RAIS SAMIA KUFUNGA TAMASHA LA TATU LA UTAMADUNI KITAIFA MKOANI RUVUMA

September 10, 2024

 Na Mwandishi Wetu,Dodoma


Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeandaa tamasha la tatu la utamaduni ambalo litafanyika Mkoani Ruvuma Manispaa ya Songea kuanzia Tarehe 20 hadi 23 septemba 2024.

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa amezungumza na wanahabari jijini Dodoma leo ambapo amesema tamasha hilo litafunguliwa na Waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo Dkt Damas Ndumbaro na kilele cha tamasha hilo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasani.

"Tamasha hili linaratibiwa na wizara yetu Kwa kushirikiana na waratibu wa tamasha la majimaji, Serebuka kutoka Mkoani Ruvuma Songea.

Msigwa amesema tamasha hilo limekuwa na faida nyingi Kwa jamii ambazo ni pamoja na kuenzi utamaduni, kuimarisha utangamano wa Kitaifa, kuitangaza nchi, kutangaza vivutio vya Utalii na kiutamaduni, kiuchumi, Kijamii, kutanua wigo na mitandao ya kibiashara kwa bidhaa zinazozalishwa nchini hususani bidhaa za utamaduni, Sanaa na ubunifu.

Madhumuni ya tamasha hili ni pamoja na; kuenzi na kulinda utamaduni wetu, kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia ukuzaji wa sekta za ubunifu na utamaduni, kutoa jukwaa la kuonyesha utamaduni kama msukumo madhubuti wa utangamano wa kitaifa kwa kuwaleta/kuwaunganisha pamoja wadau na viongozi wa sekta, kuendeleza na kuenzi urithi wa utamaduni wetu, kutoa fursa ya majadiliano ya kitaaluma baina ya wananchi wa kila mkoa, kutumia utamaduni na ubunifu kama nyenzo ya kuenzi na kukuza utambulisho wa Taifa na kutangaza fursa na rasilimali za kipekee ilizonazo nchi yetu.

Aidha Msigwa amesema tamasha la mwaka huu litakuwa na vionjo mahsusi kama ifuatavyo:-

1. Tamasha litakuwa na mirindimo ya kiasili, kuanzia mavazi, maonesho, visasili na visakale.

2. Tamasha litakuwa na mdahalo wa kitaifa utakaozungumzia mapambano dhidi ya viashiria vya mmomonyoko wa maadili na nini mchango wa jamii katika kupunguza na hatimaye kuondoa viashirika hivyo:

3. Tamasha litakuwa na onesho maalumu la matumizi ya kanga ikiwa ni vazi la utamaduni wa Mtanzania

4. Tamasha litakuwa na zaidi ya vikundi 25 kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar; vikundi hivyo ni vya sanaa ya asili, ubunifu, utamaduni na mziki wa kizazi kipya.

5. Tamasha litakuwa na mashindano ya uhifadhi wa ngoma za asili kwa vikundi 25 vya Tanzania Bara na visiwani.

6. Tamasha litakuwa na kliniki ya Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo


Hata hivyo kutokana na umuhimu na mvuto wa tamasha hilo Msigwa ameomba na kuwahakikishia kampuni zote, mashirika, asasi na taasisi zinazotoa huduma mbalimbali, washirika wa maendeleo na wadau kwa ujumla kutojitokeza kudhamini tamasha hilo.

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahususi ya kufungamanisha utamaduni na utalii, utamaduni na biashara, utamaduni na uchumi kwa ujumla."- Msigwa


Kwa ujumla, tamasha hilo ni fursa muhimu katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisayansi, kisiasa na kiutamaduni. Aidha, ni njia mahususi ya kukuza viwanda vya ubunifu sanaa na utamaduni nchini. Tamasha linaandaliwa katika namna ya kuzitangaza tunu zetu, vivutio vyetu vya kiutamaduni, hivyo Watanzania wote wanaombwa kushiriki.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »