HISTORIA MPYA MIUNDOMBINU YA KIMKAKATI KUANDIKWA

May 24, 2023

 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli moja limeridhia na kuidhinisha zaidi ya shilingi trilioni 3.5 kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Bajeti hiyo pamoja na mambo mengine inatarajiwa kuweka historia nchini ambapo barabara kuu na za mikoa zenye urefu wa kilometa 2,035 zinatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha Lami na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo mbalimbali.

Akijibu hoja za wabunge wakati wa majumuisho ya bajeti ya Wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kwa dhati kuifungua nchi kiuchumi kupitia miundombinu ya kimkakati inayosimamiwa na Wizara kwa upande wa Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi.

Prof. Mbarawa amezitaja barabara 7 zenye urefu wa kilometa 2,035 zitakazojengwa kwa utaratibu wa EPC + F kuwa ni barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo   – Londo – Lumecha/Songea (km 435), barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa (Simiyu) (km 339) na barabara ya Handeni – Kibirashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Olboroti – Mrijochini – Dalai – Chambalo – Chemba – Kwa Mtoro – Singida (km 460).

Miradi mingine ni barabara ya Arusha – Kibaya – Kongwa Junction (km 453.42), barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale (km 175), barabara ya Igawa – Songwe – Tunduma (km 218), barabara ya mchepuo ya Uyole – Songwe yenye urefu wa kilometa 48.9 pamoja na barabara ya Mafinga – Mtwango – Mgololo (km 81).

Aidha, barabara ya Express way kutoka Kibaha-Chalinze-Morogoro ambayo ujenzi wake unashirikisha sekta binafsi  itajengwa huku miradi ya mabasi ya mwendo kasi ya DART na daraja la Jangwani vikitengewa Bilioni 2.2.`

Kwa upande wa Sekta ya Uchukuzi shilingi Trilioni 1.13 zinatarajiwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ikiwemo vipande vipya vya Dodoma hadi Kigoma, Uvinza hadi Burundi na DRC.

Ununuzi na utengenezaji wa ndege nne utakaogharimu takriban shilingi bilioni 300 utatekelezwa ukiwa ni mkakati wa kuendelea kuifufua ATCL ili kulifanya shirika hilo kuwa na tija na kuchagiza uchumi nchini.

Profesa Mbarawa amesema Serikali imejipanga kuhakikisha huduma za usafiri wa anga, utabiri wa hali ya hewa na usafiri kwa njia ya maji zinakuwa salama na za uhakika.

Jumla ya wabunge 75 wamechangia katika bajeti hiyo ambapo kati ya hao 67 kwa kuongea na nane kwa maandishi. Na hatimaye bunge kupitisha kifungu kwa kifungu Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »