CP. WAKULYAMBA AWASILI SIMIYU, KUTEKELEZA AGIZO LA MHE. DKT. NCHIMBI.

October 17, 2024

 




Na Sixmund Begashe – Simiyu

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba amewasili Mkoani Simiyu kwa ziara ya kikazi ambayo ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa agizo la Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi alilotoa hivi karibuni alipotembelea Mikoa ya kanda ya ziwa.

Katika ziara hiyo,Mhe. Dkt. Nchimbi aliutaka Uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kufika Mkoani humo kushughulikia changamoto za Wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi hususan Tembo.

Akizungumza na uongozi wa Mkoa wa Simiyu, CP. Wakulyamba amesema kuwa kwa sasa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara hiyo inaongeza mikakati ya mapambano dhidi ya Wanyamapori wakali na waharibifu kwa kuajiri askari zaidi wa Uhifadhi, kuongeza vitendea kazi na kuwapatia ujuzi zaidi askari wa Uhifadhi pamoja na kushirikiana na wananchi katika mapambano dhidi ya hao Wanyamapori wakali na waharibifu.

CP. Wakulyamba ameuhakikishia uongozi wa Mkoa kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya uongozi wa Waziri Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na Katibu wake Mkuu Dkt. Hassan Abbasi utaendelea kushirikiana na Serikali ya Mkoa pamoja na wananchi katika kuhakikisha changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu inaisha sambamba na kuimarisha uhifadhi endelevu wa Maliasili zetu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Katibu Tawala Msaidi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, Bw. Juma Topela, ameupongeza uongozi wa Wizara ya Maliasili kwa ushirikiano mkubwa unatoa kupitia Jeshi la Uhifadhi katika kupambana na changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu pale wananchi wanapo toa taarifa.

Bw. Juma Topela ameahidi kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na Wizara hiyo ili Malengo ya Serikali ya kuendelea kuwalinda wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori hao yanafikiwa.

CP. Wakulyamba atakuwa Mkoani Simiyu kwa siku tatu ambapo licha ya kukutana na Viongozi mbalimbali wa Mkoa na Wilaya ya Simiyu na Meyatu, atatembelea pia Pori la Akiba Maswa na Kijereshi kabla ya kuendelea na ziara Mkoa wa Mara, Mwanza na Geita.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »