Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye kipaza sauti)
akiwatambulisha wafanyakazi wa Kampuni ya Nakuroi Investment Co. Ltd
(waliochuchumaa), ambao watatekeleza Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu mkoani Singida.
Sehemu
ya umati wa wananchi waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Mradi
Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika Mkoa wa
Singida. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni katika Kijiji cha Mkwese,
wilayani Manyoni.
Moja
ya vikundi vya ngoma kutoka Manyoni, kikitumbuiza katika hafla ya
uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu
katika Mkoa wa Singida. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni katika
Kijiji cha Mkwese, wilayani Manyoni.
Na Veronica Simba – Dodoma
Wakala
wa Nishati Vijijini (REA), umesitisha mkataba wa Mkandarasi Spencorn
Services, aliyekuwa akitekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu
ya pili kwa Mkoa wa Singida.
Mkurugenzi
Mkuu wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga aliyasema hayo hivi karibuni
katika hafla ya uzinduzi wa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini
awamu ya Tatu katika Mkoa wa Singida, uliofanyika kijijini Mkwese,
wilayani Manyoni.
Mhandisi
Nyamo-Hanga alimweleza Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Mradi huo, Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwa, ufanisi wa kazi wa
Mkandarasi husika haukuwa mzuri hivyo kusababisha baadhi ya vijiji
ambavyo vilipangwa kupelekewa umeme katika REA II, kutofikiwa na huduma
hiyo.
“Tumechukua
hatua za kinidhamu. Tumemsimamisha kazi na tutaleta wakandarasi wapya
ambao wataendelea na kazi ya kusambaza umeme pale alipoishia.”
Aidha,
Mkurugenzi Nyamo-Hanga alitoa shukrani kwa Serikali kwa ushirikiano na
msaada ambao imekuwa ikitoa, ulioiwezesha REA kuendelea na zoezi la
kuwafikishia umeme wananchi wa vijijini kwa mafanikio makubwa.
Alisema
kuwa, gharama ya utekelezaji wa REA III Mkoa wa Singida ni shilingi
bilioni 47.36 ambapo jumla ya vijiji vitakavyonufaika ni 267. Aliongeza
kuwa, Mkandarasi atakayetekeleza Mradi huo ni Nakuroi Investment Co.
Ltd.
“Tutaanza
na kuunganisha umeme katika vijiji 185 na baadaye tutamalizia vijiji 82
vitakavyokuwa vimebaki, na kuwezesha vijiji vyote vya Mkoa wa Iringa
kuwa na umeme kwa asilimia 100.”
Idadi ya vijiji vilivyo na umeme hadi sasa kwa Mkoa wa Singida ni 196, sawa na asilimia 42.
Mhandisi
Nyamo-Hanga, amewataka wananchi watakaounganishiwa umeme katika Mradi
wa Kusambaza Umeme Awamu ya Tatu, kama ilivyokuwa kwa Mradi wa Awamu ya
Pili; kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao mapema ili
wakati mkandarasi atakapofika katika maeneo yao, wawe tayari kulipia na
kuunganishiwa umeme.
Vilevile,
ameomba Serikali za Kata na Vijiji kubainisha maeneo maalum ya viwanda
ambayo katika mradi huu, yatafikishiwa miundombinu ya umeme mkubwa ili
kuwezesha wajasiriamali vijijini kupatiwa umeme utakaowezesha kuanzishwa
kwa viwanda vidogo vidogo na vikubwa vijijini kwa gharama nafuu.
Uzinduzi
wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaendelea
katika Mikoa mbalimbali nchini. Mpaka sasa, uzinduzi umekwishafanyika
katika Mikoa ya Tanga, Pwani, Dodoma, Iringa, Mbeya, Songwe, Mara na
Singida. Kwa Mkoa wa Shinyanga, uzinduzi utafanyika tarehe 1 Aprili,
mwaka huu.
EmoticonEmoticon