Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji wa Serikali, Geryson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali katika mkutano uliofanyika Desemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam.
..............................
Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam
SERIKALI imepanga
kutoa ruzuku ya tani 52,000 za mbegu bora za mahindi kwa wakulima katika msimu
wa 2024/2025.
Hayo yamebainishwa
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji wa
Serikali, Geryson Msigwa wakati akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali
yaliyotekelezwa na Serikali katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika
Desemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam.
“ Hadi
kufikia Novemba 30, 2024 jumla ya tani 4,000 za mbegu bora za mahindi zenye
thamani ya Sh. 3,496,721,000 ya ruzuku zimenunuliwa na wakulima 79,335,”
alisema Msigwa.
Akizungumzia
upatikanaji wa mbegu bora alisema makadirio ya mahitaji ya mbegu hizo nchini
kwa msimu wa 2024/2025 ni tani 80,000 ambapo upatikanaji umefikia tani
42,471.09 sawa na asilimia 53 ya makadirio ya mahitaji.
Alisema kati
ya tani hizo , tani 29,819.57 zimezalishwa ndani ya nchi na tani 12,651.52
zimeingizwa kutoka nje ya nchi.
Msigwa
alisema uzalishaji wa ndani wa mbegu zilizothibitishwa ubora za mazao
mbalimbali umeongezeka kutoka tani 42,096.68 msimu wa 2022/2023 hadi kufikia
tani 56,114 msimu wa 2023/2024.
Alisema hali
hiyo inaonesha kuimarika kwa uzalishaji wa ndani wa mbegu ikiwa ni hatua
mahsusi ya kuchangia utoshelevu wa pembejeo za kilimo ndani ya nchi kwa
kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na kushirikisha sekta binafsi katika
uzalishaji wa mbegu kwa kutumia mashamba ya Serikali yanayomilikiwa na Wakala
wa Mbegu za Kilimo (Agricultural Seed Agency – ASA).
Akizungumzia
makadirio ya mahitaji ya mbolea na visaidizi vyake kwa msimu wa 2024/25 ni tani
1,000,000 ambapo hali ya upatikanaji wa mbolea
nchini kufikia tarehe 30 Novemba, 2024 ulikuwa ni tani 769,060 sawa na asilimia
77 ya mahitaji.
Alisema kiasi
hicho cha upatikanaji kilitokana na bakaa ya msimu uliopita tani 260,403,
uzalishaji wa ndani tani 58,669 na zilizoingizwa kutoka nje ya nchi tani
449,988.
“ Uzalishaji
wa ndani wa mbolea umeendelea kuimarika kutokana na jitihada zinazofanywa na
Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa kutumia malighafi za ndani
ikiwemo rock phosphate ambapo uzalishaji wa ndani wa mbolea umeongezeka kutoka
tani 84,696 mwaka 2022/2023 hadi tani 158,628 msimu wa 2023/2024,” alisema
Msigwa.
Akielezea utekelezaji
wa utoaji wa ruzuku ya mbolea na mbegu bora katika msimu wa 2024/2025 alisema Serikali
inatekeleza mpango wa utoaji wa Ruzuku ya Mbolea na mbegu bora za mahindi kwa wakulima.
Alisema lengo
la utoaji wa ruzuku hiyo ni kupunguza gharama ya mbolea kwa mkulima ili
kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na
kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda.
Msigwa
akizungumzia mfumo wa utoaji wa ruzuku ya mbegu za mahindi na mbolea alisema utaratibu
wa utoaji wa ruzuku unatumia mfumo wa kidigitali wa Digital Subsidy System
ambao unaratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (Tanzania
Fertilizer Regulatory Authority –TFRA) na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu
Tanzania (Tanzania Official Seed Certification Institute – TOSCI).
Alisema utoaji
wa ruzuku unazingatia mahitaji halisi ya mkulima kulingana na taarifa za
usajili na bajeti ya Serikali iliyotengwa.
Aidha,
Msigwa akizungumzia usajili wa wakulima na wafanyabiashara wa pembejeo alisema
ili kutekeleza mpango wa mbolea na mbegu za ruzuku kupitia mfumo huo wa
kidigitali, wakulima wanapaswa kujisajili katika daftari la usajili wa wakulima
kwenye ngazi ya Kijiji/ Kata.
Alisema baada
ya kujisajili kwenye daftari, maafisa kilimo wanaingiza taarifa za wakulima hao
kwenye mfumo wa kidigitali wa utoaji wa ruzuku ya pembejeo.
Alisema wakulima
kupitia simu zao hupokea ujumbe mfupi unaowafahamisha namba ya siri ambayo
wataitumia kununua mbegu za mahindi na mbolea ya ruzuku kwa kipindi cha msimu
wa kilimo kulingana na ukubwa wa shamba na aina ya zao aliloainisha wakati wa usajili.
Msigwa
alisema mkulima haruhusiwi kutumia namba ya simu ya mtu mwingine wakati wa
usajili au kununulia mbegu na mbolea.
Katibu Mkuu
huyo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema wazalishaji,
waagizaji, wasambazaji binafsi (mawakala) na Vyama vya Ushirika vinavyohusika kununua
na kusambaza mbegu na mbolea husajiliwa na TOSCI na TFRA na kupewa namba
maalumu ya usajili.
“ Hadi
kufikia Novemba 30, 2024, jumla ya wakulima 4,141,730 , kampuni 31 na
wafanyabiashara/mawakala 2877 wa mbolea na mawakala 666 wa mbegu bora wenye
jumla ya vituo vya mauzo (Active outlets) 7,000 wamesajiliwa kwenye mfumo, “
alisema Msigwa.
Alisema utoaji
wa ruzuku ya mbolea na mbegu bora kwa wakulima msimu wa kilimo wa 2024/2025 umeanza
katika baadhi ya mikoa inayopata mvua kuanzia mwezi Oktoba ikiwemo mikoa ya Mbeya,
Kagera, Kigoma, Njombe, Dodoma, Singida, Morogoro, Tabora, Geita, Shinyanga,
Mwanza, Mara, Simiyu, Manyara, Iringa, Rukwa, Katavi na Songwe ambapo ununuzi
wa mbolea na mbegu bora unaendelea.
Alisema katika
kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai, 2024 hadi kufikia tarehe 30 Novemba, 2024 jumla ya tani 253,669.342 za
mbolea zenye thamani ya Shilingi 435,724,224,815 zimenunuliwa kwa utaratibu wa
ruzuku na wakulima 406,966 ambapo ruzuku ya Serikali ni Sh. 90,485,490,128.
Msigwa
aliongeza kuwa katika kuimarisha huduma za ugani, Serikali imenunua na
kusambaza vishikwambi 5,285 kwa Maafisa Ugani, magari 15 kwa maafisa Kilimo
ngazi ya mkoa, magari madogo 10 kwa maafisa Kilimo ngazi za wilaya na pikipiki
6,444 kwa maafisa wa Kata na Vijiji.
Alisema ,
Serikali imenunua na kusambaza vipima afya ya udongo 143 (soil scanner); visanduku
vya ugani 1,000 (extension kit) na sare za maafisa ugani 6,456.
Aidha,
Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba 50 za maafisa ugani pamoja na kununua
pikipiki 300 ili kutosheleza mahitaji ya pikipiki kwa maafisa ugani waliopo.
Msigwa
alitumia mkutano huo kutoa wito kuwa msimu wa kilimo umeanza katika maeneo
mengi nchini, hivyo wakulima wote wahakikishe wana namba ya mkulima ambayo
pamoja na kuwawezesha kununulia mbolea pia inatumika kunununulia mbegu bora za
mahindi kwa mfumo wa ruzuku.
Kwa wakulima
ambao hawajapata namba hiyo, wajitokeze kwenye ofisi za vijiji/mitaa kwa ajili
ya kujiandikisha kwenye daftari la mkulima.
Aliwaomba Wataalam
wa kilimo katika ngazi za Wilaya na Vijiji/mitaa kwa kutumia vishikwambi
walivyopewa, waongeze kasi ya usajili wa wakulima kwenye mfumo ili kuwezesha
wakulima kupata namba zitakazotumika kununualia mbolea na mbegu bora za ruzuku.
Halmashauri zote Tanzania Bara zitoe kipaumbele
katika uimarishaji na ugharamiaji wa huduma za ugani kwa kuhakikisha kwamba
kila Afisa Ugani anatumia vitendea kazi alivyopewa na anatekeleza wajibu wake kwa
kuwahudumia wakulima ipasavyo.
Msigwa
alihitimisha mkutano huo kwa kueleza kwamba Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji
wa mkutano mkubwa wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa masuala ya Nishati
utakaofanyika Januari 28, 2025.
Alisema hatua
hiyo inatokana na mkakati wa Serikali ya Awamu ya sita ya kuimarisha
upatikanaji wa nishati ya umeme nchini kwa kupeleka umeme vijijini na
vitongojini kwa kasi hali ambayo imewavutia viongozi hao kuamua kufanyia
mkutano huu mkubwa nchini kwetu.
Alisema sisi
kama wanahabari tunalo jukumu la kushiriki na kuendelea kuwahabarisha
Watanzania kuhusu mafanikio haya muhimu.
Alisema Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini ambapo hadi sasa vijiji 12,278 kati ya vijiji 12,318 tayari vimeunganishwa kwa umeme. Vijiji 40 vilivyosalia vitakuwa vimeunganishwa na umeme ndani ya mwezi huu.
EmoticonEmoticon