DKT.KIJAJI AZINDUA CHANJO YA MIFUGO NGORONGORO

July 03, 2025


Na Mwandishi Wetu, NCAA.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amezindua zoezi la Chanjo ya Mifugo katika Kijiji cha Mokilal Tarafa ya Ngorongoro Mkoani Arusha ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa miaka mitano wa kuchanja mifugo.

Dkt. Kijaji ameeleza kuwa katika utekelezaji wa zoezi hilo ambalo ni mpango wa kitaifa wa Miaka mitano kuanzia 2025-2030 ulizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 16 Juni, 2025 Bariadi Mkoani Simiyu na tayari kiasi cha shilingi bilioni 216 zimetengwa kufanya kazi hiyo na mwaka huu  zaidi ya Bilioni 62 imeshatolewa.

Amesema kuwa Serikali imetoa punguzo la bei na kila Ng'ombe mfugaji atachangia shilingi  500 badala ya  shilingi 1000 na Mbuzi na Kondoo wafugaji watachangia shilingi 300 pekee badala  ya shilingi 500 ambapo mpango huu unalenga kuwasaidia wafugaji.



Mkurugenzi wa huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Benezeth Lutege ametaja 

Sababu za kuchanja mifugo hiyo kuwa ni

Kuongeza thamani mifugo kwenye masoko ya nje,  kujua idadi ya mifugo na wamiliki wake ili kurahisisha upangaji wa maeneo ya malisho na sababu nyingine kuwasaidia amana katika vyombo vya kifedha kupata mikopo kwa kuwa  taarifa za mifugo yao itakuwa inatambulika mifumo ya kielektroniki (barcode)  kupitia alama ya hereni za utambuzi kwa kila mmiliki wa mifugo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.  Kenan Kihongosi ameeleza kuwa Wananchi wa Ngorongoro na Mkoa wa Arusha kwa ujumla wamekuwa na muitikio mkubwa katika zoezi hilo na wataendelea kuhamasisha wafugaji wote kuchanja mifugo yao ili kutimiza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha maisha ya Wananchi

Mbunge wa Ngorongoro Mhe. Emmanuel Shangai ameishukuru Serikali kwa kuwasikiliza Wafugaji na kuwapatia chanjo ya mifugo yao na kuwaomba Wananchi wote kujitokeza kuchanja mifugo hiyo ili kuondokana na maradhi mbalimbali,  kuboresha afya na thamani ya mifugo yao.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »