Na. Zainab Ally - Kilombero
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA, limeungana na mamilioni ya Wanawake Duniani kwa kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa leo Machi 8, 2025, katika mji wa Ifakara, Wilaya ya Kilombero, mkoa wa Morogoro, Maadhimisho hayo yalihusisha maelfu ya wanawake kutoka taasisi, mashirika na jamii Mkoani Morogoro, ambapo yalilenga kuhamasisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika nyanja mbalimbali, hasa katika uhifadhi wa maliasili.
TANAPA ilitumia fursa hiyo kutangaza hifadhi zake na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa maliasili, Kwa kutumia mabango, michoro ya mandhari ya hifadhi, na shamrashamra za nyimbo za kizalendo zilizovutia hisia za maelfu ya wanawake waliohudhuria Maandamano hayo makubwa yaliyoanzia katikati ya Mji wa Ifakara yakizunguka maeneo mbalimbali, yakijumuisha ujumbe wa usawa na haki za kijinsia.
Katika kilele cha maadhimisho hayo, TANAPA ilionesha umuhimu wa rasilimali za hifadhi kwa viongozi waliohudhuria akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, ambapo Kyobya aliongozana viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wabunge, na viongozi wa CCM kutembelea mabanda ya bidhaa mbalimbali likiwemo banda la TANAPA, lililokuwa sehemu ya kutangaza rasilimali za Taifa na kuonyesha juhudi za uhifadhi zinazofanywa na TANAPA.
Aidha, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa, Theodora Batiho, alieleza kwa kina mchango wa TANAPA katika matumizi ya teknolojia ya kisasa, akitaja gari maalumu la kuonesha video za hifadhi ambalo limeleta matokeo chanya katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi, uharibifu wa mazingira, na madhara ya ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa, huku akisisitiza kuwa teknolojia ya majiko banifu ya kupikia, inayotolewa kwa jamii, imekuwa na faida kubwa katika kupunguza uharibifu wa mazingira.
Katika hotuba yake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero aliwahimiza wanawake kuishi katika maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kujenga uchumi imara na kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Alisisitiza kuwa usawa na uwezeshaji wa wanawake ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya kitaifa.
Kauli mbiu ya maadhimisho haya, "Wasichana na Wanawake 2025: Tuimarishe Usawa, Haki na Uwezeshaji," iliendelea kutoa wito kwa wanawake kuwa mstari wa mbele katika kujenga jamii yenye usawa na fursa sawa kwa wote, huku wakiwa na jukumu muhimu la kulinda maliasili na mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo.
TANAPA, kwa kushirikiana na wanawake wengine walionesha ushirikiano na juhudi za pamoja ikiwa ndio msingi muhimu katika kujenga Taifa lenye maendeleo endelevu, ambapo usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake, na uhifadhi wa maliasili ni nguzo muhimu kwa mafanikio ya taifa.
EmoticonEmoticon