NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI,DK.MEDARD KALEMANI AZINDUA MRADI WA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI MKOA WA SHINYANGA AWAMU YA TATU

April 02, 2017

A 1
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani akizungumza na wananchi kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu jana wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme vijiji katika mkoa wa Shinyanga awamu ya tatu.
A 2
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani akibonyeza kitufe kuwasha kifaa maalumu cha Umeme Tayari (UMETA) kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu jana wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme vijiji katika mkoa wa Shinyanga awamu ya tatu jana.
A 3
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani (katikati) akikata utepe jana kuashiria uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme vijiji katika mkoa wa Shinyanga awamu ya tatu jana kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu.
A 4
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack katika uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme vijijini.
A 6
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga akizungumza.
A 5
Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi akizungumza na wananchi baada ya kutambulishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba (pembeni yake).
A 7
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani akifurahia ngoma na kikundi cha utamaduni wakati wa hafla ya uzinduzi huo.
A 8
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani akimzawadia kifaa maalumu cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho kinatumika bila utandazaji nyaya (wiring) katika nyumba, mkazi wa kijiji cha Negezi wakati wa uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini.
A
Sehemu ya wananchi wakifuatilia matukio katika hafla hiyo ya uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini kijijini Negezi kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu.
A 9
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani akiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba kuelekea sehemu ya kukaa mara baada ya kuwasili viwanja vya uzinduzi kijijini Negezi. Kushoto ni Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kangese.
Na Mwandishi Maalumu, Kishapu
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani amezindua mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu katika mkoa wa Shinyanga wilayani Kishapu wenye thamani ya sh. bilioni 35.5.
Katika uzinduzi huo uliofanyika kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu, ukihusiha vijiji 149, Dk. Kalemani aliagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikishwa wanasambaza umeme sehemu zote bila upendeleo.
Aliwahimiza wananchi kutumia fursa ya kuwepo kwa nishati hiyoi katika kuboresha maisha yao kwa kutumia miradi ya uzalishaji mali pamoja na huduma mbalimbali za kijamii.
Aliwataka wautumie kwa kujenga viwanda vya kusindika mazao pamoja na huduma za afya,elimu, maji na viwanda vingine kama mashine za kusaga ambazo zitawapatia kipato na kuboresha maisha.
Aidha, naibu waziri huyo alizitaka serikali za kata na vijiji kubainisha maenbeo maalumu ya viwanda ambayo katika mradi huo yatafikishiwa miundombinu ya umeme mkubwa.
”Tunataka kuwezesha wajasriamali vijijini kupatiwa umeme utakaowezseha kuanzishwa kwa viwanda vidogo na vikubwa vijijini kwa gharama nafuu,” alisema Dk. Kalemani.
Aliongeza kuwa wananchi watakaounganishiwa umeme wanatakiwa kukamilisha utandazaji wa nyaya katikia nyumba zao mapema ili mkandarasi akifika wawe tayari kulipia na kuunganishiwa umeme.
Alisema kwa sehemu ambazo utandazaji utakuwa haujakamilika au nyumba si kubwa wanahimizwa kuomba kufungiwa kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho hakihitaji kutandaza nyaya.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba aliishukuru Serikali kwa mradi huo wa REA huku akisema utasaidia kutengeneza ajira wilayani humo.
Taraba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema nishati ya umeme vijijini itasaidia kuanzishwa kwa viwanda vidogo na vya kati hivyo aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo na kuacha uharibifu wa mazingira.
Hata hivyo, alitoa kilio chake kwa kumuomba naibu waziri kushughulikia changamoto ya baadhi ya wakandarasi kutomaliza miradi kwa wakati jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo.
Pia mkuu huyo wa wilaya aliwaomba wananchi watoe ushirikiano kwa kutoa maeneo kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya umeme kwa kuwa ni kujiletea maendeleo yao wenyewe.
 Aliomba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Shinyanga kutatua kero ya kukatika kwa umeme mara kwa jambo ambalo limekuwa ni kero kwa wananchi na linarudisha nyuma maendeleo.
Utekelezaji wa mradi huo ulianza Februari 2017 na unatarajiwa kukamilika Machi 2019 ambapo tayari sh. bilioni 7.4 zimetumika katika awamu ya kwanza wakati awamu ya pili jumla ya sh. bilioni 22.95 zilitumika.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »