DC MATIRO AONGOZA MKUTANO WA WADAU WA CHANJO YA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI MKOA WA SHINYANGA

April 17, 2018

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mheshimiwa Josephine Matiro amefungua na kuongoza mkutano wa wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Shinyanga uliolenga kujadili namna ya kufanikisha zoezi la chanjo hiyo kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 mkoani humo. kutano huo umefanyika leo Jumanne Aprili 17,2018 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Shinyanga.

Akifungua mkutano huo,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga alisema Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na wadau wa chanjo imeanzisha chanjo mpya ya kuwakinga na ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.

Matiro alisema saratani ya mlango wa kizazi ni ya kwanza nchini Tanzania kwa kusababisha vifo ikifuatiwa na saratani ya matiti ambazo zote zinasababisha zaidi ya asilimia 50 ya vifo vyote vya akina mama vitokanavyo na saratani hivyo kunahitajika juhudi na ushirikiano zaidi kupunguza vifo hivyo.

“Lengo la kuanzisha chanjo hii ni kukinga mabinti kutokana na madhara makubwa yanayoweza kuwapata ambayo husababisha vifo vingi kwa wanawake,na walengwa wa chanjo hii mwaka huu ni wasichana wote wanaotimiza miaka 14 ambapo katika mkoa wa Shinyanga wasichana wasiopungua 29,479 watachanjwa”,aliongeza.

Alisema chanjo hiyo itatolewa bila malipo katika vituo vya kutolea huduma vya serikali na binafsi ,baadhi ya shule na maeneo katika jamii ambazo zitatolewa kwa njia ya huduma za mkoba.

“Saratani hii inachangiwa na vitu vingi ikwemo kuanza kujamiiana katika umri mdogo,kuwa na wapenzi wengi,ndoa za mitaala,kuzaa watoto wengi na uvutaji wa sigara”,alieleza.

Alizitaja dalili za saratani ya mlango wa kizazi kuwa ni kutokwa damu ya hedhi bila mpangilio,kutokwa damu baada ya kujamiiana,maumivu ya mgongo,miguu na kiuno,kuchoka,kupungua uzito,kukosa hamu ya kula,kutokwa uchafu wa rangi ya kahawia au wenye damu kwenye uke na maumivu ya miguu au kuvimba.

Hata hivyo alisema dalili mbaya zaidi zinazoweza kujitokeza kuwa ni pamoja na kuishiwa damu,figo kushindwa kufanya kazi,kupatwa na fistula na uvimbe wa tezi.

Kwa upande Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Dkt. Rashid Mfaume alisema kati ya wasichana 7304 wanaougua saratani ya mlango wa kizazi nchini kila mwaka,4216 sawa na asilimia 58 wanafariki dunia hivyo ni muhimu zaidi kupata kinga kuliko tiba.

Alisema uzinduzi rasmi wa chanjo hiyo mkoani Shinyanga utazinduliwa siku ya Jumatatu Aprili 23,2018 katika manispaa ya Shinyanga.

Naye Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Albert Msovela alisema tayari pesa kwa ajili ya chanjo hiyo zimeshatumwa kwenye halmashauri kinachotakiwa ni utekelezaji tu ili kuhakikisha mkoa unafanya vizuri katika zoezi hilo la utoaji chanjo kwa wasichana. ANGALIA PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MKUTANO HUO HAPA CHINI



Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akifungua mkutano wa wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Shinyanga - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog




Matiro alisema serikali imeamua kuanza kutoa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa sababu saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kwa kuua wanawake wengi ukilinganisha na saratani nyingine nchini.



Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Dkt. Rashid Mfaume akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Shinyanga.


Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Shinyanga.

Mkutano ukiendelea...


Wadau wakiwa ukumbini..Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba na Afisa Tawala wilaya ya Kahama, Said Yasin


Kushoto ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngassa Mboje akiwa na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bakari Kasinyo

Wadau wakiwa ukumbini



Mkutano unaendelea


Mtakwimu (Mpango wa taifa wa chanjo), David Kayabu akitoa mada kuhusu zoezi la chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi


Daktari wa Meno mkoa wa Shinyanga, Dkt. Nuru Mpuya ambaye ni Mkufukunzi wa mafunzo ya chanjo ya HPV akitoa mada ukumbini kuhusu chanjo hiyo

Afisa Elimu mkoa wa Shinyanga, Mohammed Kahundi akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo

Picha za pamoja wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi
Picha za pamoja wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi

Picha za pamoja wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi


Picha za pamoja wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »