miradi.

"Hapa mmezungukwa na waendelezaji wa miradi ya namna hii wenye uzoefu, ni vyema mkajenga utaratibu wa kuwa mnabadilishana uzoefu ili kuimarisha uendeshaji wa mradi," alisisitiza Balozi Kingu.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mratibu wa Mradi, Sista Imakulata Mlowe alitoa shukrani kwa uwezeshwaji unaofanywa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na aliahidi kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Balozi Kingu.

"Tangu kuanza kwa mradi mwaka 2011, REA imetuwezesha sehemu kubwa katika hatua zote; tunaahidi kutimiza maelekezo yote yaliyotolewa," alisema Sista Mlowe.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage alisema hadi sasa REA imewezesha zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi.

"REA imetoa ruzuku kwa awamu tofauti kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo wakiwemo benki ya Dunia na Serikali ya Sweden ili kuwezesha mradi huu tangu hatua za mwanzo za utafiti wa awali, ujenzi wa njia kuu za kusafirisha na kusambaza umeme kwa watumiaji takriban 600.

Mhandisi Advera alibainisha maeneo mengine yaliyowezeshwa na REA kuwa ni pamoja na ruzuku iliyotolewa kukamilisha mradi ikihusisha ujenzi wa sehemu ya kupokelea maji, nyumba ya mtambo, uwekaji wa mabomba pamoja na shughuli nyingine za Mradi.

Alisema kukamilika kwa mradi kutazalisha kiasi cha kilowati 317 ambazo kiasi zitatumiwa na mwendelezaji na kiasi kitakachobaki zitaingizwa katika Gridi ya Taifa.

Alisema kuwa REA imeendelea kufadhili miradi ambayo itaongeza wigo wa Gridi ya Taifa ili kukuza uchumi wa Taifa kwa kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi.

"REA imefadhili miradi ya uzalishaji na usambazaji nishati vijijini inayotekelezwa na taasisi mbalimbali za Serikali na Sekta Binafsi kwa kutoa ruzuku pamoja na kuwezesha mikopo ya masharti nafuu sambamba na kuwajengea uwezo waendelezaji wa miradi," alisisitiza Mha. Mwijage.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu yupo Mkoani Njombe kwa ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya uzalishaji na usambazaji wa umeme inayowezeshwa na REA.