Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akionyesha mbegu bora ya muhogo
aina ya Momba inayozalishwa katika shamba la Mpambaa halmashauri ya
Singida, katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo na
anayefuata ni Afisa Kilimo halmashauri ya Singida Abel Mungale.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta
Rehema Nchimbi akiandaa mashimo ya kupanda mbegu bora ya mbaazi
inayozalishwa katika shamba la Mpambaa halmashauri ya Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta
Rehema Nchimbi akipamba mbegu bora ya mbaazi inayozalishwa katika shamba
la Mpambaa halmashauri ya Singida, anayefuata ni Mwenyekiti wa
halmashauri ya Singida Eliya Digha.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta
Rehema Nchimbi akiwaonyesha watumishi wa halmashauri namna ya kupanda
mbegu bora ya mbaazi katika shamba la Mpambaa halmashauri ya Singida.
Watumishi wa halmashauri ya Singida wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi (hayupo pichani).
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akipanda mti wa mwembe katika eneo la sekondari ya Ilongero Wilayani Iramba.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akipanda viazi
lishe na mihogo katika shamba la mkulima bora wa eneo la Old Kiomboi
Wilayani Iramba.
……………….
Watumishi wa halmashauri zote saba
za Mkoa wa Singida wameagizwa kulima nusu ekari ya mazao yanayotumia
maji kwa ufanisi hasa zao la muhogo, viazi au mtama ili kuwa na uhakika
wa chakula cha kutosha msimu ujao huku shule zote zikiagizwa kulima
ekari moja ya mihogo au mtama ili wanafunzi wapate chakula shuleni.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta
Rehema Nchimi ametoa agizo hilo alipotembelea na kuzindua shamba la
mbegu bora ya mihogo la ekari kumi lililopo kijiji cha Mpambaa,
Halmashauri ya Singida ambalo litazalisha mbegu kwa ajili ya wakulima wa
Mkoa wa Singida.
Dokta Nchimbi ametumia kauli mbiu
ya kuongoza ni kuonyesha njia kwa kulima mihogo shamba lake mwenyewe
lenye ukubwa wa ekari tatuna hivyo kuwaagiza watumishi na viongozi wote
kuonyesha mfano kwa kulima mazao hayo kwa msimu huu.
Pamoja na upandaji wa mbegu za
Muhogo, Dokta Nchimbi pia amezindua shamba la mbegu bora za mbaazi kwa
kupanda mbegu hizo pamoja na kupalilia shamba la mbegu bora za mtama
ambapo aina 25 za mtama zinafanyiwa majaribio ili kupata mbegu
itakayofaa kwa mkoa wa Singida.
Aidha ametembelea mashamba ya
wakulima wa mtama wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi pamoja na kushiriki
upandaji wa mtama wa shamba la shule ya Msingi Mampanta wilayani Iramba
na kupanda viazi na mihogo katika shamba la Mkulima wa Old Kiomboi
wilayani Iramba.
Amesema wakulima wakielimishwa juu
ya mazao yanayotumia maji kwa ufanisi watapanda mazao hayo ambayo ni
mtama, viazi, muhogo na mbaazi ambapo wakulima watakuwa na uhakika wa
chakula pamoja na kujipatia fedha kwa kuuza mazao hayo.
Dokta Nchimbi ametoa hamasa kwa
wakulima wote kulima mazao hayo yanayotumia maji kwa ufanisi na wajitume
kwa bidii kuliko kulalamikia serikali bila kufanya kazi kwakuwa awamu
ya sasa ya uongozi ni ya kuchapa kazi kwa bidii.
Wakati huo huo Dokta Nchimbi
amefanya vikao na watumishi wa halmashauri za Singida, Ikungi na Iramba
mara baada ya kutembelea mashamba ya wakulima na kushiriki nao katika
kupanda mtama, kupalilia baadhi ya mashamba, kupandqa mihogo na viazi.
Dokta Nchimbi amewaasa watumishi
wote Mkoani Singida kuwa waadilifu, wachape kazi na hasa kulima mazao
yanayotumia maji kwa ufanisi pamoja na kufanya shughuli nyingine za
kuwaingizia kipato kama vile kufuga kuku na kuwa na mizinga ya nyuki ili
wawe na kipato kingine nje ya mshahara.
Amesema watumishi wengine
hujiingiza kwenye wizi kutokana na tamaa tu ila endapo watakuwa na
vyanzo vingine vya fedha nje ya mshahara itapunguza kutokuwa waaminifu
pamoja na kutokulalamika mara kwa mara.
Baadhi ya watumishi waliohudhuria
vikao hivyo wamempongeza Mkuu wa Mkoa Dokta Nchimbi kwa nasaha alizowapa
huku wakiahidi kuchapa kazi kwa bidii na uadilifu pamoja
wakijishughulisha na kilimo ili wawe na kipato cha ziada.
EmoticonEmoticon