DKT. KALEMANI AENDELEA KUZINDUA MIRADI YA UMEMEMVIJIJINI AWAMU YA TATU (REA PHASE III MIKOA YA KUSINI NA RUKWA

August 15, 2017
                   Na Henry Kilasila - Rukwa

Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dkt Medard Kalemani ameendelea na ziara za uzinduzi wa Miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA PHASE III) ambapo Agosti 14, 2017 alikuwa Mikoani Rukwa katika Kijiji cha Kabwe Wilaya ya Nkasi.

Dkt. Kalemani alisema jumla ya Shilingi Bilioni 42.5 zitatumika kupeleka umeme katika Mkoa huo na kuongeza Mradi huo utatekelezwa katika vipindi viwili tofauti ambapo sehemu ya kwanza itahusisha upelekaji umeme katika vijiji 111.

"Sehemu ya pili itahusisha vijiji 145 ambapo itaanza baada ya kukamilika kwa sehemu ya kwanza. Kufikia mwaka 2021 vijiji vyote vya Mkoa wa Rukwa vitakuwa vimepatiwa umeme".Alisema Dk. Kalemani.

Aidha, Dkt. Kalemani alimtambulisha Mkandarasi atakayejenga Mradi wa REA Mikoani humo Kampuni ya Kitanzania ya Nakuroi Investment Company Limited.

Alimwagiza Mkandarasi kuhakikisha anapeleka umeme Kijiji kwa Kijiji na Kitongoji kwa Kitongoji bila kuruka na sehemu zinazotoa huduma za Kijamii kama Mashule, Zahanati, Magereza, Visima vya maji, Nyumba za Ibada na sehemu mbalimbali.

Pia alitoa maagizo kwa TANESCO kupeleka Ofisi katika Kijiji cha Kabwe na katika maeneo yote yenye Wateja wengi lakini wapo mbali na Huduma za TANESCO.

Aliongeza kwa kuwataka Mameneja na Watalaamu wa TANESCO kutokukaa Ofisini bali wawafuate Wateja.Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TANESCo, Dkt. Tito E. Mwinuka aliwaomba Wananchi hao wa Kabwe kuwa waaminifu na kutoa ushirikiano kwa Watendaji wa TANESCO kabla na hata baada ya Mradi kukamilika.

"Muitunze miundombinu ya umeme, msiihujum wala kuichoma moto". Alisema Dkt. Mwinuka.Alisema TANESCO imejipanga kuhakikisha Wananchi hao wanapata huduma ya umeme iliyobora na ya uhakika.

Mbunge wa Nkasi, Ali Kessy aliwaeleza Wananchi kuwa mradi huo wa usambazaji umeme vijijini hauna malipo ya fidia hivyo watoe ushirikiano kwa wakandarasi hao wakati wanatekeleza mradi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Nkansi Mheshimiwa Saidi Mtanda aliushukuru Uongozi wa TANESCO kwa kwani umekuwa ukitoa ushirikiano pale unapohitajika.
"Mheshimiwa Mgeni Rasmi katika Kijiji cha Nyamare kwenye chanzo cha maji tulileta Mkandarasi akatukadilia bei ya Transifoma milioni 60, tuliwasiliana na uongozi wa TANESCO wametufungia Transfoma kwa pesa zao milioni 24". Alisema Mheshimiwa Mtanda.

Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dkt Medard Kalemani alimalizia uzinduzi Mkoani Rukwa kwa kuwakabidhi Wazee kumi zawadi ya kifaa cha UMETA.
Naibu waziri Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dkt Medard Kalemani akifurahia baada ya kuzindua mradi wa REA RUKWA
Naibu Waziri Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani akiwasili eneo la uzinduzi Mkoani Rukwa, akiwa amepokelewa na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mheshimiwa Saidi Mtanda.
Kutoka kushoto Mkurugenzi Mkuu REA, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TANESCO Dkt. TITO E. Mwinuka katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Kampuni ya Nakuro Investment Company Limited inayojenga Mradi huo wa umeme Mkoani humo. 
Naibu waziri Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dkt Medard Kalemani akipata maelezo ya namna kifaa cha UMETA kinavyofanya kazi kutoka kwa Bw. Lucas Kusare Afisa Huduma kwa Wateja Mkoa wa Rukwa .

DKT. KALEMANI AENDELEA KUZINDUA MIRADI YA UMEMEMVIJIJINI AWAMU YA TATU (REA PHASE III MIKOA YA KUSINI NA RUKWA

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »