BIASHARA YA MAZAO YA MISITU NA NYUKI YAPAA – MAUZO NJE YA NCHI YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 333%
habari
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Kutoka kushoto ni Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, akiwa na makamishna wengine wa uhifadhi wafuatilia kwa makini hoja mbalimbali, ikiwemo mafanikio makubwa ya TFS katika usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki Mei 19,2025—ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga uchumi shirikishi wa kijani.
Akizungumza leo Mei 19, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alisema kuwa ndani ya miaka mitano, sekta hizo mbili zimeonyesha ushahidi wa wazi wa kuimarika kwa msingi wa uchumi wa kijani nchini.
Aliongeza kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2024/2025, uzalishaji wa mbao kutoka mashamba ya miti ya Serikali unaolimwa kibiashara umeongezeka kutoka mita za ujazo 1,108,791 hadi 1,264,535, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya 155,000 m³.
Aidha, viwanda vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya misitu vimeongezeka kutoka 636 mwaka 2020 hadi 1,671 mwaka 2025, huku viwanda vidogo vidogo kama vya useremala vikifikia zaidi ya 7,000 kote nchini.
Waziri Chana alisema kuwa thamani ya mauzo ya mazao ya misitu nje ya nchi nayo imepanda kwa kasi, kufikia Shilingi 458.47 bilioni mwaka 2024/2025, kutoka Shilingi 105.68 bilioni mwaka 2020/2021. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 333.8, jambo alilolieleza kuwa ni matokeo ya kuimarika kwa viwango vya usimamizi na ubora wa bidhaa zinazozalishwa.
Katika upande wa nyuki, Serikali imewezesha ujenzi wa viwanda nane (8) vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya nyuki, kutoka kiwanda kimoja (1) mwaka 2020. Viwanda hivyo vimejengwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Singida, Iringa, Katavi na Geita.
Mpaka kufikia Aprili 2025, Tanzania imeuza nje ya nchi jumla ya tani 1,321.35 za asali zenye thamani ya Shilingi 15.86 bilioni, ikilinganishwa na tani 430.61 za mwaka 2020/2021 zenye thamani ya Shilingi 5.17 bilioni — ikiwa ni ongezeko la asilimia 206.9.
Kutokana na mafanikio haya, Shirika la Wafugaji Nyuki Duniani limeiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Dunia wa Wafugaji Nyuki (APIMONDIA) utakaofanyika mwaka 2027 na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 4,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
“Kuongezeka kwa uzalishaji na thamani ya mauzo ya mazao ya misitu na nyuki ni ushahidi wa mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Tunajenga msingi wa uchumi wa kijani unaozingatia uhifadhi, maendeleo ya viwanda na ajira kwa vijana wetu,” alisisitiza Waziri Chana.
Katika hatua nyingine, Waziri Chana amewakaribisha wabunge wote na wadau wengine wa sekta ya maliasili kushiriki maonesho ya Siku ya Nyuki Duniani ambayo yanaendelea jijini Dodoma, na kufikia kilele chake kesho Mei 20, 2025 katika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.
--
Tulizo Henry Kilaga I A Brand Communication Strategist,
Located: Dodoma I Dar es Salaam - Tanzania.
Call/WhatsApp: +255 765 888887
RC DKT BATILDA AFUNGUA MAADHIMISHO YA NNE YA SIKU YA KIMATAIFA YA WANAWAKE KATIKA SEKTA YA BAHARI ATOA NENO
habariNa Oscar Assenga,Tanga
kuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian amesema maendeleo ya Taifa hayawezi kupimwa kwa kiwango cha uwekezaji au ujenzi wa viwanda pekee, bali kwa namna serikali na jamii zinavyoweka fursa za usawa wa kijinsia katika ajira, hususan kwa watoto wa kike na wa kiume.
Dk Burian ameyasema hayo alipokuwa akifungua maadhimisho ya nne ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake katika Sekta ya Bahari yaliyofanyika jijini Tanga (Jumapili) Mei 18/2025.
Akimnukuu mwanafalsafa maarufu Plato, aliyewahi kusema kuwa "Kilimo cha jamii yoyote ni jinsi inavyowathamini wanawake", Dk Burian alisisitiza kuwa taifa linapaswa kujipangia malengo ya kuhakikisha usawa wa kijinsia unatekelezwa kikamilifu.
"Tusiache mwanamke abaki ufukweni bali tunataka aingie ndani ya bahari," alisema kwa msisitizo..
Alieleza kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali, sekta ya bahari bado inatawaliwa na wanaume, huku takwimu zikionyesha kuwa wanawake wanaofanya kazi katika sekta hiyo ni asilimia 1.2 pekee.
Katika hatua ya kutia moyo, Dk Burian alipongeza Umoja wa Wanawake Wanaofanya Kazi katika Sekta ya Bahari katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) kwa kuanzisha programu ya 'Wakamate Wangali Wadogo' (Catch them Young) inayolenga kuelimisha na kuwahamasisha wanafunzi wa kike kujiunga na fani zinazohusiana na bahari.
Alisisitiza kuwa wanawake ndio uti wa mgongo wa sekta hiyo, akibainisha kuwa juhudi kama hizo zinaunga mkono maono ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwenye elimu ya sayansi kwa watoto wa kike, ikiwemo kuanzishwa kwa shule maalum."
Hapa Tanga, kupitia uwekezaji wa Rais, tumeanzisha shule maalum ya watoto wa kike wilayani Kilindi ambayo imepewa jina la aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Beatrice Shelukindo," alisema.
Dk Burian pia alitoa wito kwa sekta binafsi inayohusika na bahari kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa katika ajira.
"Nifahari yetu Kuwaona Wanawake wa Kitanzania wakiongoza na kushiriki miradi mkubwa ya maendeleo ya bandarini,fukwe zetu wakifundisha kwenye vyuo vya Bahari kama Chuo Cha Bahari Dar es salaam(Dar es salaam Maritime INstute-DMI)kufanya kazi kwenye Meli za kitaifa na Kimataifa Kwa hakika Hawa ni vinara na fahari yetu ni lazima tuwapongeze"alisema Burian.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WOMESA, Bi Fortunata Kikwaya, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kwa uwekezaji mkubwa walioufanya katika sekta ya bahari."
Sherehe hizi za nne zinaashiria maono yetu kuwa wanawake si wa kushirikishwa tu, bali ni wadau wakuu katika maendeleo ya sekta hii," alisema.
Bi Kikwaya alitaja mafanikio ya WOMESA kuwa ni pamoja na ongezeko la wanachama kutoka 24 mwaka 2021 hadi kufikia 174 mwaka huu, pamoja na kudhamini mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wanawake.
Kuhusu mpango wa 'Catch them Young', alisema tayari wametembelea shule 35 na kuanzisha vilabu tisa vya wanafunzi, vitatu kati yake vikiwa jijini Tanga.
Hata hivyo, alieleza kuwepo kwa mwamko mdogo wa wanawake kujiunga na WOMESA pamoja na uelewa mdogo kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya bahari.
Aliiomba Serikali kuanzisha utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike wanaotaka kusomea taaluma zinazohusiana na sekta ya bahari na kusaidia kuendeleza juhudi za kuwahamasisha kuingia katika sekta hiyo.
![]() |
Mwisho