WAZIRI wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali itaendelea kusimamia ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapata huduma bora za afya popote alipo na kwa wakati.
Mhe. Mhagama ametoa kauli hiyo mapema leo, alipofanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa lengo la kujionea namna hospitali hiyo inavyotoa huduma, ambapo ameupongeza uongozi na watumishi wa Muhimbili kwa namna wanavyotoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wananchi kwa kuzingatia weledi ubora unaotakiwa.
Mhe. Mhagama amesema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa miundombinu, vifaa tiba vya kisasa vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu na kusomesha wataalam imewezesha wataalam hao hususani wa Muhimbili (Upanga &Mloganzila) kutoa huduma za ubingwa bobezi na kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi kwa matibabu.
“Sekta ya afya hapa Tanzania ndani ya miaka hii mitatu imekuwa kuliko kipindi chochote kwani katika hospitali zetu za Taifa na kipekee Muhimbili tunazo zaidi ya aina 35 za matibabu ya ubingwa bobezi ikiwemo upandikizaji wa uloto, upandikizaji wa figo, matibabu ya magonjwa ya moyo n.k, uwekezaji ambao unaacha deni kwetu la kutoa huduma bora kwa Watanzania wenzetu ili waweze kufurahia matunda ya uwekezaji huo” amebainisha Mhe. Mhagama
Aidha, Mhe. Mhagama ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa motisha na kuwajengea uwezo wataalam ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko yanayotokea duniani kwa lengo la kuendelea kuimarisha utoaji wa matibabu hapa nchini kadiri mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanavyojitokeza duniani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini MNH Dkt. Ellen Senkoro amemuhakikishia Mhe. Waziri kuwa bodi itashirikiana na menejimenti kuhakikisha kuwa wanatafsiri kwa vitendo maono ya Mhe. Rais na maelekezo ya wizara hatimaye watu wote wanaotibiwa Muhimbili wapate huduma bora na zenye kukidhi matarajio yao.
Mhe. Waziri katika ziara yake ameambatana na viongozi mbalimbali wa Wiraza ya Afya akiwemo Naibu Katibu Mkuu Bw. Ismail Rumatila pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa wizara hiyo.
EmoticonEmoticon