MAPADRI KANISA KATOLIKI SINGIDA WAFANYA UTALII NGORONGORO NA KUHAMASISHA JAMII KUTUNZA MAZINGIRA

June 18, 2025

Kassim Nyaki, NCAA.


Mapadri 11 kutoka parokia mbalimbali za jimbo katoliki Singida leo tarehe 18 Juni, 2025 wamefanya ziara ya kutembelea vivutio vya vya utalii katika hifadhi ya Ngorongoro na kusisitiza uhifadhi na utunzaji wa mazingira ili kuendelea kuvutia wageni wengi.

Kiongozi wa mapadri hao Padri John Makabe ameeleza kuwa, ziara yao imelenga kuona maajabu wa Mungu aliyoyaumba katika hifadhi ya Ngorongoro, vivutio vya utalii kama wanyamapori, malikale na mandhari mbalimbali zilizopo  ili kwa nafasi zao wahamasishe jamii umuhimu wa uhifadhi na  kutunza mazingira kwa manufaa ya wanadamu wote.

“Tumekuja kuona mazingira na kuhimiza utunzaji wake, neno la Mungu katika kitabu cha mwanzo tumeambiwa Mungu aliumba vitu vyote na kuwakabidhi binadamu ili wavitunze na kuvilinda, sisi watumishi wa mungu ni  sehemu ya utume wetu kuelezea habari ya umuhimu wa kutunza mazingira, ziara yetu hapa Ngorongoro imetusaidia  kuona ukweli wa maajabu ya Mungu kupitia hifadhi hii, tutaendelea kuhamasisha watu kutambua umuhimu wa mazingira kama zawadi tuliyopewa na mungu ili tuyatunze na yenyewe yatutunze kwa vizazi na vizazi” amesema Padri Makabe.

Akipokea ujumbe wa mapadri hao, Kamishna Msaidizi mwandamizi anayesimamia huduma za Utalii na Masoko Mariam Kobelo ameeleza kuwa hifadhi ya Ngorongoro imeendelea kupokea wageni wengi wa ndani na nje ya nchi na kubainisha kuwa jitihada za Serikali na wadau wa sekta binafsi kutangaza vivutio vya utalii nchini zimeendelea kuzaa matunda ambapo uongozi wa NCAA unahakikisha kuwa wageni wote wanapata huduma bora na kufurahia shughuli za utalii wanapokuwa ndani ya hifadhi.


Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »