NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, SONGEA
SERIKALI
imewahakikishia Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya
Kazi, kuwa inayachukulia kwa uzito mkubwa, maoni na mapendekezo yao kuhusu
maboresho ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi
Kauli
hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, wakati akifunga
Kikao Kazi cha Mafunzo ya Uelimishaji kwa Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kusini na Watendaji wa Tume ya Usuluhishi
na Uamuzi (CMA) mjini Songea, Februari 10, 2024.
Akieleza
zaidi Mhe. Profesa Ndalichako amesema tayari inayafanyia kazi baadhi ya
mapendekezo ya maboresho ya sheria yaliyotolewa na waheshimiwa Majaji kwenye
kikao kazi kama hicho kilichofanyika mjini Bagamoyo mwezi Julai, 2023
“Mapendekezo
ya kuboresha kifungu cha 39 (2) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263]
kilichoweka ukomo wa muda wa kuwasilisha madai bila kutoa wigo wa kupokea madai
hayo iwapo kuna sababu za msingi za kucheleshwa, tumeyafanyia kazi na
tunataraji muswada wa marekebisho kuwasilishwa bungeni hivi karibuni.” Amesema
Mhe. Profesa Ndalichako.
Aidha,
Mhe. Profesa Ndalichako amesema Ofisi yake kupitia Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi inatarajia kupokea maoni zaidi kutoka kwa waheshimiwa majaji kwa
lengo la kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi
[Sura 263].
“Natamani
kuona kuwa kati ya mapendekezo yenu katika mafunzo haya iwe ni namna gani
rahisi tunaweza kutumia sheria kuwezesha waajiri wote ambao hawajajisajili WCF,
kufanya hivyo mara moja,” amesema
Mhe.
Profesa Ndalichako pia amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya
Uongozi mahiri wa Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa wafanyakazi katika sekta
zote na ndio maana imeendelea kutekeleza na kuboresha masuala ya fidia kwa
wafanyakazi katika sekta binafsi na umma
Amesema,
katika kipindi kifupi cha Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kumeshuhudiwa
mabadiliko mbalimbali katika sekta ya hifadhi ya jamii ikiwemo kupunguza
kiwango cha uchangiaji kwa waajiri wa sekta binafsi kutoka asilimia 1 ya
mshahara wa mfanyakazi kila mwezi hadi kufikia asilimia 0.5;
Awali
akifungua mafunzo hayo mwishoni mwa juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani aliwahimiza waajiri nchini kujisajili WCF na
kutoa taarifa za ajira za wafanyakazi wao ili kulinda haki za wafanyakazi hao
pindi wanapopatwa na majanga wakiwa kazini.
"Pamoja
na uwepo wa sheria inayowabana waajiri wanaoshindwa kuwasajili wafanyakazi wao
WCF lakini bado kuna waajiri ambao hawatoi taarifa za ajira za wafanyakazi wao
na hivyo kuuweka mfuko katika nafasi ngumu ya kutekeleza majukumu yake,"
alifafanua
Jaji
Siyani ametoa mfano wa kisa cha mfanyakazi mmoja aliyekuwa akifanya kazi kwenye
kampuni moja ya ujenzi mkoani Lindi ambaye aliumia akiwa kazini na kupelekea
kupoteza baadhi ya viungo vyake na
kumsababishia ulemavu wa kudumu kwa zaidi ya asilimia 75 lakini alikosa vigezo
vya kupata fidia kwa kuwa mwajiri wake hakuwa amejisajili na kuwasilisha
michango WCF kwa mujibu wa sheria.
“Licha
ya kijana huyo kufanya kazi kwa zaidi ya miaka miwili lakini taarifa zake
hazikuwepo WCF na hivyo kukosa haki ya kupata fidia yoyote” ameeleza Jaji
Siyani; na kuongeza kuwa iwapo zingekuwepo taarifa za mfanyakazi huyo, bila
shaka angepata fidia bora zaidi ya ile iliyotokana na majadiliano na maridhiano
na mwajiri wake.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John
Mduma, amesema Mahakama ya Tanzania ni wadau muhimu wa Mfuko huo katika
utekelezaji wa majukumu yake kwa kuwa Mfuko unategemea maamuzi mbalimbali ya
mahakama katika utekelezaji wake wa majukumu ikiwemo maamuzi ya kesi za
mirathi.
Dkt.
Mduma amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya
Serikali yanayozitaka taasisi zake kuhakikisha zinashirikiana kwa
karibu kwa dhumuni la kuongeza tija na huduma bora kwa wananchi.
Pia,
mafunzo hayo yanatoa fursa ya kubadilishana uzoefu baina ya wataalam wa
Mahakama na WCF kupitia mada mbalimbali zitakazowasilishwa ambapo washiriki
wanaweza kuja na mapendekezo yatakayoboresha utendaji kazi wa Mfuko huo.
"Ni
matarajio yangu kuwa mafunzo haya yataleta manufaa makubwa kwa pande zote
mbili, ikiwemo kuimarisha mahusiano kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi
na kuchangia kukuza uchumi wa nchi yetu na hasa kupunguza umasikini kwa
wafanyakazi watakaopata majanga yanayotokana na kazi zao," amesisitiza Dkt.
Mduma.
Mafunzo
hayo ambayo ni ya awamu ya nne yamewaleta pamoja washiriki kutoka mikoa ya
Ruvuma, Mtwara, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa ambapo miongoni mwa mada
zinazotarajiwa kuwasilishwa ni kuhusu sheria ya fidia kwa wafanyakazi, taratibu
za uwasilishaji na ushughulikiaji wa madai ya fidia kwa wafanyakazi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (katikati)
akizungumza wakati akifunga Kikao kazi cha Mafunzo ya Uelimishaji kwa
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania - Divisheni ya Kazi, Kanda ya
Kusini, iliyofanyika Februari 10, 2024. Wengine pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa
WCF, Dkt. John Mduma (kushoto) na kulia ni Mhe. Joseph Karayemaha, Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Songea.
EmoticonEmoticon