Showing posts with label afya. Show all posts
Showing posts with label afya. Show all posts

DKT HUSSEIN :ACHENI KUTUMIA MITISHAMBA KUTIBU MACHO

February 02, 2024 Add Comment

 


Daktari Bingwa wa Macho katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo Dkt Hussein Abbas Tayebji amewataka wananchi wanaotumia njia ya kienyeji kutibu macho ikiwemo kutumia mkojo na maji ya chumvi kuweka kwenye macho kama tiba kuacha kufanya hivyo kwani wanaweza kupata madhara makubwa zaidi.

Kauli ya Daktari hiyo imekuja siku chache baada ya kuwepo kwa wimbi la Ugonjwa wa Macho maarufu kama Red Eyes likiendelea kuwatesa watanzania katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Dkt Hussein ambaye pia ni Mratibu wa Macho Mkoa wa Tanga aliyasema hayo leo wakati akizungumzia kuhusu ugonjwa huo kwa mkoa ambapo alisema mpaka sasa zaidi ya wagonjwa 90 wameugua huku asilimia kubwa wakitokea kwenye Jiji la Tanga

Alisema kwamba badala yake wananchi wanapougua ugonjwa huo wafike kwenye Vituo vya Afya au Hospitali kwa ajili ya kuwaona madaktari ili kuweza kupatiwa matibabu ikiwemo kupewa ushauri nini wafanye.

“Lakini niwaambie kwamba watu waache kutumia mitishamba,kuweka mkojo kwenye macho na maji ya chumvi kwani kufanya hivyo kunaweza kunaweza kusababishia matatizo makubwa sana huku akishauri wafike kwa daktari ili waweze kupata tiba sahihi”Alisema

Aidha Daktari huyo aliwataka pia wale wanaopata maambukizi ya ugonjwa huo wasitumie dawa za mwenzake maana wakitumia dawa vibaya wanaweza kupata matatizo makubwa kwani kila mtu anakuwa na kipimo chake cha matumizi.

Dkt Hussein alisema kwamba mtu mmoja akipata ugonjwa huo anaweza kumuambukiza mwenzake huku akitoa tahadhari wananchi waache kushirikiana kwenye vitu kama vile Taulo,Vitambaa(leso) ya mwenzake ikiwemo maji ya choo.

Hata hivyo Dkt Hussein pia alisema kwamba hivi sasa wanaendelea kutoa elimu kwa wanafunzi ikiwemo maeneo mbalimbali ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo na hatua za kukabiliana nazo wanapokumbana na hali hiyo.

"Lakini mtu akiumwa na ugonjwa huo ikiwemo wanafunzi,watumishi wanashauriwa kupumzika nyumbani angalau siku mbili tatu ili asiendelee kusambaza kwa watu wengine "Alisema Dkt Hussein
DKT. MOLLEL AOMBA WANANCHI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KATIKA HAMASA YA KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE

DKT. MOLLEL AOMBA WANANCHI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KATIKA HAMASA YA KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE

February 02, 2024 Add Comment



Na WAF – Dodoma

Serikali imetoa wito kwa Watanzania, Viongozi wa kisiasa, kidini na kimila kuungana na Serikali katika kuhamasisha umma kujiunga na Bima ya Afya kwa wote pale mchakato utakapoanza rasmi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali namba 56 kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas Mbunge wa Jimbo la Kinondoni aliyeuliza Je, nini kauli ya Serikali juu ya Bima ya Afya kwa Watoto?

Dkt. Mollel amesema kuwa nchini kuna watoto Milioni 31, milioni 1.5 wako kwenye mfumo wa Bima ya afya ya sasa na milioni 30.7 wako kwenye mifumo ya bima za afya nyingine zilizopo nchini.

“Niwahakikishie wananchi kuwa ujio wa bima ya afya kwa wote utakuwa suluhisho la changamoto ya matibabu kwa wananchi wote bila kujali hali ya kiuchumi na kikwazo cha fedha, hivyo naomba mchakato utakapoanza wananchi mjitokeze kujiunga na skimu za zitakazobainishwa ambazo zitakua kwa rika zote”. Ameeleza Dkt. Mollel.

  

SERIKALI YAWATAKA WAZAZI KUWATOA WATOTO KWENYE KAMPENI YA KUPATA CHANJO

February 02, 2024 Add Comment

 SERIKALI kupitia Wizara ya Afya Nchini imewataka Wazazi, Walezi na Walimu kujitokeza kwa wingi kuwatoa watoto wote kwenye kampeni kubwa ya kupata chanjo ya Magonjwa ya Surua na Rubela ambayo itaanza mwezi wa pili ili kuimarisha kinga zao katika kuepukana na magonjwa ya milipuko.


Akizungumza leo Februari 01, 2024 Jijini Dar es Salaam Wakati wa Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Kutathimini Huduma za Chanjo Nchini kwa mwaka 2023, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amewahimiza wananchi kufanya usafi wa mazingira ili kuendelea kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

"Ni jukumu la wananchi kujikinga na maradhi ya milipuko kwa kufanya usafi wa mazingira, kunawa mikono ili kuhakikisha wanapoanda chakula katika mazingira bora hasa wakati wa kuwapatia watoto chakula na wazingatie kanuni za Afya" amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kununua vifaa vya afya, hivyo watumishi wanatakiwa kuzingatia maadili katika kuwapa wananchi taarifa sahihi, lengo ni kuhakikisha kwamba wananchi wanahudumiwa vizuri pindi wanapopata changamoto zao kutatuliwa kwa haraka.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema takribani mikoa nane tayari ina maambukizi ya kipindupindu, hivyo amewataka waganga wakuu wa mikoa kusimamia afua za usafi ili kuhakikisha miundombinu ya kunawia mikono ipo katika kukabiliana na magonjwa.

WAGONJWA WA RED EYE WARIPOTIWA KATIKA VITUO NA HOSPITAL MBALIMBALI ZANZIBAR

WAGONJWA WA RED EYE WARIPOTIWA KATIKA VITUO NA HOSPITAL MBALIMBALI ZANZIBAR

January 31, 2024 Add Comment






Naibu waziri wa afya Zanzibar Mhe.Hassan Khamis Khafidh akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya ugonjwa wa macho mekundu (red eye) huko Wizara ya Afya Mjini Unguja.



Mratibu wa huduma za afya ya msingi na matibabu ya macho dkt. Rajab Mohammed Hilal akitoa maelezo ya kitaalam kuhusiana na ugonjwa wa macho mekundu (red eye) huko Wizara ya Afya Mjini Unguja.
-


PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR

Na Fauzia Mussa, Maelezo Zanzibar

Jumla ya wagonjwa 4,579 wa ugonjwa wa macho (red eyes) wameripotiwa katika vituo vya afya, na hospitali Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya ugonjwa huo huko Wizara ya Afya wilaya ya mjini Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Hassan Khamis Hafidh amesema idadi ya takwimu hizo zimejumuisha wagonjwa waliofika kwenye vituo vya afya na hospitali za binafsi na serikali Unguja na Pemba.

Aidha amewataka wananchi kuacha kutumia dawa za kienyeji kutibu ugonjwa huo ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza sambamba na kuchukua tahadhari za usafi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara ili kujikinga na maradhi hayo .

amesema endapo jamii itaendelea kutumia dawa hizo kunaweza kuongeza ukubwa wa tatizo hilo hivyo aliwataka wananchi kufika hospitali mara tu wanapoona dalili za ugonjwa huo ili kupata matibabu stahiki na kwa wakati sahihi.

Hatahivyo aliiasa jamii kuacha kushikana mikono na mtu mwenye maambukizi au kugusa sehemu ya kitu ambacho kimeguswa na mtu huyo, na kuwataka kutumia maji baridi kunawia uso mara kwa mara, pamoja na kujitenga wakati wa kusubiri huduma katika vituo vya afya ili kuepusha maambukizi mapya.

“ni vizuri mgojwa yeyote wa macho asisubiri eneo walilokaa wagonjwa wengine atibiwe chumba maalum kilichotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa namna hiyo na akimaliza matibabu aende moja kwa moja nyumbani ili kupunguza hatari ya maambukizi mapya”alisema naibu Waziri.

Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusiana na ugonjwa huo mratibu wa huduma za afya ya msingi na matibabu ya macho Dkt. Rajab Mohammed Hilal
amesema ugonjwa wa macho mekundu husababishwa na virusi wanaoitwa Adenovirus na kupelekea maambukizi ya kirusi kwenye ngozi nyembamba inayozunguka gololi la jicho (conjunctiva) pamoja na kioo (Cornea) cha jicho.

Aliongeza kwa kusema ugonjwa huo unaambukizwa kutoka kwa mtu mmoja mwenye ugonjwa huo na kwenda kwa mwengine na kusambaza maambukizi kwa haraka sana ndani ya siku 10 hadi 12.

Alifahamisha kuwa dalili kubwa za ugonjwa huo ni pamoja na jicho kuwa jekundu, kuwasha na kuchomachoma , mifuniko ya macho kuvimba, macho kuogopa mwangaza, macho kutoa matongo matongo meupe au ya njano kuona ukungu kwa uoni wa mbali katika macho, pamoja na maumivu ya macho.

Alisema miongoni mwa athari za muda mrefu zinazoweza kujitokeza endapo jamii itaendelea kutumia dawa za kienyeji kutibu ugonjwa huo ni pamoja kupunguza uoni.

Itakumbukwa kuwa wiki mbili zilizopita ugonjwa wa macho mekundu (red eye) uliripotiwa katika mikoa ya Tanzania bara na kutokana na maingiliano ya wananchi ya mara kwa mara ugonjwa huo umeweza kuingia visiwani Zanzibar.

MTOTO AKAA SIKU 60 ICU HOSPITALI IKITUMIA MILIONI 10,100,000 KUMTIBU

January 26, 2024 Add Comment

 


 



Januari 26, 2024, Dodoma

Na Raymond Mtani-BMH

Novemba 11, 2023, Bi. Janeth (35), mkazi wa Manyoni Singida, alifika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) baada ya kukaa siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni akiimuuguza mwanaye aliyepatwa “degedege”.

Siku hiyo, ikawa safari ya siku 60 za mtoto wake huyo mwenye umri wa miaka 4 kwenye Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda ya Kati.

“watu walikuwa wanakuja, wanaruhusiwa wanamuacha mwanangu, wakati mwingine anabaki peke yake”. alisema Bi. Janeth.

Dkt. Venance Misago ni Bingwa wa Ganzi na Wagonjwa Mahututi, na Mkuu wa Idara ya Huduma za Uangalizi Maalumu BMH amesema, Moyo wa mtoto huyo ulisimama ghafla (cardiac arrest) mara nne (4) ndani ya siku 60 mtoto huyo alipokuwa ICU.

“aligundulika kuwa na maambukizi kwenye Ubongo (meningitis), hali iliyokuwa inasababisha apoteze fahamu mara kwa mara” alieleza Dkt. Misago.

Aidha, Dkt. Misago amesema kuwa kwa kawaida mgonjwa hukaa katika Chumba cha uangalizi maalumu siku 3 hadi 14 lakini maambukizi aliyokuwa nayo mtoto huyo yalisambaa kiasi cha kusababisha presha kushuka na kupelekea Moyo kusimama (septic shock) mara kwa mara.

Ingawa hali hiyo haikuwa rahisi kwa Bi. Janeth, hakusita kumshukuru Mungu, Madaktari na Wauguzi waliyomhudumia mwanaye.

“...nilipitia wakati mgumu kiasi cha kukata tamaa, namshukuru Mungu kwa kumponya mwanangu, nawashukuru Madaktari na wauguzi kwa kumpambania mwanangu” alieleza Bi. Janeth kwa furaha.

Kwa mujibu wa Awadhi Mohamed, Mkurugenzi Msaidizi huduma za Usitawi wa Jamii Hospitali ya Benjamin Mkapa imetumia Shilingi 10, 100,000 kugharamia dawa, vifaa tiba na chakula kwa kipindi chote cha siku 60 Mtoto wa Bi. Janeth alipokuwa ICU.

Kupona kwa mtoto huyo ni kielelezo cha faida za uwekezaji katika sekta ya Afya nchini, hasa mapinduzi yanayofanywa katika kuboresha huduma za Wagonjwa Mahututi.

Ingawa, wakosoaji wa serikali hasa Wizara ya Afya wamekuwa na jicho la kutoridhishwa na hatua za maboresho hususani kasi ya utekelezaji na ubora wa huduma, historia ni mwalimu mzuri.

Historia inakili kwamba, maboresho ya huduma ni mchakato, huduma za Afya nchini haziwezi kutokea ghafla mithili ya kimbunga, zinapitia mkondo huo huo wa mchakato wa maboresho ikiwa ni pamoja na huduma za ICU.

Mathalani, taarifa za Maktaba ya Historia ya Tiba ya Nchini Marekani zinadokeza mchakato wa maboresho ya huduma za ICU katika nchi za Ulaya ulianza kwa kanuni za kutenga majeruhi wa vita vya Crimean kwa kuwaweka mahututi jirani na vituo vya wauguzi (nursing stations) ili wapewe uangalizi maalumu.

Hiyo ilikuwa 1854, maboresho hayo yaliyohamasishwa na Bi. Florance Nightingale kusaidia kuokoa Maisha ya Majeruhi wengi wa vita, Ulaya ilisubiri karibu miaka 100 na mlipuko wa Polio kuwa na ICU ya kwanza, iliyojengwa 1953 huko Copenhagen, Denmark.

Hali hii ni tofauti na Tanzania, kwa mujibu wa Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, alipowasilisha Makadiliyo ya bajeti, mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, aliliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu hatua kubwa zilizopigwa katika huduma za Wagonjwa Mahututi.

Waziri huyo wa Sekta ya Afya, alinukuliwa Mei 12, 2023 akisema kuwa baada ya shambulio la Uviko 19, serikali imeweza kuongeza wodi za Wagonjwa Mahututi kutoka 45 had 258 ndani ya kipindi cha miaka 2, yaani 2020 hadi 2023.

“Tunaweza kulaza wagonjwa mahututi 1000 kila siku nchini” alisema Mhe. Ummy Mwalimu.

Hapana shaka, kama ilivyo kwa Mtoto wa Bi. Janeth, maboresho ya huduma za ICU yaliyofanyika katika kipindi hicho cha miaka 2 yamesaidia kuokoa maelfu ya Maisha ya Watoto na watu wazima waliyokumbwa na changamoto mbalimbali za kiafya zilizowalazimu kuhitaji ICU.

Mwaka 2020, Hospitali ya Benjamin Mkapa ilikuwa na Wodi ya Wagonjwa Mahututi yenye vitanda 6 pekee, lakini kupitia maboresho hayo, hadi Makala haya yanaandi.kwa, Hospitali hiyo ina Wodi mbili za wagonjwa Mahututi zenye vitanda 22.

Kwa mujibu wa Dkt. Misago, vitanda hivyo vina mashine za kusafisha mfumo wa hewa (Suction Machine), mashine za kusaidia kupumua (Ventilator), mashine za kusaidia Moyo, Figo na Kuzuia damu Kuganda (Syringe pump and Infusion Pump) pamoja na mashine za uangalizi wa mwenendo wa matibabu ya Mgonjwa (Monitors).

Hali hiyo, inasaidi kuokoa Maisha ya wanchi wengi wenye kuhitaji huduma hizo kwa uhakika, kumbuka iliichukua Ulaya miaka 99 kupata ICU ya kwanza, huku Tanzania ikijenga ICU zaidi ya 200 ndani ya siku 730.