SERIKALI YATAKA WANANCHI KUITAMBUA NA KUITUAMINI MIRADI YA MAENDELEO KATIKA MAENEO YAO

September 15, 2024

 


Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imewataka wananchi kuitambua na kuthamini uwekezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao na kuacha imani potofu katika utekelezaji wa miradi hiyo, hususani ujenzi wa Skimu za umwagilliaji na barabara kwa madai kuwa maeneo ya miradi ni ya matambiko hivyo isitishwe.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe katika muendelezo wa ziara yake ya kikazi akiwa Mkoani Tabora ambapo alitembelea eneo la mradi wa Umwagiliaji Mwasimbo Igunga, Mwampuli, Mwanzugi na Makomero.

Akiwa katika ziara hiyo ameahidi kurudisha ushirika katika eneo la mradi wa umwagiliaji Mwampuli, kujengwa fensi kuzunguka maeneo ya shamba kwa ajili ya usalama na kukarabati maghala ya mpunga.

Pia, kuanzisha kituo cha zana za kilimo ambacho kitakua na trekta na pawatila za serikali kwa ajili ya wakulima hao.

Waziri Bashe, ameelekeza kujengwa kwa bwawa upya, kujenga mashine za kukoboa mpunga na kukarabati za awali na kuweka mipaka katika eneo la umwagiliaji.

Waziri Bashe, amesema ameshangazwa na hatua ya wananchi wa Nzega vijijini kupinga utekelezaji wa miradi ya skimu za umwagiliaji unaohusisha ujenzi wa miundombinu ya bwawa la Nsembo, ujenzi wa barabara, madaraja madogo na mitaro ya kupitisha maji pembezoni mwa barabara.

Amesema, wananchi hao wanapinga miradi hiyo kwa imani potofu kuwa inapingana na mila na sehemu inapopita miradi hiyo ni maeneo ya matambiko hivyo iondolewe.

“Hii inashangaza sana ndugu zangu wa Nzega vijijini ipo haja sisi serikali kuongeza utoaji elimu, haiwezekani wananchi wanasimama na kudai hawataki barabara, hawataki miundombinu, wanachotaka ni ngoma za asili na matambiko, hivyo hatua zinazochukuliwa na serikali ni kuharibu mila,”amesema waziri Bashe

Akiwa wilayani Igunga Waziri Bashe, ameahidi kutuma timu ya wataalamu kufanya utafiti katika ujenzi wa bwawa la kukusanya maji, kutokana na maji mengi wakati wa mvua katika maeneo hayo, huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalam wa Wizara hiyo watakapo fika kufanya utafiti.


"Ninawaomba ndugu zangu wataalam watakapofika muwape ushirikiano," aliomba.

Ameeleza kuwa bwawa litakapojengwa watawekewa maeneo ya kunyweshea mifugo lengo ni kuhakikisha mifugo haingii mashambani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa,amesema Tume ipo katika hatua za mwisho kuanza utekelezaji wa mradi wa skimu ya Mwamapuli iliyopo katika Kijiji cha Mwanzugi, kata ya Igunga wilaya ya Igunga -Mkoa wa Tabora.

Amesema skimu hiyo ilijengwa kwa mara ya kwanza mwaka 1968 hadi mwaka 1970 lakini bwawa lilikamilika mnamo mwaka 1986 hadi mwaka 1994, mifereji na miundombinu ya shambani ilijengwa na jumla ya hekta 630 zilianza kumwagiliwa Katika mwaka wa fedha 2024/2025.

“Serikali kupitia Tume imedhamiria kuboresha na kuendeleza skimu ya Mwampuli ambapo jumla ya hekta 1,557 zitajengewa miundombinu ya umwagiliaji na kufanya skimu kuwa na jumla ya hekta 2,187,”amesema Mndolwa

Mndolwa ameongeza kuwa mradi huo umeshatangazwa kwa ajili ya kumpata Mkandarasi atakaye fanya shughuli ya ujenzi.

Kwa upande wa mkazi wa eneo hilo, Jilala Shomba, amesema kuwa wapo tayari kwa miradi inayoletwa na serikali katika maeneo yao.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »