Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Ashatu Kijaji akijibu hoja
mbalimbali za wabunge katika mkutano wa tano wa Bunge la 11
linaloendelea Mjini Dodoma.
……………………………………………………………………………
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Benki
Kuu ya Tanzania (BOT) imesitisha kuweka dhahabu kama hazina ya
rasilimali za kigeni kwa sababu ya kuyumba kwa bei ya madini hayo katika
soko la dunia na kusababisha uwezekano wa kupunguza thamani ya hazina
ya rasilimali ya nchi.
Kauli
hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Igunga Mhe.
Dalaly Kafumu aliyehitaji kufahamu sababu za Serikali kukataa kutunza
dhahabu safi katika Benki Kuu wakati Tanzania ni nchi mojawapo
inayozalisha dhahabu safi.
Mhe.
Kijaji amesema kuwa jukumu la msingi la Benki Kuu ni kuandaa na
kutekeleza Sera ya Fedha inayolenga kuwa na utulivu wa bei kwa ajili ya
ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa hivyo ili kufanikisha azma hiyo Benki
Kuu inadhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa kutumia nyenzo mbalimbali
zikiwemo za kuuza dhamana na hati fungani za Serikali pamoja na
kushiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni kati ya mabenki.
“Katika
kutekeleza jukumu lake la msingi, Benki Kuu hutunza hazina ya
rasilimali za kigeni zinazotosha kuagiza bidhaa nje kwa kipindi
kisichopungua miezi minne lakini kwa muda mrefu sasa Benki Kuu ya
Tanzania haiweki dhahabu kama sehemu ya rasilimali hizo kutokana na
kuyumba kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia”, alisema Mhe. Kijaji.
Naibu
Waziri huyo ametoa mfano wa kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la
Dunia ambapo dhahabu ilishuka kutoka dola 1,745 za kimarekani katika
mwezi Septemba 2012 hadi dola za kimarekani 1,068 kufikia mwezi Desemba
2015.
Mhe.
Kijaji amefafanua kuwa hazina ya rasilimali za kigeni zinaweza kuwa
dhahabu – fedha (monetary gold) au fedha za kigeni ambapo uamuzi kuhusu
hazina itunzwe vipi unazingatia vigezo mbalimbali vikiwemo vile vya
kudumisha thamani, wepesi wa kubadilisha pamoja na faida inayopatikana
kwa kuwekeza hazina hiyo.
Aidha,
Mhe. Kijazi amesema kuwa ununuzi na uuzaji wa madini ya dhahabu
unahitaji ujuzi maalum ambapo kwa kuzingatia jukumu la msingi la Benki
Kuu inaonyesha dhahiri kuwa Benki hiyo haijajijengea uwezo katika eneo
la biashara ya madini hayo.
EmoticonEmoticon