Showing posts with label afya. Show all posts
Showing posts with label afya. Show all posts

TMDA YAWANOA WADHIBITI WA VIFAA TIBA BARANI AFRIKA JUU YA TATHMINI YA VIFAA TIBA VYA WAMAMA NA WATOTO

November 01, 2023 Add Comment


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini (TMDA) inaendesha mafunzo ya siku tatu Jijini Dar es Salaam ya kufanya tathmini ya udhibiti wa vifaa tiba vya Wamama, Watoto wachanga na Watoto kwa wataalam wa vifaa tiba kutoka Mamlaka za udhibiti za nchi 11 za Afrika.

Kongamano hilo ni la kwanza Barani Afrika ambapo mafunzo hayo yanafanyika kufuatia nchi za Afrika kutokuwa na uwezo wa kudhibiti bidhaa za Wakinamama na Watoto hivyo mafunzo hayo yatasaidia uwezo wa kutathimini bidhaa kabla hazijaingia kwenye soko.

Kongamano hilo la siku tatu, limezinduliwa mapema leo na Mkurugenzi wa Vifaa tiba na vitendanishi Bi. Kissa Mwamwitwa aliyekuwa amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Bw. Adam Fimbo ambapo ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Afya kwa kuipa uwezo TMDA kujulikana Afrika na kuweza kutoa utaalamu ambao wanatoa kwa Nchi zingine.

"Warsha hii imedhaminiwa na Wadau wa maendeleo USAID-MTaPS, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Jukwaa la Afrika la Udhibiti wa Vifaa tiba, AUDA-NEPAD na TMDA.

Tunaishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Rais wetu Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Afya kwa kutupatia uwezo ambao tunaonekana Bara la Afrika.’’ Amesema Bi. Kissa Mwamwitwa.

Ambapo amesema watabadilishana uzoefu ilikupata watalaam watakaokuwa wana uwezo wa kusaidia eneo hilo la vifaa tiba kwa akinamama na watoto kabla havijaingia sokoni.

"Ili kundi lilikuwa nyuma la akina mama, watoto wachanga na watoto wadogo. Hivyo kupitia mafunzo haya wadhibiti watakuwa wanatumika katika kutoa utalaam katika nchi zao baada ya kujifunza hapa.

Mafunzo haya yanafanyika kutokana na kuwa na mapungufu upande huo, na ni mara ya kwanza kufanyika hapa barani Afrika na tunashukuru Tanzania kuwa mwenyeji na pamoja na uwenyeji pia tumetoa watalaama ambao watashiriki kutoa mafunzo.’’ Amesema Bi. Kissa Mwamwitwa.

Wataalam hao wanatoka katika mamlaka za Udibiti wa vifaa tiba na vitendanishi kwa nchi za Afrika ikiwemo Uganda, Kenya, Ethiopia, Nigeria, Afrika Kusini, Botswana, Zambia, Rwanda, Ghana, Senegali na mwenyeji Tanzania.

Kwa upande wake Paulyne Wairimu ambaye ni Mwenyekiti wa Afrika Medical Forum-AMDF amebainisha kuwa Wadhibiti watapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ya tathimini na kufanyia kazi katika taasisi zao.

‘’Upande wa udhibiti vifaa vya Wamama na Watoto wachanga unaenda kupewa kipaumbele katika ukanda huu wa Afrika ilikusaidia eneo hili.’’ Amesema Paulyne Wairimu.

Nae mwakilishi kutoka USAID-MTaPs, Nereah Kisera amesema kuwa wanaendesha mpango wa vifaa kwa wamama na watoto kwa ufadhili chini ya USAID ambapo wakiwa na lengo la kuona kunakuwa na kujengewa uwezo mkubwa wa kuelewa juu ya vifaa upande wa udhibiti wa vifaa hivyo.



TANZANIA, UJERUMAN KUZUNGUMZA JINSI YA KUREJESHA MABAKI MIILI YA WATANZANIA ILIYOPO NCHINI HUMO

October 31, 2023 Add Comment

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Frank-Walter Steinmeier mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Oktoba, 2023.


-Rais Samia asema ndugu wanasubiri  mabaki ya miili ya wapendwa wao,  aishukuru Ujeruman

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

SERIKALI za nchi za Tanzania na Ujeruman zimesema  zitafanya  mazungumzo yatakayowezesha mabaki ya miili ya watanzania walipoteza maisha wakati wa ukoloni yaliyopo nchini Ujerumani yanarejeshwa nchini.

Kwa muda mrefu mabaki ya miili hiyo ya Watanzania imehifadhiwa katika makumbusho mbalimbali nchini Ujerumani na sasa uamuzi wa kuyarejesha umefikia hatua nzuri na hatimaye mabaki hayo yarejeshwe na kukabidhiwa kwa ndugu.

Ikumbukwe kwamba baadhi ya mabaki hayo ni ya miili ya machifu na viongozi waliokuwa vinara katika vita vya Tanganyika dhidi ya Ujerumani (Maji Maji).

Akizungumza leo Oktoba 31, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Ujerumani  Frank-Walter Steinmeier amesema katika mazungumzo yao wamezungumza masuala mbalimbali likiwemo kurejeshwa kwa mabaki hayo.

"Nakushukuru Rais Frank - Walter Steinmeier kwa kukubali mualiko wangu wa kuja kufanya ziara nchini,  huu ni uthibitisho wa uhusiano mzuri  kwa miaka miaka 60 baina ya nchi hizi.

"Katika mazungumzo yetu tumejadili masuala mbalimbali lakini tumezungumzia kuhusu mabaki ya wapendwa wetu walioko Ujerumani ,  tunaendelea kuzungumza ili mabaki ya miili ya wapendwa wetu irejee nyumbani Tanzania.

Wakati anazungumzia mabaki hayo , Rais Dk.Samia amesema anajua kuna familia ambazo zinasubiri mabaki ya miili ya ndugu zao ambayo yapo kwenye   makumbusho za Ujerumani, lakini sasa wanakwenda   kuyazungumza ili yaweze kurudishwa Tanzania.

Akielezea zaidi kuhusu mazungumzo kati yake na Rais Steinmeier, Rais Samia amesema wamezungumza kuhusu kuendelea kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili sambamba na kushirikiana katika nyanja mbalimbali kama elimu, afya, uhifadhi , kilimo, sekta ya ubunifu na maeneo mengine ambayo wamekuwa wakishirikiana.

Aidha Rais Samia ameishukuru nchi ya Ujeruman kwa misaada mbalimbali waliyoitoa na wanayoendelea kuitoa kwa ajili ya kusaidia maeneo mbalimbali akitolea mfano kuwa katika eneo la Bima ya Afya kwa Wote nchi hiyo iliahidi kusaidia lakini wanaendelea na ujenzi wa hospitali kubwa Dodoma.

"Ujeruman wamekuwa wakitusaidia katika maeneo mbalimbali,  mbali ya ujenzi wa hospitali pale Dodoma lakini Ujeruman wametusaidia kujenga Hospitali Lugalo.Pia wamekuwa wakitusaidia katika uhifadhi katika hifadhi ya Serengeti na Selous.

Kwa upande wake Rais wa Ujeruman Steinmeier amemshukuru Rais Dk.Samia kwa kumualika kufanya ziara nchini huku akielezea namna ambavyo wamekuwa na mazungumzo mazuri yanayolenga kuimarisha uhusiano na kushirikiana katika sekta mbalimbali.

Kuhusu mabaki ya miili ya watanzania yaliyoko nchini Ujeruman amesema hilo ni jambo ambalo linazungumzika na watafikia pazuri huku katika hilo litaambatana na kupeleka Ujerumani taarifa za hali za wahanga wa vita vya majimaji ambao natarajia kukutana nao kesho.

" Nitakwenda kukutana na wahanga wa vita , nitawasikiliza na yale ambayo watanieleza nitakwenda nayo Ujeruman ili kufikisha ujumbe wao, "amesema huku akieleza ni vema pia nchi hizo  kutosahau historia ya mambo yaliyopita na kubwa zaidi kudumisha uhusiano .

Pia amesema katika eneo la ubunifu,  amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwasaidia wabunifu wachanga ili kukuza bunifu zao lakini amesisitiza kuendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali.

WAZIRI UMMY AWATAKA WATUMISHI WA HOSPITALI YA RUFAA YA BOMBO KUFANYA KAZI KWA BIDII

October 17, 2023 Add Comment


WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu akisisitiza jambo kwa timu ya usimamizi wa huduma za Afya mkoa (RHMT) na Timu ya uendeshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga –Bombo (HMT) leo mara baada ya kutembelea hospitali hiyo,kulia kwake ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Bombo Dkt  Rashid Suleiman akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo Dkt Joseph Mberesero

KATIBU wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo Abasi Mlawa akimueleza jambo wakati wakati wa ziara yake alipozungumza na timu ya hospitali hiyo (HMT)

Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo Abasi Mlawa kushoto akisisitiza jambo kwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kulia ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt Rashid Suleiman


 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kushoto akimuonyesha Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo Abasi Mlawa kulia eneo ambalo kutajengwa jengo la mama na mtoto katika Hospitali hiyo wakati wa ziara ya Waziri huyo leo katika Hospitali hiyo
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu na Mbunge wa Jimbo la Tanga (CCM) katikati akisisitiza jambo kwa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Dkt Rashid Suleiman kulia ni Dkt Juma Ramadhani ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Matibabu ya  Dharura katika Hospitali hiyo (EMD) 


Na Oscar Assenga,TANGA

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo huku akiwataka watumishi wa Hospitali hiyo kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuhakikisha wagonjwa wanaokwenda wanapata huduma.

Ummy ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga (CCM) amefanya ziara ya kutembelea kwenye hospitali hiyo ambapo pamoja na mambo mengine alizungumza na timu ya hospitali hiyo (HMT) ambapo aliwataka madaktari na wauguzi kuhakikisha wanatoa maelezo sahihi ya wagonjwa wanaolazwa kwa ndugu.

Amesema hatua hiyo itawaepusha kuwaondolea wagonjwa sintofahamu hususani wanapokuwa wakiulizwa na aina ya ugonjwa anaoumwa mgonjwa wake .

Akiwa kwenye mazungumzo hayo aliwataka watumishi wa Hospitali hiyo kufanya kazi kwa waledi mkubwa hususani katika kuwahudumia wagonjwa wanaofika kupata huduma za matibabu.

Hata hivyo amewapongeza watumishi kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuwatiaa moyo huku akiwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea

ZAIDI YA WAGONJWA 1000 WAFANYIWA UCHUNGUZI NA KUPATIWA MATIBABU KAMBI YA MADAKTARI BINGWA TANGA

September 27, 2023 Add Comment
Mratibu wa Kambi hiyo ambaye pia ni Mhazini wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt Mathew Shao kulia akiteta wakati wa kambi ya Huduma za Madaktari Bingwa wa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayoendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga.

Wananchi wakiendelea kupatiwa huduma mbalimbali wakati wa kambi hiyo inayoendelea kwenye viwanja vya CCM Mkwakwani Jijini Tanga






Na Oscar Assenga, TANGA

ZAIDI ya wagonjwa 1000 wamefanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu katika kambi ya Huduma za Madaktari Bingwa wa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayoendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga.

Kambi hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga Mhe. Ummy Mwalimu iliyoanza Septemba 25 mwaka huu na inayotarajiwa kumalizika leo tarehe 27 September ilikuwa ikitoa huduma za kibingwa katika magonjwa mbalimbali.

Akizungumza leo Mratibu wa Kambi hiyo ambaye pia ni Mhazini wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt Mathew Shao alisema mwamko wa wananchi umekuwa kuridhisha kutokana na kuongezeka idadi yao kila siku.

Dkt Shao ambaye pia ni Daktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa alitaja magonjwa hayo ya kibingwa ni Moyo,Sukari,Mifupa,Pua/koo,masikio,wanawake na uzazi,kinywa na meno,watoto ,mfumo wa mkojo(Urojolia) na Macho.

Aliyataja magonjwa mengine ni ya Upasuaji,utoaji wa dawa na vipimo vya sukari,moyo-Echo,ECG,Utrasound,Sickle Cell,Uzito na urefu,hali ya lishe,ukimwi/TB,Ushauri na nasaha na elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza (NCD)

Mwisho.

MAMIA YA WANANCHI WAJITOKEZA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA UCHUNGUZI TANGA

September 25, 2023 Add Comment
Huduma Matibabu ya Kibingwa zikiendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga 
Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Moi Dkt Hellena Mwijage akizungumza kuhusiana na kambi hiyo ya matibabu
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali Jijini Tanga wakipatiwa huduma 

Huduma za upimaji urefu zikiendelea katika kambi hiyo
Sehemu ya Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo wakiendelea wakiwa tayari kuwahudumia wananchi kwenye kambi hiyo


Na Oscar Assenga, TANGA.

MAMIA ya Wananchi kutoka maeneo mbalimbali Jijini Tanga wamejitokeza kwa wingi kwenye kambi ya Huduma za Madaktari Bingwa kwa Uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayoendelea kwenye viwanja vya Mkwakwani.

Kambi hiyo ya Huduma za Madaktari Bingwa imeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) ambapo siku ya kwanza ya zoezi hilo mwitikio wa wananchi walijitokeza kwa wingi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kupata matibabu wananchi hao walifurahia huduma hiyo huku wakikipongeza chama cha madaktari kwa kuwa na utaratibu huo mzuri kwa wananchi.

Akizungumza mmoja wa wananchi hao Jonas Mwakifuo ambaye ni Mkazi wa Mwanzange Jijini Tanga alisema kwamba huduma ambazo zinatolewa ni nzuri kwa sababu wananchi wengi wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali lakini hawana fedha za kuweza kugharamia matibabu.

Alisema hivi sasa kumekuwa na wimbi kubwa la magonjwa mbalimbali ikiwemo tezi dume na mfumo wa mkojo na figo ambayo yamekuwa yakiwatesa wananchi wengi hivyo uwepo wa madaktari hao utawasaidia kuweza kupata matibabu ya kibingwa.

“Kwa kweli tunawashukuru madaktari Bingwa hawa maana hii imekuwa ni faraja kubwa sana kwetu kwa sababu tunapata huduma kwa hakika niwapongeeza madaktari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya”Alisema

Kwa upande wake mkazi wa Sahare Jijini Tanga Zuhura Omari alisema kwamba kambi hiyo imekuja wakati muafaka kwani hivi sasa wananchi wengi wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari na uzito mkubwa.

Alisema hivyo huduma hiyo inakwenda kuwa mwarobaini wa kutibu magonjwa hayo hivyo wanashukuru kwa madaktari wote ambao wamefanikisha huduma hiyo muhimu kwao.

Hata hivyo Mariam Saidi ambaye ni mkazi wa Barabara 12 Jijini Tanga alisema kwamba kambi hizo ni muhimu kutokana na kwamba zinawapa fursa wananchi kuweza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yanayowakabili kwa muda mchache.

Akizungumza katika kambi hiyo Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Moi Dkt Hellena Mwijage alisema kambi hiyo ni utaratibu ambao wamekuwa wamejiwekea kila wanapoadhimisha Kongamano la Madaktari nchini wanaanza na shughuli za kijamii.

Mwijage alisema kwa mwaka huu Kongamano hilo linafanyika mkoani Tanga hivyo wameanza na huduma za kijamii na wamepiga kambi kwenye uwanja wa Mkwakwani kwa muda wa siku tatu

Hellena ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) alisema kambi hiyo ya uchunguzi kwa magonjwa mbalimbali itakuwa ya siku tatu huku wananchi wakikaribishwa wajitokeze kuweza kupata huduma na matibabu rasmi na muhimu kutokana na matatizo yao.